RC MTAMBI , VIONGOZI WA DINI , LAZARO NYALANDU WAWAOMBA WANANCHI KUJITOKEZA KUPIGA KURA , KUDUMISHA AMANI

>>Wanaohamasisha wananchi kutopiga kura wanakiuka katiba
DIMA Online , Mara
WANANCHI mkoani Mara, wametakiwa kujitokeza kwa wingi wakati wa uchaguzi mkuu tarehe, 29, Oktoba, 2025 katika vituo vya kupigia kura ili waweze kuwachagua viongozi bora watakaowatumikia.
Wananchi wametakiwa kuwapuuza watu wanaowashawishi kutopiga kura kwani kitendo hicho ni ukiukwaji wa haki za Binadamu ikiwemo haki ya kupiga kura kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 5(1).
Katiba hiyo inasema kwamba kila raia wa Tanzania mwenye umri wa miaka kumi na nane au zaidi atakuwa na haki ya kupiga kura katika uchaguzi wa Rais na Wabunge, au viongozi wengine kwa mujibu wa Katiba au sheria nyingine.
Wakizungumza katika kikao cha Kamati ya Amani mkoa wa Mara , Mkuu wa mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi amesema kwamba Katiba lazima iheshimiwe hivyo wananchi wanatakiwa kutumia haki yao kujitokeza kupiga kura.
Mkuu wa mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi akizungumza kwenye kikao cha kamati ya amani ya mkoa wa Mara ,Octoba, 17, 2025 katika ukumbi wa Hoteli ya MK mjini Musoma.
" Twendeni tukatumie haki yetu ya kikatiba tukapige kura ,tuchague viongozi wazuri na tuendelee kudumisha amani. Vyombo vya ulinzi na usalama vipo kwa ajili ya kuhakikisha usalama wa kila mtanzania .
" Kila anayeitakia mema nchi yetu lazima awe salama . Unapoona kiashiria chochote cha kusumbua maisha ya watanzania wenzako lazima amani yao utaifa wao uwepo. Tutoe elimu ya utaifa , tueleze misingi ya utanzania wetu inaanzia wapi" amesema RC Evans.
Waziri mstaafu wa Wizara ya maliasili na utalii, Lazaro Nyalandu, amesema umoja ni nguvu inayoweza kuwasukuma mbele watanzania na ni tunu ya Tanzania hivyo anawahamasisha wananchi kujitokeza kupiga kura kuchagua viongozi watakaowatumikia .
Waziri mstaafu wa Wizara ya maliasili na utalii, Lazaro Nyalandu akizungumza kwenye kikao cha kamati ya amani ya mkoa wa Mara ,Octoba, 17, 2025, katika ukumbi wa Hoteli ya MK mjini Musoma.
" Kuna wimbi limeanza kujitokeza wengine wanasema sisi hatutapiga kura , tukifanya hivyo umoja wetu , nguvu zetu kama Taifa zitabomoka. Nguvu ya Taifa itayumba pale ambapo vijana wetu wataanza kujitoa katika fursa za kushiriki kupiga kura kuwaweka madarakani viongozi .
" Vijana wakishiriki uchaguzi watapata fursa ya kuendelea kujifunza na kujiandaa kuchukua vijiti vya uongozi na wao kuwa viongozi" amesema Lazaro.
Ameongeza kuwa upigaji kura ni desturi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania . " Naomba tushawishi watu kwenda kupiga kura , kila kunapofanyika uchaguzi duniani uuliza ni asilimia ngapi ya watu wa nchi hiyo walitoka kwenda kupiga kura.
" Asilimia ni wingi wa watu wanaokuwa na imani , asilimia ya kura zinazopigwa zinamheshimisha Rais, Bunge na nchi miongoni mwa mataifa" amesema Lazaro.
Hata hivyo amepongeza kampeni zinazoendelea kwani zimegubikwa amani na utulivu huku akizidi kuwasisitiza wananchi kujitokeza kupiga kura uchaguzi mkuu.
Viongozi wa Dini
Viongozi wa dini katika mkoa huo wa Mara wamewataka wananchi wakiwemo waumini kushiriki uchaguzi na kwamba wasidanganywe na wanaopinga uchaguzi na kuwashawishi wananchi kutopiga kura kwakuwa kupiga kura ni haki yao kuwachagua viongozi wanaowataka.
Viongozi wa dini mkoa wa Mara wakiliombea Taifa baada ya kikao cha Amani katika ukumbi wa Hoteli ya MK mjini Musoma.
Mwenyekiti wa akina mama wa Kiislam mkoa wa Mara, Asha Mohamed amewaomba wanawake mkoani humo kujitokeza kupiga kura wasikubali kuchaguliwa viongozi.
" Tumeshakutana na akina mama wa Kiislam kuwapa elimu ya kupiga kura naomba wananchi na wanawake wote tarehe , 29 mwezi huu tujitokeze tukapige kura na tudumishe amani yetu" amesema.
Amani idumishwe
Wakati huohuo , Viongozi hao wa dini wamewaomba Watanzania wakiwemo wa mkoa wa Mara kudumisha amani kwani Tanzania ni nchi ya amani na yenye fursa mbalimbali, hivyo ni jukumu la kila mwananchi kuitunza nchi yake kwa kila hali.
Viongozi wa Dini mkoa wa Mara wakiwa katika picha ya pamoja na mkuu wa mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi baada ya kikao cha kamati ya amani mkoani humo kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya MK mjini Musoma.
" Kuna watu hawapendi wanapoona Waislam na Wakristo wa Tanzania wanaendelea kukaa kwa pamoja kama ndugu wakiishi kwa umoja wakishirikiana kwa mema na mabaya. Nchi yetu ni ya amani na utulivu nchi ya watu wanaosikilizana, kusemezana , kujadiliana hivyo ni lazima tuilinde amani yetu" amesema Lazaro Nyalandu.
Askofu wa kanisa la Anglikana Dayosisisi ya Rorya, Moses Yamo ameviomba vyombo vya ulinzi na usalama mkoa wa Mara visitumie nguvu kubwa katika kuimalisha utulivu wakati wa uchaguzi kwani nguvu kubwa ikizidi inaweza kuwapa hofu wananchi na kutojitokeza kwenda kupiga kura na badala yake vihamasishe wananchi kwenda kupiga kura.
Ameongeza serikali ichukue hatua kuwadhibiti watu wachache wanaotumia mitandao ya kijamii kupotosha watu na kutishia watu huku kamati ya amani ikihimizwa kuhakikisha inasaidia kudumisha amani mkoani Mara.
Post a Comment