HEADER AD

HEADER AD

MEYA KIBAHA ATEMBELEA KITUO CHA WATOTO YATIMA NA KUTOA MSAADA

Na Gustaphu Haule,Pwani

WATOTO Yatima wa kituo cha Shalom kilichopo Mtaa wa Kidenge" B"Kata ya Msangani Manispaa ya Kibaha ambao walishindwa kwenda shuleni kutokana na changamoto ya ukosefu wa sare za Shule sasa changamoto hiyo imetatuliwa.

Changamoto hiyo imetatuliwa  mara baada ya Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Mawazo Nicas kutembelea kituo hicho na kutoa msaada wa sare za shule(uniform)jozi 50 zikiwa na soksi zake.

      Mlezi wa kituo cha watoto yatima cha Shalom Lilian Mbise akiwa na watoto wake mara baada ya kupokea msaada wa sare za shule jozi 50 kutoka kwa Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Mawazo Nicas.

Dkt.Nicas amefika katika kituo hicho Januari 14/2026 akiwa ameambatana na afisa ustawi wa jamii Faustina Kayombo pamoja na Mratibu wa dawati la familia na mtoto kutoka Manispaa ya Kibaha Mary Mmasi.

Akikabidhi msaada huo kwa mlezi wakituo hicho Lilian Mbise Stahiki Meya huyo alitumia nafasi hiyo kumpongeza mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa kwa namna ambavyo amekuwa akiwakumbuka watoto Yatima.



Amesema Manispaa ya Kibaha inavituo Tisa vya kulelea watoto Yatima vikiwa na jumla ya watoto 610 ambavyo kwa namna moja au nyingine Manispaa ya Kibaha imekuwa ikivisaidia mara kwa mara .

Amesema kipindi hiki ni kipindi cha watoto kwenda Shule lakini Manispaa ilipata taarifa ya  kuwepo kwa  changamoto ya watoto wa kituo hicho kushindwa kwenda shule kutokana na uhaba wa sare za shule ( Uniform) na kwamba kutokana na umuhimu wa watoto hao Manispaa ikaona ni vyema ikawasaidia.

        Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Mawazo Nicas akiwa amembeba mtoto yatima wa kituo cha Shalom alipokwenda Januari 14/2026 kwa ajili ya kutembelea kituo hicho na kutoa msaada wa sare za shule jozi 50.

Dkt.Nicas amesema kuwa mahitaji ya watoto hao ni makubwa na kwamba sio kama sare hizo zitakuwa zimemaliza kila kitu hivyo ametumia nafasi hiyo kuwaomba wadau wengine kujitokeza ili kuona namna ya kuwasaidia watoto hao.

",Leo nimefika kuwatembelea watoto yatima wa kituo hiki cha Shalom na nimewaletea sare za shule 50 ili kusudi waweze kwenda shuleni kusoma lakini sare hizo zitagawanywa katika vituo viwili kikiwemo na kituo cha Buloma Foundation cha Kata ya Sofu,"amesema Dkt.Nicas

Dkt.Nicas amesema kuwa Manispaa ya Kibaha itaendelea kuwashika mkono watoto Yatima ili na wao waweze kuishi kwa furaha kama ambavyo wengine wanaishi na kwamba hivyo ndivyo Rais Dkt . Samia Suluhu Hassan anavyotaka kuona.

       Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Mawazo Nicas akisalimiana na mtoto yatima wa kituo cha Shalom kilichopo Mtaa wa Kidenge Kata ya Msangani alipokwenda Januari 14/2026 kwa ajili ya kutembelea kituo hicho.

Amesema kuwa,Rais Dkt .Samia Suluhu Hassan anapenda kuwaona Watanzania wanaishi kwa furaha na miongoni mwao wapo watoto yatima na ndio maana ndani ya siku 100 za Rais Samia Manispaa ya Kibaha inataka kuona inakuwa na mafanikio makubwa.

Amewaasa watoto hao kusoma kwa bidii kwa ajili ya kuandaa maisha yao ya baadae na kwamba chochote wanachotendewa wasidhani kama Kibaya lakini kwakuwa ni sehemu ya kufikia mafanikio yao.

Afisa Ustawi wa Jamii Faustina Kayombo,amesema kuwa Manispaa ina vituo tisa ambavyo uhudumia watoto wenye kuanzia umri wa mwezi mmoja hadi miaka 18 .

       Afisa Ustawi wa Jamii wa Manispaa ya Kibaha Faustina Kayombo.

Kayombo amesema lengo la vituo hivyo ni kuhakikisha watoto wanakuwa katika ulinzi,usalama na wanapata huduma zote muhimu ikiwemo kupata haki ya chakula, elimu ,afya ,malazi na huduma nyingine muhimu.

Amesema Manispaa ya Kibaha imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha watoto wanapata chakula na mahitaji mengine na kwamba awamu iliyopita walitoa chakula katika kituo hicho na sasa wametoa sare za shule.

      Watoto yatima wa kituo cha Shalom kilichopo Mtaa wa Kidenge Kata ya Msangani Manispaa ya Kibaha Mkoa wa Pwani.

Nae mlezi wa kituo cha Shalom Lilian Mbise amemshukuru Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Mawazo Nicas pamoja na mkurugenzi wake Dkt.Rogers Shemwekwa kwa namna ambavyo wamewagusa watoto yatima wa kituo hicho huku akisema kwasasa sare hizo zitawafanya watoto kuwa na muonekano sawa na watoto wengine.

        Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Mawazo Nicas (kushoto) na mlezi wa kituo cha watoto yatima cha Shalom Lilian Mbise ( Kulia) wakiwa katika makabidhiano ya sare za shule kwa watoto hao hafla ambayo ilifanyika Januari 14/2026 katika kituo hicho kilichopo Mtaa wa Kidenge" B" Kata ya Msangani Manispaa ya Kibaha

No comments