HEADER AD

HEADER AD

HAWA WANAWAKE HAWA!

Mruhusu akuchune, hutabaki hata ngozi, 
Huo wa kwako unene, utabaki kama panzi, 
Mwanamke we muone, atafilisi kizazi, 
Hawa wanawake hawa, twende nao pole pole.

Wanawake we waone, si kwa rangi wala ngozi,
Wembamba hata wanene, wanajua yao kazi,
Mwanaume ujivune, wanakufungia kazi,
Hawa wanawake hawa, twende nao pole pole.

Hili tukubaliane, maana si upuuzi,
Ukweli huu tuone, na tuufanyie kazi,
Na wao na tushindane, tutayatoa machozi,
Hawa wanawake hawa, twende nao pole pole.

Wawili hao waone, jinsi wametupa kazi,
Hawa wa kwanza muone, ule wake upuuzi,
Asimame asikane, ndiye ametupa kazi,
Hawa wanawake hawa, twende nao pole pole.

Twavuja jasho tuone, magonjwa vifo ni wazi,
Ile bustani nene, laini laini kazi,
Hatuoni hata tone, ni wa kwake ubitozi,
Hawa wanawake hawa, twende nao pole pole.

Ya shetani yamkune, ya Mungu yawe kiazi,
Ulokatazwa unone, kinyume chake Mwenyezi,
Acha kazi zituvune, masika na kiangazi,
Hawa wanawake hawa, twende nao pole pole.

Delila naye muone, ni zaidi ya jambazi,
Kwa Samsoni anune, siri zake ziwe wazi,
Ubembelezi uone, siri kaiweka wazi,
Hawa wanawake hawa, twende nao pole pole.

Akitaka akuchune, hiyo uelewe wazi,
Humuwezi hata tone, akikufungia kazi,
Hata ubaki unune, atakuchekesha wazi,
Hawa wanawake hawa, twende nao pole pole.

Hata mkeo muone, alivyo ni kiongozi,
Usimuonemuone, na japo hajitangazi,
Anaweza akubane, hadi uchakae ngozi,
Hawa wanawake hawa, twende nao pole pole.

Ni vizuri tuwaone, wenzi na tena wapenzi,
Hata wao watuone, kwao twajiweka wazi,
Njia yote tupatane, hata mambo ya uzazi,
Hawa wanawake hawa, twende nao pole pole.

Sio muda tujivune, kufanya mambo kinazi,
Tupinge wasituchune, wakati tunawaenzi,
Pamoja tushikamane, masika na kiangazi,
Hawa wanawake hawa, twende nao pole pole.

Kizuri hiki kione, wanawake ni walezi,
Wema sana uwaone, kwetu siyo wapagazi,
Lakini mtibuane, hasara kwako ni wazi,
Hawa wanawake hawa, twende nao pole pole.

Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

No comments