MWANAHARAMU

Mwanaharamu apite,
Na cheo kile apate,
Makubwa na yamkute,
Abakie anatweta.
Baba haramu ajute,
Watoto na wamsute,
Misaada waifute,
Abakie anajuta.
Nyumbani kwake akute,
Pesa za kula achote,
Mbili tatu azipate,
Cha kula nyumbani hata.
Mama haramu asote,
Atupe mwana ajute,
Mwingine asimpate,
Abakie anajuta.
Fisadi na aipate,
Hatia na imkute,
Mali zake wazipate,
Abakie anajuta.
Kifungo na akipate,
Ni mafunzo ayapate,
Kutoka huko ajute,
Mkia akiufyata.
Mvivu njaa ajute,
Chakula na asipate,
Akili mpya apate,
Kazi ende kutafuta.
Muache ndoto aote,
Shuka late alivute,
Njaa na imkong’ote.
Abakie anajuta.
Mwongo aibu apate,
Wakumsuta apate,
Hata nje asitoke,
Abakie anajuta.
Mnafiki aipate,
Aumbuke atepete,
Masikio wamvute,
Abakie anajuta.
Mtaka sifa apate,
Duniani na apete,
Mbinguni tusimkute,
Abakie anajuta.
Kimbelembele ajute,
Mambo yake wamtete,
Atakacho asipate,
Abakie anajuta.
Mchawi na tumfute,
Na kichaa kimpate,
Mtu asimkamate,
Akatubu kwa kujuta.
Muuaji asipite,
Silaha asizipate,
Na watu asiwakute,
Ashikwe anatepeta.
Mzinzi aone pete,
Ndoa yake imsute,
Atongoze asipate,
Huyu ni wa kumsuta.
Mbaya wako mfute,
Mbele yako asipite,
Laana na impate,
Aache kufwatafwata.
Akilizo azichote,
Kwazo mali akapate,
Akija asikukute,
Na ayapate matata.
Nafasi mbawa iote,
Ya kwako asiipate,
Ibaki kwako ni kete,
Abaki anajing’ata.
Wabaya uwakung’ute,
Waondoke kwako wote,
Wema ndiyo uwapate,
Pamoja muweze pita.
Mabaya wayatafute,
Ili kazi wakufute,
Cheo chako wakipate,
Wabaki wametepeta.
Eti hali iwe tete,
La kukucheka wapate,
Kama ni ndoto waote,
Dua halitakupata.
Mungu wako mtafute,
Wakija na wampate,
Pa kudhuru wasipate,
Msalama iwe chata.
Kwa Mungu wako wavute,
Na Neno waliokote,
Wajisachi na wajute,
Njia mbaya wanapita.
Hata wengine walete,
Mungu wako wampate,
Neema na iwapate,
Huko ni kushinda vita.
Wakosa wote wajute,
Amani wasiipate,
Toba kwa Mungu wapate,
Furaha waweze pata.
Kila mtu na apate,
Ya kwake na ayaokote,
Ya wengine asipate,
Shida asije kupata.
27. Haramu ile yoyote,
Itakacho isipate,
Sifuri iiokote,
Kote kuwe ni kujuta.
Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
 
 
 
 
Post a Comment