HEADER AD

HEADER AD

MCHUNWAJI UNATISHA

MCHUNWAJI unatisha, jinsi unajivimbisha,

Pesa zako zinakwisha, moyo waufurahisha,

Afya yako inakwisha, funguo unachezesha,

Mwangalie huyu nyani, kweli haoni kundule.

Kutoa ofa wakesha, nyumbani hujawalisha,

Vile wakikuimbisha, we kibopa unatisha,

Hapo wakulainisha, unazidi kuwalisha,

Mwangalie huyu nyani, kweli haoni kundule.

Mungu kakusimamisha, riziki kuizalisha,

Tena kakupa maisha, familia inatosha,

Njiani wakuyumbisha, kila kitu wadondosha,

Mwangalie huyu nyani, kweli haoni kundule.

Wewe umeshajiwasha, mshumaa unakwisha, 

Eti unajiridhisha, mwanga wako unatosha,

Hujui wewe waisha, giza kwako warudisha?

Mwangalie huyu nyani, kweli haoni kundule.

Hivi tunakukumbusha, unachunwa unakwisha,

Na tena twakuamsha, usingizi umetosha,

Kizidi kujilalisha, maisha wayafupisha,

Mwangalie huyu nyani, kweli haoni kundule.

Sasa kweli wajirusha, watu wawahangaisha,

Kote unawafikisha, na tena kuwaridhisha,

Nyumbani unakufisha, udongo wawalambisha,

MWangalie huyu nyani, kweli haoni kundule.

Mahali kikufikisha, wakijua umekwisha,

Kwenda nawe tena hasha, kwani umeshachemsha,

Wao wataliamsha, tayari ushawakosha,

Mwangalie huyu nyani, kweli haoni kundule.

Kizuri haya maisha, mengi hapa yanakwisha,

Kama ulijizungusha, dunia takuzungusha,

Malipo yake hutisha, na pumzi utashusha,

Mwangalie huyu nyani, kweli haoni kundule.

Mchunwaji unatisha, japo ndio unakwisha,

Vile hayo yaridhisha, uzidi tuwakilisha,

Pengine soma kutosha, moyo utauridhisha,

Mwangalie huyu nyani, kweli haoni kundule.

Mungu vitu apitisha, kwako hajatawanyisha,

Watu anawalengesha, mbele uweze wavusha,

Wa kwanza kwenye maisha, familia kuridhisha,

Mwangalie huyu nyani, kweli haoni kundule.

Mtunzi ni  Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments