KULA VYAKULA ASILI
NI vyakula vya asili, kula tunashauriwa,
Hivyo mwilini ni mali, ndivyo tunavyoambiwa,
Na tena vingi si ghali, vizuri vikitumiwa,
Tokomeza lishe duni, na magonjwa nyemelezi.
Ni muhimu kwa watoto, vyakula vikatumiwa,
Ni afya vyaleta joto, watoto watajaziwa,
Na tena vina mvuto, jinsi vinaandaliwa,
Tokomeza lishe duni, na magonjwa nyemelezi.
Picha na mtandaoTofauti navyo vile, vyakula vinatumiwa,
Virutubisho ni tele, tumeshathibitishiwa,
Havina madhara vile, au tungeliambiwa,
Tokomeza lishe duni, na magonjwa nyemelezi.
Ndizi viazi vitamu, vizuri vikatumiwa,
Matembele vuta hamu, damu unaongezewa,
Kunde mbaazi ni tamu, vema kama vyatumiwa,
Tokomeza lishe duni, na magonjwa nyemelezi.
Kula vyakula asili, ambavyo twashauriwa,
Ni hatua ya akili, magonjwa kutozidiwa,
Yaliyo mengi makali, ambayo tunavamiwa,
Tokomeza lishe duni, na magonjwa nyemelezi.
Yale yasoambukiza, magonjwa tunavamiwa,
Mengi yatunyong’onyeza, kwa ulaji yachangiwa,
Vitu tunajibugiza, sana vinachambuliwa,
Tokomeza lishe duni, na magonjwa nyemelezi.
Toka Wizara Kilimo, sisi tunashauriwa,
EU hata FAO wamo, ushauri tunapewa,
Asili vipewe promo, vizidi kukumbatiwa,
Tokomeza lishe duni, na magonjwa nyemelezi.
Mwili kuurutubisha, waziwazi twaambiwa,
Vyakula asili tosha, endapo vikitumiwa,
Pazuri tatufikisha, mengine kufanikiwa,
Tokomeza lishe duni, na magonjwa nyemelezi.
Kwa kinga bora mwilini, na kutokushambuliwa,
Vya asili viwe dini, jinsi vinavyotumiwa,
Tutadunda duniani, bila magonjwa vamiwa,
Tokomeza lishe duni, na magonjwa nyemelezi.
Mama lishe baba lishe, huko tunahudumiwa,
Kwetu vema tuwachoshe, vyakula vya kupatiwa,
Vya asili tujilishe, mbele tutafanikiwa,
Tokomeza lishe duni, na magonjwa nyemelezi.
Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Post a Comment