HEADER AD

HEADER AD

WANANCHI 200 KIBAHA WAPATA HUDUMA BURE YA UCHUNGUZI WA MAGONJWA

 


Na Gustaphu Haule, Pwani 

HALMASHAURI ya Manispaa ya Kibaha imetoa huduma bure ya uchunguzi wa magonjwa mbalimbali kwa wananchi zaidi ya 200 waliopo katika Halmashauri hiyo.

Baadhi ya magonjwa yaliyofanyiwa uchunguzi ni pamoja na ugonjwa wa presha,kisukari na huduma ya kuchangia damu ambapo kati ya hao Wananchi 50 waligundulika kuwa na ugonjwa wa presha na wananchi nane wamegundulika kuwa na ugonjwa wa kisukari.

Afisa afya wa mkoa wa Pwani David Vuo alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Waandishi wa habari katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya afya yaliyofanyika Oktoba 25/2025 katika viwanja vya bwawani vilivyopo Kata ya Tumbi Manispaa ya Kibaha.

Afisa afya wa Mkoa wa Pwani David Vuo( kushoto) na Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kibaha Dkt . Catherine Saguti (Kulia)wakiwa wameshika bango la ujumbe wa kilele cha maadhimisho ya wiki ya afya yaliyofanyika Oktoba 25 katika viwanja vya Bwawani Manispaa ya Kibaha.

Vuo ambaye alikuwa akimwakilisha Mganga Mkuu wa mkoa wa Pwani  Kusirye Ukio amesema kuwa wiki ya afya ni nguzo ya kampeni ya afya ( Mtu ni Afya) iliyozinduliwa mwaka 2024 na Makamu wa Rais Dkt.Philip Mpango katika  hafla iliyofanyika kwenye viwanja vya stendi ya zamani ya Mailimoja Manispaa ya Kibaha.

Amesema maadhimisho ya wiki ya afya ya mwaka 2025 yamekwenda sambamba na kauli mbiu ya "Kushiriki uchaguzi wa mwaka 2025 kwa amani na utulivu "ambapo ametoa wito kwa Wananchi kuhakikisha ifikapo Oktoba 29 wajitokeze kushiriki uchaguzi kwa kuwachagua viongozi wanaowataka kwa amani na utulivu.

"Oktoba 29/2025 ni siku ya uchaguzi mkuu hivyo nawasihi Wananchi wa Manispaa ya Kibaha  na Mkoa kiujumla wajitokeze kupiga kura kwa ajili ya kuwachagua viongozi wanaowataka kwa ustawi wa nchi yetu,"amesema Vuo.

Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kibaha Dkt .Catherine Saguti amesema kuwa kila mwaka huwa wanaadhimisha siku ya afya (Afya Day) lakini kwa mwaka huu walianza Oktoba 18 kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii.

             Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Catherine Saguti.

Amesema moja ya shughuli hizo ni kufanya Jogging iliyowashirikisha wadau mbalimbali pamoja na kufanya usafi wa mazingira katika Mtaro wa Soko la Loliondo na kutoa huduma bure katika vituo vya kutolea huduma ya afya .

Saguti amesema kuwa Oktoba 24 walikuwa wakitoa huduma ya upimaji wa magonjwa mbalimbali katika viwanja vya bwawani Kata ya Tumbi na Oktoba 25 ndio kilele cha maadhimisho ya wiki ya afya iliyokwenda sambamba na kufanya Jogging,kukimbiza kuku na kucheza mpira wa miguu.Wafanya Jogging wa Manispaa ya Kibaha katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya afya yaliyofanyika Oktoba 25/2025.

.    Baadhi ya wadau wakiwa katika Jogging ya maadhimisho ya kilele cha wiki ya afya ( Afya Day) yaliyofanyika Oktoba 25 katika Manispaa ya Kibaha Mkoa wa Pwani

Saguti amesema kuwa pamoja na kufanya maadhimisho hayo lakini pia ameendelea kuwahamasisha Wananchi wa Manispaa hiyo wakiwemo vijana,wa kike na wakiume na wazee kuhakikisha wanashiriki uchaguzi siku ya Oktoba 29 mwaka huu.

Mwakilishi wa Vijana Wilaya ya Kibaha Mjini Joel Kituu ametumia nafasi hiyo kuwahamasisha vijana wenzake kuona umuhimu wa kujitokeza Oktoba 29 kupiga kura kuwachagua viongozi wanaowataka.

Kituu ,amesema vijana wajitokeze kupiga kura kwa amani na utulivu kwakuwa kupiga kura ni kutimiza haki yao ya msingi na kikatiba bila kusahau bima ya afya kwa wote ni msingi bora kwa huduma ya afya.

Hata hivyo,mmoja wa wananchi wa Manispaa ya Kibaha Kassim Chamiti ameishukuru idara ya afya kwa kufanya maadhimisho hayo kwakuwa yamewasaidia kupata huduma afya bure huku akisisitiza suala la kujitokeza kupiga kura siku ya Oktoba 29 mwaka huu.




No comments