HEADER AD

HEADER AD

NATAMANI KUMUONA


Kumuona natamani, mwenye thamani jimboni, 

Mwenye yakini moyoni, ya watu kuwathamini, 

Mwenye uchungu jamani, mwenye kujua thamani, 

Natamani kumuona mbunge mwenye yakini. 


Wa rushwa simtamani, atatuweka shakani,

Simtaki wa sabuni, mwenye kitu mkononi, 

Namtaka wa imani, mwenye nidhamu kazini, 

Natamani kumuona mbunge mwenye yakini. 


Mwenye utu na busara, jimboni ahitajika, 

Na asiye na papara, huyo ndiye namtaka, 

Si wa kuleta hasara, kamwe hatakubalika, 

Natamani kumuona mbunge mwenye yakini. 


Si wa kulala bungeni, vikao vikifanyika, 

Mwenye akili makini, asiwe wa kuropoka, 

Awe mjuzi wa fani, mtatuzi wa hakika, 

Natamani kumuona mbunge mwenye yakini. 


Mwishoni nimefikia, mengi nimehadithia, 

Wasia nimeutoa, kwa moyo safi na nia, 

Ujumbe nimeutoa, kwa shairi kupitia, 

Natamani kumuona mbunge mwenye yakini. 


SirDody

No comments