ENG. KUNDO AJINASIBU KULIFUNGUA JIMBO LA BARIADI MJINI KIMAENDELEO
Na Abdallah Nsabi, Simiyu
MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Bariadi Mjini kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Eng. Andrea Kundo amewaahidi wananchi kutatua changamoto za maeneo ya Kata za Guduwi na Malambo, huku akiahidi kuendeleza utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo itakayowanufaisha wananchi wa maeneo hayo na vijiji jirani.
Akiwa katika Tawi la Mlimani, Kata ya Guduwi, Eng. Kundo amewaeleza wananchi mpango wake wa kuanza ujenzi wa daraja la mto Bariadi litakalounganisha Kata za Guduwi na Mhango pamoja na vijiji vya jirani, hatua itakayorahisisha usafiri, kukuza biashara, na kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi.
Mgombea ubunge wa jimbo la Bariadi mjini Eg Andrea Kundo akizungumza na wakazi wa kata ya malambo.
Ameahidi kufungua na kuboresha barabara zenye jumla ya kilomita 50 katika maeneo ya Mlimani na vitongoji vyake ili kurahisisha mawasiliano na upatikanaji wa huduma za kijamii. Vilevile, alieleza dhamira yake ya kuboresha miundombinu ya maji safi na salama kwa wananchi wa Guduwi pamoja na kuhakikisha kila kaya inapokea huduma ya umeme.
Katika Kata ya Malambo, Mtaa wa Voda, Eng. Kundo ameahidi kufungua barabara katika maeneo mbalimbali ya mtaa huo ili kuboresha miundombinu ya usafiri na kurahisisha shughuli za kila siku za wananchi, hususan wafanyabiashara wadogo na wajasiriamali wa mtaa huo.
Mgombea ubunge wa jimbo la Bariadi mjini,Eng Andrea Kundo akiwa na wakazi wa kata ya Guduwi
Ameahidi kufungua na kuboresha barabara zenye jumla ya kilomita 50 katika maeneo ya Mlimani na vitongoji vyake ili kurahisisha mawasiliano na upatikanaji wa huduma za kijamii. Vilevile, alieleza dhamira yake ya kuboresha miundombinu ya maji safi na salama kwa wananchi wa Guduwi pamoja na kuhakikisha kila kaya inapokea huduma ya umeme.
Akizungumza mbele ya wananchi amemnadi Mgombea Urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan akisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya sita imeleta mageuzi makubwa ya maendeleo katika Jimbo la Bariadi Mjini kupitia miradi ya elimu, afya, maji, na miundombinu.
Wananchi wa Guduwi na Malambo, Asheri Gunday na Samsoni Kija wamempongeza Eng. Andrea kwa uongozi wake wa karibu na namna anavyotekeleza ahadi kwa vitendo, na jinsi anavyoshughulikia changamoto za wananchi katika maeneo yao.





Post a Comment