MKURUGENZI TAKUKURU AKABIDHI VIFAA TIBA KUSAIDIA UKUAJI WA WATOTO NJITI HOSPITALI YA TUMBI

Na Gustaphu Haule, Pwani
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) imekabidhi vifaa tiba vya kisasa ( mashine) kwa ajili ya kusaidia ukuwaji wa watoto Njiti katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani iliyopo Tumbi Kibaha vyenye thamani zaidi ya TSh. Milioni 9.
Vifaa vilivyotolewa kitaalam ni Infant Radiant Warmer na Phototherapy Unit ambavyo vyote vinatumika kumsaidia mtoto Njiti mara baada ya kuzaliwa.
Makabidhiano ya vifaa hivyo yamefanyika Januari 21/2026 katika viwanja vya hospitali ya Rufaa Tumbi baina ya Mkurugenzi wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na TAKUKURU nchini Crispin Chalamila na Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo Amani Malima hafla ambayo imehudhuriwa na watumishi wa Takukuru Mkoa wa Pwani na wafanyakazi wa hospitali hiyo .
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru Nchini Crispin Chalamila ( Kulia) akimkabidhi vifaa tiba kwa ajili ya kusaidia watoto Njiti Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani ( Tumbi) iliyopo Kibaha katika hafla iliyofanyika Januari 21/2026 hospitalini hapo.Akizungumza kabla ya kukabidhi msaada huo, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Nchini Crispin Chalamila amesema kuwa msaada wa mashine hizo umetolewa kwa lengo la kuendelea kuunga mkono jitihada za serikali za kupunguza vifo vya watoto Njiti nchini.
Chalamila amesema msaada huo ni muendelezo wa misaada inayotolewa na taasisi hiyo katika hospitali mbalimbali nchini na kwamba fedha za kununulia mashine hizo zinatokana na michango binafsi ya watumishi wa Takukuru .
Mkurugenzi wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na TAKUKURU nchini Crispin Chalamila."Watumishi wa TAKUKURU kwa pamoja tulikubaliana tutoe sehemu ya mishahara yetu kama michango ili kufanikisha ununuzi wa mashine hizi na hadi sasa tumekwisha toa katika hospitali za Mikoa nane nchini"amesema Chalamila.
Amesema kuwa mpango wa kutoa msaada wa vifaa vya kusaidia ukuaji watoto njiti Nchini ulianza mwaka 2024 katika Mkoa wa Arusha na hadi sasa tayari wametoa vifaa hivyo kwa mikoa nane na malengo yao ni kuzifikia hospitali za Mikoa 28 hapa nchini.
Amesema wameamua kufanya hivyo kwa ajili ya kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwakuwa wanafahamu Serikali ina majukumu mengi na haiwezi kufanya mambo yote kwa wakati mmoja na kwamba wakisubiri hadi Serikali ifanye uenda ikachelewa.
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru Nchini Crispin Chalamila (Kulia) akimkabidhi vifaa vya kuwasaidia watoto Njiti Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani (Tumbi ) Kibaha Amani Malima ( kushoto) katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika Januari 21/2026 katika hospitali hiyo.Chalamila ameongeza kuwa walichagua eneo la afya upande wa watoto Njiti sio kwa bahati mbaya lakini ni baada ya kufanya utafiti na kugundua mahitaji ya watoto Njiti ni makubwa lakini kwa Mkoa wa Pwani ameona kuna uhitaji mkubwa zaidi kutokana na takwimu za vifo kwa watoto hao zilitolewa na daktari wa watoto wa hospitali hiyo Adelina Rutashobya.
Ametoa wito kwa taasisi nyingine za kiserikali na watu binafsi kujitokeza kutoa msaada wa vifaa vya kusaidia ukuaji wa watoto Njiti kwakuwa changamoto bado ni kubwa .
Amesema TAKUKURU inashukuru kwa ushirikiano mkubwa uliopo kati ya uongozi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani na kwamba taasisi yake itaendelea kutoa elimu kuhusu masuala ya rushwa kwa watumishi wa hospitali hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru Nchini Crispin Chalamila ( katikati) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani na viongozi wa Takukuru Mkoa wa Pwani na Taifa.Hata hivyo,Chalamila amesema kulingana na uhitaji wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani wataona namna ya kusaidia vifaa vingine hapo baadae mara baada ya kuzifikia kwa awamu ya kwanza hospitali zote huku akiwaomba viongozi wa hospitali hiyo kuhakikisha wanavitumia vifaa hivyo na kuvitunza vizuri ili viweze kusaidia watoto wengi zaidi na kwa muda mrefu.
Daktari wa watoto katika hosptali hiyo, Adelina Rutashobya,amesema katika kipindi cha mwaka 2025 walipokea jumla ya watoto 1,393 ambapo kati yao 370 walizaliwa kabla ya wakati sawa na asilimia 27 na kwamba watoto 173 waligundulika na magonjwa ya moyo na 61 walifariki.
Mashine za kusaidia watoto Njiti zilizotolewa na taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)."Asilimia 10 ya watoto hao walipewa rufaa na asilimia 80.8 waliruhusiwa lakini pamoja na mafanikio machache changamoto inayotukabili ni ukosefu wa vifaa tiba na dawa kwa ajili ya watoto njiti"amesema Rutashobya
Rutashobya amesema upungufu wa vifaa hivyo ni pamoja na mashine za uangalizi wa karibu za watoto, mashine za maji pamoja na dawa za kukomaza mapafu ya watoto.
Naye kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Pwani, Domina Mkama, amesema wamekuwa wakishirikiana na hospitali hiyo katika ufuatiliaji wa fedha za miradi na wanapata ushirikiano mzuri kutoka kwao.
Amesema kuwa mbali na ufuatiliaji wa fedha za miradi lakini pia wamekuwa wakishirikiana katika masuala mbalimbali ikiwemo utoaji wa elimu za rushwa na afya.
Mganga Mfawidhi wa hosptali hiyo, Dkt.Amani Malima amemshukuru Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru na taasisi yake kwa kutoa msaada huo s hapo .
Malima amesema msaada uliotolewa na taasisi hiyo ni muhimu kwa ustawi na ukuwaji wa watoto Njiti na kwamba watahakikisha wanatunza vifaa hivyo kama ambavyo mkurugenzi Mkuu alivyowaelekeza.






Post a Comment