HEADER AD

HEADER AD

MGANGA MKUU HALMASHAURI YA KIBAHA AWAHAMASISHA VIJANA KUJITOKEZA KUPIGA KURA


Na Gustaphu Haule, Pwani 

MGANGA mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Catherine Saguti amewahamasisha vijana waliopo katika Manispaa hiyo kujitokeza kwa wingi Oktoba 29 kwa ajili ya kupiga kura ili waweze kuchagua viongozi sahihi.

Saguti ,ametoa wito huo Oktoba 18,2025 wakati akizungumza na Wananchi mbalimbali pamoja na vijana wa Klabu za Jogging katika eneo la soko la  Loliondo mara baada ya kumaliza zoezi la kufanya usafi katika mtaro wa daraja la mto Loliondo.

Amesema wote wanajua kuwa Oktoba 29,2025 Taifa linakwenda kuwa na tukio kubwa la uchaguzi mkuu wa Rais, Mbunge na diwani kwahiyo ametumia nafasi hiyo kuhamasisha vijana wote wa Halmashauri ya Manispaa kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwa amani na utulivu.

        Vijana wa Jogging Manispaa ya Kibaha wakihamasisha usafi wa mazingira katika soko la Loliondo Kata ya Tangini Oktoba 18,2025.

"Leo tupo hapa tunafanya usafi wa mazingira lakini wote tunajua kuwa tunaelekea kwenye uchaguzi Oktoba 29 basi nipende kuwahamasisha vijana wote waliopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha kujitokeza kwa wingi kwenda kupiga kura kwa amani na utulivu ili waweze kuchagua viongozi sahihi,"amesema Saguti.

Akizungumza kuhusu Jogging ( Mbio za Polepole) zilizofanyika kutoka eneo la Mailimoja hadi katika soko la Loliondo Saguti amesema kuwa lengo la Jogging hiyo ilikuwa ni kwa ajili ya kuhamasisha usafi wa mazingira katika Manispaa ya Kibaha .

Saguti amesema pamoja na kufanya usafi huo lakini pia ni sehemu  ya idara ya afya katika kufanya muendelezo wa matukio ya kijamii  kuelekea siku ya afya ( Afya Day) itakayofanyika Oktoba 25 mwaka huu.

      Washiriki wa Jogging katika Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha wakifanya usafi wa mazingira katika soko la Loliondo tukio ambalo lilifanyika Oktoba 18,2025

Amesema wakati wanaelekea katika kilele cha afya Day idara ya afya imekuwa ikijitoa kushirikiana na vikundi vya Klabu za Jogging kwa ajili ya kuhamasisha masuala ya usafi wa mazingira.

Nae Mratibu wa magonjwa yasiyoambukiza wa Manispaa ya Kibaha ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya uhamasishaji siku ya afya day  Dkt.Sabinus Ndunguru amesema kuwa wamekuwa wakihamasisha mazoezi na ufanyaji wa usafi.

Ndunguru amesema lengo mahususi ni kuhamasisha Wananchi wa Kibaha kujitokeza siku ya Ijumaa Oktoba 24  katika viwanja vya Mailimoja kupata elimu kuhusu magonjwa yasiyoambukiza kama vile ugonjwa wa ini.

       Vijana wa jogging wakihamasisha usafi wa mazingira katika Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha iliyofanyika Oktoba 18,2025 Kibaha Mkoani Pwani.

Amesema mbali na hilo, lakini pia siku hiyo  kutakuwa na zoezi la uchangiaji damu kwakuwa mahitaji ya damu ni makubwa katika hospitali na Oktoba 25  ni siku ya maadhimisho ya afya day ambapo kutakuwa na mazoezi kuanzia Mailimoja hadi stendi mpya ya mabasi.

Hatahivyo, Ndunguru amewahamasisha Wananchi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha kujitokeza siku ya Oktoba 29 kwenye jambo la Kitaifa kupiga kura kwa amani ili wakawachague viongozi wanaowataka.

       Wananchi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha wakifanya usafi katika Mtaro wa maji machafu uliopo karibu na Soko la Loliondo Manispaa ya Kibaha, zoezi ambalo lilikuwa likifanyika kwa usimamizi wa Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kibaha Catherine Saguti.

Nae mwananchi wa Kibaha Mailimoja Omary Ahamed ameipongeza ofisi ya Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kibaha kwakuendesha jogging ambayo inahamasisha masuala ya usafi wa mazingira kwakuwa inasaidia kuboresha afya za Wananchi.

Hatahivyo,Ahamed ,amewaomba Wananchi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha kujitokeza siku ya Oktoba 29 kupiga kura kwa ajili ya kuchagua viongozi watakaofaa kuongoza nchi kwa muda wa miaka mitano ijayo.

Vijana wa jogging wakibeba ujumbe Oktoba 18 walipokuwa siku ya Loliondo wakifanya usafi wa mazingira.


Ujumbe wa Vijana uliotolewa wakati wakihamasisha jamii kufanya usafi wa mazingira katika soko la Loliondo lililopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha.

No comments