HEADER AD

HEADER AD

BILIONI 19.8 KUTUMIKA KUJENGA SOKO LA MNARANI, MIUNDOMBINU YA BARABARA KIBAHA

Na Gustaphu Haule ,Pwani

HALMASHAURI ya Manispaa ya Kibaha mkoani Pwani imesaini mikataba na kampuni ya M/S Dimetoclasa Real Hope Limited kwa ajili ujenzi wa mradi wa soko la Mnarani na  ujenzi wa miundombinu ya barabara wenye thamani ya zaidi ya Sh.bilioni 19.8.

Hafla hiyo imefanyika Septemba 25,2025 katika viwanja vya stendi ya Loliondo vilivyopo Mtaa wa Tangini Kata ya Tangini katika Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Mkoani Pwani kupitia mkurugenzi wa Manispaa hiyo Dkt.Rogers Shemwelekwa na kampuni hiyo.

        Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa (Kulia) akionyejsha mkataba wa ujenzi wa Soko la Mnarani uliosainiwa kati yake na kampuni ya Dimetoclasa Real Hope Limited.

Mradi huo ni kati ya miradi ya TACTIC inayofadhiliwa na Serikali kuu kupitia mkopo wa Benki ya dunia wenye thamani ya dola za kimarekani milioni 410 ambapo Manispaa ya Kibaha ni moja kati ya wanufaika 45 wa mradi huo.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa mkataba huo Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema lengo la mradi huo ni pamoja na kutoa huduma bora kwa wananchi waweze kupata bidhaa katika sehemu salama.


        Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akizungumza katika hafla ya kutiliana Saini ya mikataba ya ujenzi wa Soko la Mnarani lililopo Katika Manispaa ya Kibaha.

Kunenga amemtaka mkandarasi huyo Dimetoclasa Real Hope Limited  anayetekeleza mradi huo kuzingatia muda uliowekwa ili wafanyabiashara waweze kuendelea na biashara zao katika eneo hilo.

Aidha, Kunenge amewataka wananchi kuwa walinzi wa vifaa vitakavyotumika katika mradi huo kuepusha hasara ambazo zinaweza kuchelewesha mradi.

Kunenge amesema mradi huo ni sehemu ya kuongeza  kipato kwa wakazi wa Manispaa ya Kibaha na kuongeza ajira lakini amesema lazima mradi huo ukikamilika wahusika na Soko hilo wapewe kipaumbele.

Mwenyekiti wa Soko la Mnarani Mohamed Mnembwe amesema anamshukuru wa kupata mradi huo mkubwa kupitia  Rais Dkt .Samia Suluhu Hassan ambao aliona kuwa Wananchi wa Kibaha wanahitaji soko.

      Mwenyekiti wa Soko la Mnarani Mohamed Mnembwe akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa ujenzi wa Soko jipya la Kisasa ,hafla hiyo ilifanyika katika viwanja vya stendi ya Loliondo Manispaa ya Kibaha.

Amesema kuwa  baada ya kupata taarifa za mradi huo wafanyabiashara walihupokea kwa mikono miwili na hivyo kuamua kutoa ushirikiano wa kuhama katika eneo hilo ili kusudi mradi uweze kuanza kutekelezwa na kwamba anawapongeza  wafanyabiashara hao kwa kukubali kuhama sambamba na uvumilivu waliokuwanao.

Mwakilishi wa mtendaji mkuu wa wakala wa barabara za mjini na vijijini (TARURA) mhandisi Emmanuel Myanga ,amesema mradi wa Tactic ni mojawapo ya miradi inayofadhiliwa na Serikali Kuu kupitia mkopo wa Benki ya Dunia wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 410.

Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (TARURA ) Mhandisi Emmanuel Mnyanga akizungumza katika hafla ya kutiliana Saini mikataba ya ujenzi wa Soko la Mnarani pamoja na barabara za lami katika Kata ya Tangini hafla ambayo ulifanyika viwanja vya Loliondo.

Myanga amesema  malengo ya mradi huo ni kuboresha miundombinu ya Miji 45 ya Tanzania pamoja na kujengea uwezo Halmashauri ili ziweze kujiimarisha katika usimamizi wa uendelezaji Miji pamoja na ukusanyaji wa mapato.

Amesema Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha ipo katika utekelezaji wa kundi la pili inayojumuisha Miji 15 ambapo kwa Kibaha tayari imekamilisha taratibu za zabuni na wamesaini mikataba na wakandarasi walioshinda zabuni ili ujenzi uanze maramoja.

Amesema kuwa katika Manispaa ya Kibaha miradi inayotarajiwa kutekelezwa kwa sehemu ya kwanza ni pamoja na ujenzi wa barabara inayoanzia Tughe kwenda katika Kanisa la Anglikani yenye urefu wa (Km 1.1),barabara ya Picha ya Ndege kuelekea hospitali ya Lulanzi,(Km.3.7)ujenzi wa Soko la Mnarani na uboreshaji wa bustani ya mapumziko.

      Baadhi ya wananchi na wakuu wa taasisi za Serikali wakishuhudia hafla ya utiaji saini wa mikataba ya ujenzi wa Soko la Mnarani pamoja na ujenzi wa barabara za lami katika Manispaa ya Kibaha, hafla hiyo imefanyika katika viwanja vya Loliondo.

Amesema kigezo kilichotumika kuwapata wanufaika wa mradi huo ni taarifa ya idadi na kiwango cha ongezeko la watu kutoka ofisi ya Taifa ya Takwimu( NBS) ambapo kwa upande wa Manispaa ya Kibaha mradi uliosainiwa Septemba 25/2025 utaanza kutekelezwa Oktoba 1,2025 na utachukua muda wa miezi 15 hadi kukamilika.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Pili Mnyema anaishukuru Serikali kwa kazi kubwa inayoendelea kufanya hasa katika Manispaa ya Kibaha na katika mradi huo Pwani imenufaika katika Wilaya mbili ikiwemo Kibaha na Bagamoyo.

       Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Pili Mnyema akizungumza katika hafla ya kutiliana Saini ya mikataba Kuhusu ujenzi wa Soko la Mnarani lililopo Katika Manispaa ya Kibaha.

Mnyema amesema kukamilika kwa mradi huo itasaidia kupanuka kiuchumi kwa wafanyabiashara na hivyo kuongeza pato la Taifa huku akisema mkoa utahakikisha wanasimamia mradi huo ili uweze kukamilisha kwa wakati.



No comments