MLO MZURI NYUMBANI
SUBIRA ya hotelini, siyo kama ya nyumbani,
Chakula cha hotelini, unasubiri mezani,
Wakichelewa nyumbani, waenda hadi jikoni,
Mlo mzuri nyumbani, wakati unaotaka.
Chai kule hotelini, waisubiri mezani,
Yachakatwa kama nini, ni kiduchu kikombeni,
Wakati kule nyumbani, kombe kubwa sebuleni,
Mlo mzuri nyumbanj, wakati unaotaka.
Mwenye mji wa nyumbani, huulizi ule nini,
Na wakati hotelini, sema utakula nini,
Ndipo waende jikoni, na wewe njaa tumboni,
Mlo mzuri nyumbani, wakati unaotaka.
Wataka supu mezani, ya kongolo la buchani,
Wauliza ndiyo nini, si mambo ya hotelini,
Wakati kule nyumbani, majibu yako mekoni,
Mlo mzuri nyumbani, wakati unaotaka.
Hoteli juu na chini, ndizo zatamba mjini,
Chakula kwenda mezani, kwingine oda jikoni,
Huko ni matatizoni, subira hadi jioni,
Mlo mzuri nyumbani, wakati unaotaka.
Mpishi wa hotelini, chumvi nyingi mkononi,
Hapo hamuelewani, kwako chumvi ni ya nini,
Utamu wa ulimini, mdogo kama thumni,
Mlo mzuri nyumbani, wakati unaotaka.
Nimekaa hotelini, chai ifike mezani,
Ningelikuwa nyumbani, ningeifwata jikoni,
Shibe yangu ya jioni, iniweke kivulini,
Mlo mzuri nyumbani, wakati unaotaka.
Mchemsho kwangu dini, yaeleweka nyumbani,
Kuagiza hotelini, madikodiko mezani,
Haya sitaki jamani, kwa afya niko makini,
Mlo mzuri nyumbani, wakati unaotaka.
Niko mbali na nyumbani, utawala u hewani,
Kimya mpole mezani, ndiyo jadi ya ugeni,
Lakini kwangu moyoni, yamenifika shingoni,
Mlo mzuri nyumbani, wakati unaotaka.
Simu iko mkononi, kwajili kesho jioni,
Ntakachokula mezani, nitaagiza njiani,
Ntakapofika mezani, nacho kije kwa sahani,
Mlo mzuri nyumbani, wakati unaotaka.
Ubeti niko mwishoni, chakula chaja mezani,
Swaumu kali tumboni, iko mapumzikoni,
Nabugia mdomoni, nende zangu kitandani,
Mlo mzuri nyumbani, wakati unaotaka.
Hoteli barabarani, hilo nimeshaamini,
Amani iko nyumbani, mjini na kijijini,
Chakula wakibaini, bila nini wala nini,
Mlo mzuri nyumbani, wakati unaotaka.
Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Post a Comment