TAKUKURU PWANI YAOKOA FEDHA ZA WANANCHI WA KITONGOJI CHA NYAKAHAMBA

Na Gustaphu Haule, Pwani
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mkoa wa Pwani imefanikiwa kurejesha tabasamu kwa Wananchi wa Kitongoji cha Nyakahamba kilichopo Kata ya Kerege Wilayani Bagamoyo baada ya kuokoa fedha za Wananchi hao kiasi cha Tsh. 1,376,250.
Fedha hizo walikuwa wametozwa na Mwenyekiti wa Kitongoji hicho kwa ajili ya kulipia maji ambayo mkanadarasi alishalipwa.
Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Pwani Domina Mukama,ametoa taarifa hiyo Septemba 11,2025 kwa Waandishi wa habari ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo katika kipindi cha Aprili hadi Juni ,2025.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Pwani Domina Mkama.Mukama amesema kuwa kazi hiyo ilifanyika katika mradi wa upanuzi wa vituo vya kutekea maji kwenye Kitongoji cha Nyakahamba Kata ya Kerege wenye thamani ya Sh.milioni 60.
Amesema kuwa katika mradi huo, kazi zilizopangwa kutekelezwa ni pamoja na kulaza mabomba na shughuli mbalimbali za uunganishaji( Fitting) na ujenzi wa vituo vitatu vya kutekea maji.
Ameongeza kuwa katika Tsh. Milioni utekelezaji wa mradi huo Wananchi walikuwa wakilalamika ukusanyaji wa fedha usio halali ambapo baada ya kupata taarifa hiyo TAKUKURU ikaanza kufanyia kazi malalamiko hayo.
Amesema baada ya TAKUKURU kuingilia kati walibaini kuwa wananchi hao hawakustahili kulipia maji katika kipindi cha majaribio kwani mkanadarasi alikuwa ameshalipwa gharama za maji kabla ya kukabidhi mradi huo kwa Ruwasa Kata ya Mapinga .
Amesema fedha za Wananchi zilizorejeshwa na TAKUKURU zitarudishwa kwa Wananchi wa Kitongoji cha Nyakahamba ili ziweze kuwanufaisha kulipia gharama za maji mara baada ya mkandarasi atakapokuwa amekabidhi mradi huo Ruwasa kwa ajili ya uendeshaji.
Jengo la ofisi ya Takukuru Mkoa wa Pwani lilipo katika Halmashauri ya Manispaa ya KibahaMukama amesema kuwa TAKUKURU mkoa wa Pwani imeendelea na ufuatiliaji matumizi ya fedha za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kwamba tayari wamefuatilia zaidi ya Sh.bilioni 32 katika miradi ya maendeleo 40 kutoka sekta ya Elimu, Afya na Barabara.
Kuhusu suala la elimu kwa umma Mukama amesema kuwa ushirikiano wa wadau na TAKUKURU katika mapambano dhidi ya rushwa umeongezeka na wananchi wamekuwa na uelewa wa madhara ya rushwa katika jamii.
Amesema uelewa wa Wananchi hao imetokana na kutoa elimu ya masuala mbalimbali ya rushwa tuliyoitoa kupitia semina 42, Mikutano ya hadhara 39, vipindi vya redio vitatu, Uimarishaji Klabu za wapinga rushwa 77, na uandishi wa makala 12 .
Kwa upande wa uchunguzi wa mashtaka katika kipindi cha Aprili hadi Juni TAKUKURU mkoa wa Pwani imepokea taarifa 29 kati ya hizo taarifa 16 hazikuhusu vitendo vya rushwa na taarifa 13 zilihusu vitendo vya rushwa ambazo zinashughulikiwa na zipo katika hatua mbalimbali.
Amesema upande wa mashtaka kesi mpya zilizofunguliwa 14 na zinazoendelea Mahakamani 24 ambapo kati ya hizo kesi 17 ziliamuliwa na Jamhuri ilishinda kesi 15 na kesi mbili Jamhuri haikushinda.
Mukama amesema kuwa TAKUKURU Mkoa wa Pwani imeweka mikakati mbalimbali ya kutoa elimu ya madhara ya rushwa katika uchaguzi mkuu kupitia semina , mikutano ya hadhara na vipindi vya redio ili kuwafikia wadau wote wanaoshiriki katika uchaguzi.
"Lengo ni kushiriki uchaguzi usiokuwa na vitendo vya rushwa Oktoba 2025 na ndio maana Takukuru inaendelea na majukumu ya uzuiaji, uchunguzi na kuendesha mashauri ya rushwa Mahakamani kulingana na Sheria,"amesema Mukama.
Hata hivyo,Mukama ametoa wito kwa Wananchi wa Mkoa wa Pwani, watumishi na wadau wote kuendelea kuunga mkono jitihada za mapambano dhidi ya rushwa ikiwa pamoja na kuwafichua watu wanaoshiriki kufanya vitendo vya rushwa kwa kutoa taarifa sahihi zitakazowezesha kuwachukulia hatua wahusika.



Post a Comment