WAKATI Tanzania inajiandaa kwa uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, taifa hilo linakabiliana na mchanganyiko wa hisia na matarajio.
Ripoti ya mwaka 2025 ya Country Governance and Government Index (CGGI) imeiweka Tanzania miongoni mwa nchi 10 bora barani Afrika kwa viwango vya utawala bora, ikiwa ya sita barani Afrika na ya 78 duniani.
Matokeo haya yameibua mjadala mkubwa ndani ya nchi: wafuasi wa serikali wanayataja kama ushahidi wa mafanikio ya kiutawala, huku wanaharakati na wapinzani wakihoji hali halisi ya demokrasia na uwajibikaji wa kisiasa.
Uchaguzi ujao unaleta kipimo kingine cha moja kwa moja cha kimataifa na hisia za utawala bora iwapo huo utawala bora unaonekana kwa vitendo katika maisha ya wananachi ya kila siku.
Vigezo vinavyopimwa na CGGI na utaratibu wa tathmini
Ripoti ya CGGI hupima utawala bora kwa kuzingatia vipengele vitatu vikuu: utendaji wa sera, uthabiti wa taasisi za umma, na uwajibikaji wa serikali kwa wananchi.
Utendaji wa sera unahusisha uwezo wa serikali kusukuma mbele mipango ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi, taasisi zinapimwa kwa uthabiti wa kutoa huduma bila kuathiriwa na misukosuko ya kisiasa, na uwajibikaji wa umma unahusiana na uwazi, ushirikishwaji wa wananchi, na usimamizi wa rasilimali.
Utaratibu wa CGGI unategemea takwimu za muda mrefu, kuanzia miaka mitatu hadi mitano, kutoka kwa mashirika huru za kimataifa, taasisi za utafiti, na vyuo vikuu.
Kwa kutumia takwimu hizi, ripoti inatoa picha ya mwenendo wa muda mrefu wa utawala badala ya kuzingatia matukio ya kisiasa ya muda mfupi.
Hivyo, ingawa alama ya CGGI inaweza kuonyesha maendeleo, haiwezi kupima kwa kina hisia za wananchi kuhusu hali halisi ya kisiasa, hasa wakati nchi inajiandaa kushiriki katika uchaguzi muhimu kama wa Oktoba 29.
Nini maana ya hatua hii?
Matokeo ya CGGI yanatoa picha ya Tanzania kama taifa linalojitahidi kuimarisha taasisi zake na sera za kiutendaji, jambo linaloongeza hadhi ya nchi kimataifa na kuvutia wawekezaji.
Uchaguzi huu ni kipimo kingine halisi cha jinsi wananchi wanavyohisi uwazi, uwajibikaji, na nafasi yao katika mchakato wa kisiasa.
Kwa mujibu wa mtandao wa PolicyForum, unaeleza utawala bora ni mfumo wa kutumia mamlaka kwa njia inayozingatia uwazi, uwajibikaji, ushirikishaji, ufanisi, tija, uadilifu, usawa, na utawala wa sheria, kwa lengo la ustawi wa wananchi na matumizi sahihi ya rasilimali, fedha, na madaraka.
Kwa ujumla, nafasi ya Tanzania katika CGGI ni utekelezaji wa misingi hii inayotajwa na PolicyForum. Licha ya kukosolewa mara kadhaa kuhusu utawala wa sheria kuweka katika nafasi ya juu kimataifa ni ishara nyingine ya mafanikio ya kiutawala kwa Tanzania.
Kwa mfano kiongozi wa chama kikuu cha upinzani Tanzania, CHADEMA, Tundu Lissu, kuwa jela kwa tuhuma za uhaini, kesi yake inajadiliwa zaidi kwa muktadha wa utawala bora.
Tafsiri nyingine ya kiwango cha utawala bora cha Tanzania ni kuonyesha kuwa safari ya mjadala wa utawala bora ni mchakato unaohitaji kuunganisha tathmini za kimataifa na hali halisi ya wananchi. Na kwa hayo uchaguzi wa Oktoba 29 unatoa fursa nyingine ya kupima kwa vitendo jinsi alama hizi zinavyolingana na hisia halisi za wananchi.
Nini kinaifanya Tanzania kuwa kinara utawala bora?
Kwa mujibu wa vigezo ni kwamba Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuimarisha mifumo ya ukusanyaji mapato na uwazi wa bajeti, hatua ambazo zimeongeza ufanisi wa serikali na kupunguza upotevu wa fedha za umma.
Ukuaji wa uchumi kwa wastani wa zaidi ya asilimia 5 kila mwaka, na udhibiti wa mfumuko wa bei ni sababu ya Tanzania kuwa ilipo kwenye viwango vya utawala bora. Vigezo vinataja pia uwekezaji katika huduma za afya, elimu, na miundombinu ya kijamii, ikiwa ni pamoja na reli na barabara, umeongeza uthabiti wa kiutendaji wa taifa na kuonyesha maendeleo yanayogusa moja kwa moja wananchi.
Waziri wa Sheria na Katiba, Dkt. Damas Ndumbaro, aliwahi kutoa picha ya masuala ya haki za binadamu na utawala bora Tanzania: "Chombo cha kisheria cha kusimamia haki za binadamu Tanzania, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kimepata heshima daraja A na waangalizi mahususi wa kimataifa, daraja A ndilo la juu zaidi, kwamba chenyewe na nchi yote inakwenda vizuri, tuachane na propaganda."
Hata hivyo, haya yanayotajwa yanaleta maswali. "Ni kweli tumepiga hatua katika kuboresha demokrasia na utawala bora? anauliza Onesmo Mushi, kupitia mtandao wa X.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan .
Wengi wa wapinzani, wanaharakati wa kiraia, na baadhi ya wachambuzi huru wanasisitiza kuwa bado kuna changamoto kubwa katika demokrasia, uhuru wa vyombo vya habari, na heshima kwa haki za kiraia.
Hata Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Tanzania inakiri kuwa bado kuna changamoto kadhaa zinazokwamisha utawala bora ikiwemo rushwa ingawa hatua zimechukuliwa kupunguza tatizo, kukosekana kwa ushirikishwaji na ukosefu wa uwajibikaji kwa baadhi ya sekta za umma.
Rais wa chama cha wanasheria Tanzania, Boniface Mwabukusi hivi karibuni alieleza umuhimu wa kuweka mifumo thabiti inayohakikisha heshima ya utawala wa sheria, uwajibikaji na uwazi pamoja na ushiriki wa wananchi.
Rais wa chama cha wanasheria Tanzania, Boniface Mwabukusi
Hoja hizi zinatokana na changamoto zilizoko zinazoibua maswali kuhusu utawala bora Tanzania, kufuatia kuripotiwa kwa matukio yanayoashiria uvunjifu wa haki za binadamu ikiwemo masuala ya utekaji, ambayo Polisi mara kadhaa imesisitiza kuyafanyia kazi, yakiwemo ya wale watu wanaodaiwa kujiteka.
"Maswali ni lazima likiwemo hili la je, alama nzuri ya kimataifa ya Tanzania kwenye utawala bora, inalingana na hali halisi ya kisiasa na hisia za wananchi? jibu lolote utakalopata, linagusa uelewa kwa sababu vigezo vya kimataifa vinavyotumika kupima utawala bora vinaipa Tanzania nafasi hiyo, pengine hoja ya hali halisi ni kutizama kwa namna ingine", anasema Rehema Mema, mwanahabari wa siasa na utawlaa bora.
Kwa muktadha wa anayoyasema Rehama, uchaguzi wa Oktoba 29 unatoa kipimo cha moja kwa moja cha jinsi mambo yanavyoweza kupimwa ndani na nje ya nchi, bila kuathiri misingi ya utawala bora.
Post a Comment