AMEKUFA NA KINYONGO
AMEKUFA na kinyongo, ndivyo wengi twaamini,
Kutotinga kwa ulingo, alivyokwenda vitani,
Mambo yalifanywa fyongo, kumkandamiza chini,
Kweli hapa duniani, hivipati vyote vyako.
Nasema kwenye siasa, alivyokuwa makini,
Kama mtu wa hamasa, ikulu pawe nyumbani,
Lakini amepakosa, hadi kwenda kaburini,
Kweli hapa duniani, huvipati vyote vyako.
Raila jela lifungwa, hata kwenda ugenini,
Jinsi alisongwasongwa, kwamba abakie chini,
Licha ya kote kupingwa, lizidisha upinzani,
Kweli hapa duniani, huvipati vyote vyako.
Chaguzi za vyama vingi, na yeye mashindanoni,
Alivyoupiga mwingi, angelifika enzini,
Lakini vingi vigingi, akabaki pembezoni,
Kweli hapa duniani, huvipati vyote vyako.
Hadi akajiapisha, tena mbele hadharani,
Hasira akaonesha, kotekote duniani,
Wapi kulimfikisha, hakufika kileleni,
Kweli hapa duniani, huvipati vyote vyako.
Licha ya kuwa pembeni, wala si serikalini,
Hakubaki asilani, kubwaga manyanga chini,
Lizidi kuwa kazini, hadi kufika mwishoni,
Kweli hapa duniani, huvipati vyote vyako.
Raila na wengi wafu, wameenda kaburini,
Pamoja na kuwasifu, wanafaa kileleni,
Kama kura ya turufu, hawakutinga kitini,
Kweli hapa duniani, huvipati vyote vyako.
Yabaki historia, ya Raila duniani,
Alivyotutumikia, hata kukawa amani,
Pale alipoingia, tukaishi kivulini,
Kweli hapa duniani, huvipati vyote vyako.
Kwao aliitwa baba, heshima kubwa jamani,
Kwa wengine huyo baba, aliushika mpini,
Akisema walishiba, hata kwenda mzigoni,
Kweli hapa duniani, huvipati vyote vyako.
Unayoyatekeleza, ukiwapo duniani,
Ndiyo yatakueleza, ukitoka duniani,
Vema ukajiongoza, ubakie midomoni,
Kweli hapa duniani, huvipati vyote vyako.
Raila ameondoka, toka kwetu duniani,
Jinsi aliwajibika, anabaki maishani,
Mema yake tutashika, hasa kusaka amani,
Kweli hapa duniani, huvipati vyote vyako.
Angelikuwa Rais, muda Fulani zamani,
Ila hakuwa Rais, ni mambo ya duniani,
Taasisi ya Rais, kupata ngumu jamani,
Kweli hapa duniani, huvipati vyote vyako.
Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
Post a Comment