HEADER AD

HEADER AD

KHADIJA RUNGWE MAARUFU MTOTO WA MZEE WA UBWABWA AMESEMA AKICHAGULIWA ATATATUA CHANGAMOTO KIBAHA MJINI

  

>>Asema baba yake wakati akigombea urais alikuja na sera ya ubwabwa lakini watu hawakuielewa

Na Gustaphu Haule, Pwani

MGOMBEA wa ubunge Jimbo la Kibaha Mjini kupitia Chama Cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) Khadija Hashim Rungwe ambaye ni mtoto wa mzee wa ubwawa Hashimu Rungwe amewaomba Wananchi wa Kibaha Mjini kumchagua kuwa mbunge ili aweze kutatua changamoto mbalimbali zilizopo katika Jimbo hilo.

Khadija ametoa ombi hilo wakati akizungumza na wananchi wa Kibaha katika mkutano wake wa uzinduzi wa Kampeni uliofanyika Septemba 20, 2025 katika viwanja vya Kata ya Picha ya Ndege vilivyopo katika Manispaa ya Kibaha mkoa wa Pwani.

Khadija aliambatana na baba yake mzazi Hashimu Rungwe ambaye ni mwenyekiti wa Taifa wa CHAUMMA amesema anazitambua changamoto za Kibaha Mjini ndio maana ameona aingie kugombea ubunge ili awasaidie Wananchi hao.

Amesema kuwa Kibaha Mjini imekaa kama mtoto ambaye hana muelekeo na sasa wamchague yeye kuwa mbunge kwakuwa ana sababu za msingi na anatosha kuwa mbunge wa jimbo la Kibaha Mjini.

Amesema anatambua Kibaha ina changamoto nyingi ikiwemo ya watoto kutomaliza shule kutokana na sababu mbalimbali na kwamba akishakuwa mbunge atahakikisha anafuatilia kujua sababu za wanafunzi kutomaliza shule na kuona namna ya kuwasaidia ili warudi shule kusoma.

Pia amesema kuna changamoto sekta ya afya kwani hospitali zinalalamikiwa kukosa dawa na hata gharama za matibabu ni kubwa na kwamba kama binadamu hana uhakika wa matibabu ni wazi kuwa wananchi wanateseka.
   Mgombea ubunge Jimbo la Kibaha Mjini kupitia Chama Cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA)Khadija Rungwe akiwa katika uzinduzi wa kampeni zake zilizofanyika Septemba 20,2025 katika Kata ya Picha ya Ndege Manispaa ya Kibaha Mkoa wa Pwani.

Ameongeza kuwa anatambua Jimbo la  Kibaha Mjini barabara zake ni mbovu na wakati wa mvua hazipitiki kwahiyo akichaguliwa atakwenda kuzisimamia changamoto hizo na kuhakikisha anawaletea wananchi maendeleo.

Amewaambia wafanyabiashara kwamba anajua kuna changamoto ya masoko na wakati mwingine wanapata shida ya kuhamishwa hamishwa katika maeneo yao bila sababu hali ambayo inasababisha kukwamisha maendeleo ya biashara zao 

Amesema wakimchagua kuwa mbunge  atakwenda kulisimamia hilo na ikiwezekana atatengeneza sehemu maalum ya kila mwananchi kutoa maoni yake.

"Ndugu zangu wananchi wa Jimbo la Kibaha mimi mkinichagua sitokuwa mbunge wa kusinzia bungeni na hata kusubiri niletewe shida za watu ofisini bali nitakuwa natoka mwenyewe kwenda katika Kata na mitaa kwa ajili ya kujua shida na changamoto za wananchi ili niweze kuzitafutia ufumbuzi,"amesema Khadija.

Ameongeza kusema kwamba  Mwenyekiti wa CHAUMMA Taifa , Hashim Rungwe alikuja na sera ya ubwabwa lakini watu hawakumuelewa lakini maana yake ilikuwa ni kuwahakikishia watanzania kupata chakula cha uhakika, kwahiyo akichaguliwa atasimamia suala la chakula kwa wananchi wake kwani kukiwepo na chakula mambo mengine pia yataenda sawa.

Naye mgombea wa udiwani wa Kata ya Kibaha kupitia CHAUMMA , Hamo Machapula amewaambia wananchi wasichague mtu kwasababu ya maslahi yake binafsi na familia yake na wala wasichague mtu kwa ajili ya kuendeleza biashara zake .

        Mgombea udiwani Kata ya Kibaha kupitia Chama Cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) Hamo Machapula akizungumza katika uzinduzi wa kampeni za ubunge Jimbo la Kibaha Mjini zilizofanyika Septemba 20,2025 katika Kata ya Picha ya Ndege na kushoto ni Khadija Rungwe mgombea ubunge Jimbo la Kibaha Mjini.

Machapula amesema kuwa wananchi wasitishwe eti wakichagua CHAUMMA watakosa maendeleo katika Jimbo la Kibaha Mjini kwani maendeleo hayaletwi na CHAUMMA wala CCM maendeleo yanaletwa na Serikali.

Amesema wamchague Khadija Rungwe kwa maendeleo kwani viongozi wa CCM hawapo kwa ajili ya maendeleo bali wapo kwa ajili ya maslahi yao binafsi .

Naibu Katibu Mkuu wa CHAUMMA Benson Kigaila amesema kuwa Khadija anafahamu shida za Kibaha ,anajua shida za  miundombinu ya barabara ambazo mvua ikinyesha watu wanabeba viatu mkononi.

      Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Ukombozi wa Umma( CHAUMMA) Benson Kigaila (Kulia) akimnadi mgombea wa ubunge wa Jimbo la Kibaha Mjini kupitia chama hicho Khadija Rungwe (kushoto) katika uzinduzi wa kampeni uliofanyika Septemba 20,2025 Kata ya Picha ya Ndege Manispaa ya Kibaha

" Anajua vijana wanahitaji mikopo lakini anajua mikopo hiyo hawaipati badala yake wanaenda kwenye mikopo ya kausha damu. Khadija anajua kwenye shule madarasa hayatoshi ,wanafunzi wanakaa chini  kwa kukosa madawati,walimu wachache na anajua ipo michango mingi shuleni kana kwamba Wananchi hawalipi kodi" amesema.

Amesema  Khadija anajua hospitali za Serikali zipo chache na zilizopo hazina watumishi wala dawa za kutosha na ukienda unaandikiwa cheti ukanunue dawa katika maduka binafsi na anajua changamoto wanayokutananayo wajawazito.

Amewasisitiza wananchi kuwa Oktoba, 29, 2025 watoke nyumbani waende kuchagua CHAUMMA na wachague mabadiliko huku akisema Khadija Hashim Rungwe ndio mtu sahihi kwa Jimbo la Kibaha Mjini.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa CHAUMMA Taifa Hashim Rungwe amesema kuwa zama za CCM zimekwisha na sasa wafanye mabadiliko ya kuhakikisha wanamchagua kijana mwenzao Khadija Rungwe ili aende Bungeni akawasemee changamoto zao.



No comments