TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA YAWAPIGA MSASA WAANDISHI WA HABARI MARA

>>Kamishna Masanja akumbusha haki ya kupata taarifa , kukusanyika
>> Asema wanaowaweka watu ndani zaidi ya saa 24 wanakiuka haki za Binadamu na utawala bora
>> Waandishi wa habari watakiwa kuandika ukweli
DIMA Online , Musoma
TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nchini, imetoa elimu ya haki na wajibu kwa Waandishi wa habari mkoa wa Mara huku ikiwasisitiza kuandika ukweli kwani wao ni wasimamizi wa haki za wanyonge.
Pia Tume hiyo imetoa elimu ya haki muhimu wakati wa uchaguzi ikiwemo kuchagua na kuchaguliwa, haki ya kupata taarifa, uhuru wa kujieleza, uhuru wa kukusanyika na kutokubaguliwa, wajibu wa wananchi wakati wa uchaguzi na umuhimu wa kushiriki uchaguzi.
Akizungumza na Baadhi ya Waandishi wa habari wakati wa mafunzo ya siku moja yaliyofanyika ukumbi wa Jeshi la Polisi mkoa wa Mara, Kamishna wa haki za Binadamu na utawala bora nchini kutoka makao makuu Dodoma, Dkt. Thomas Masanja amesema lengo la Tume hiyo ni kulinda , kuhifadhi na kuendeleza haki za Binadamu.
Kamishna wa haki za Binadamu na utawala bora nchini kutoka makao makuu Dodoma, Dkt. Thomas Masanja akiwapiga msasa waandishi wa habari mkoani Mara, Septemba 19, 2025 mjini Musoma.
Dkt. Masanja amewataka waandishi wa habari kushirikiana na Tume hiyo kutoa taarifa pindi kunapotokea ukiukwaji wa haki za Binadamu na utawala bora huku akikemea kitendo cha baadhi ya viongozi kuweka watu ndani zaidi ya saa 24.
" Mkuu wa wilaya , mkuu wa mkoa na mtendaji wa Kijiji ama Kata anaruhusiwa kumweka mtu ndani saa 24 tu zaidi ya hapo anakuwa amekiuka haki za Binadamu, hivyo unatakiwa kulalamika tume ya haki za binadamu.
Baadhi ya Waandishi wa habari mkoani Mara wakiwa katika picha ya pamoja na maafisa wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora .
" Malalamiko yanaweza kuwa ya uvunjifu wa haki za Binadamu , ukiukwaji wa misingi ya utawala bora, mwenendo wa mtu yeyote au taasisi yoyote katika kutekeleza madaraka au utekelezaji unaokiuka madaraka.
" Pia matumizi au matendo ya watu wenye madaraka katika utumishi wa serikali kuu, serikali za mitaa , mashirika , makampuni ya umma, vyombo binafsi na watu binafsi kuhusu matumizi mabaya ya madaraka, kutotenda haki au kuonewa" amesema Kamshina Dkt.Thomas .
Akizungumzia haki muhimu wakati wa uchaguzi, Kamishna Dkt .Thomas amesema kila raia mwenye sifa anastahili kushiriki uchaguzi kuchagua na kuchaguliwa bila vizuizi visivyo halali, wananchi wana haki ya kupata taarifa za kuaminika kuhusu wagombea , vyama na taratibu za uchaguzi.
Waandishi wa habari wakiwe kwenye mafunzo ya siku moja ya masuala ya Haki za Binadamu na Utawala Bora .
" Wananchi , vyama vya siasa na vyombo vya habari wana haki ya kutoa maoni kuhusu masuala ya uchaguzi yaani uhuru wa kujieleza, wananchi wana haki ya kukusanyika ikiwemo kushiriki mikutano ya kampeni na mijadala ya kisiasa.
"Pia kutobaguliwa makundi yote katika jamii yakiwemo ya wanawake , vijana na watu wenye ulemavu , wanapaswa kushiriki uchaguzi kwa usawa" amesema Kamishna Dkt.Thomas .
Afisa sheria Tume ya haki za Binadamu na Utawala Bora, Majid Kangile amewahimiza waandishi wa habari kuandika habari kwa kuzingatia kanuni za maadili ya uandishi wa habari hususani katika kipindi hiki cha uchaguzi.
Amezitaja kanuni hizo ni pamoja na kuandika ukweli , wajibu na uwajibukaji, haki na usawa, kutoandika habari za uongo, kumheshimu faragha na utu wa mtu, kuwalinda watoto , kutoandika habari za ubaguzi na kauli za chuki.
Afisa sheria wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Irene Ishengoma amewataka waandishi wa habari kuwa makini katika utoaji wa habari kwasababu kwa kipindi hiki cha uchaguzi habari za siasa zinafuatiliwa na kutizamwa sana .
Afisa sheria wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Irene Ishengoma akitoa elimu kwa waandishi wa habari mkoa wa Mara.
" Tujitahidi hata vichwa vya habari vibebe ujumbe uliopo ndani , tutoe habari ambazo zitajenga uaminifu kwa walaji wa habari, tujitahidi kuandika habari ambazo hazitaharibu heshima ya mtu " amesema Irene.
Naye Mkaguzi mkuu wa ndani Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora , CPA Joel Kahesi, amesema waandishi wa habari ni wasimamizi wa haki za wanyonge huku akirejea katika maandiko matakatifu ya kitabu cha Mithali 31 : 9 .
Mkaguzi mkuu wa ndani Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora , CPA Joel Kahesi akitoa mafunzo kwa waandishi wa habari mkoa wa Mara.
" Kitabu hicho kinasema ; fumbua kinywa chako, uhukumu kwa haki; uwapatie masikini na wahitaji haki yao. Waandishi wanatoa taarifa kwa ajili ya wale wasio na sauti ya kusema. Kitabu cha Waefeso 5 : 9-13 kinasema; kwakuwa tunda la nuru ni katika wema wote na haki na kweli; mkihakiki ni nini impendezayo Bwana .
Bibilia katika kitabu hicho inasema wala msishirikiane na matendo yasiyozaa ya giza, bali myakemee , kwakuwa yanayotendeka kwao kwa siri, ni aibu hata kuyanena . Lakini yote yaliyokemewa hudhihilishwa na nuru maana kila kilichodhihirika ni nuru" amesema CPA Joel.
Dira
>> Kuwa Taasisi ya Kitaifa ya Haki za Binadamu inayoaminika kuongoza jamii kufurahia haki za Binadamu, kuzingatia misingi ya utawala bora na kuheshimu utu wa watu.
Dhamira
>> Kuiongoza Jamii kuwa ya haki kupitia ukuzaji, ulinzi na utunzaji wa haki za Binadamu na misingi ya utawala bora kwa kushirikiana na wadau.
Post a Comment