HEADER AD

HEADER AD

SERIKALI YATOA BILIONI 45.6 UJENZI WA MADARAJA YA DHARURA

Alodia Babara, Kagera,

SERIKALI nchini imetoa Tsh. Bilioni 45.6 kwa ajili ya ujenzi wa madaraja matano ya dharura ambayo yalianza kutekelezwa mwaka 2024 katika kipindi cha mvua zilizonyesha juu ya kiwango na kusababisha maji kujaa katika baadhi ya barabara na kushindwa kupitika mkoani Kagera.

Baada ya barabara kujaa maji kutokana na mvua hizo Serikali ilitoa fedha za dharura kujenga madaraja ili kuwanusuru wananchi kwani baadhi ya maeneo walikuwa wameanza kutumia mitumbwi kutokana na barabara kujaa maji.

Watumishi katika ofisi ya Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Kagera  wametembelea miradi ya ujenzi wa madaraja hayo matano na kujionea maendeleo ya miradi hiyo ambapo daraja moja kati ya hayo la Kyanyabasa, wananchi walikuwa wanavuka kwa kutumia kivuko.

Meneja wa Wakala wa Barabara TANROADS mkoa wa Kagera ,Mhandisi Joel Mwambungu amesema, madaraja hayo ambayo ni daraja la Kanoni lililopo Bukoba Manispaa, Kyetema, Kalebe na Kyanyabasa yaliyopo halmashauri ya Bukoba na daraja la Kamishango Wilaya ya Muleba, yalianza kutekelezwa Novemba 2024 na yatakamilika Februari mwaka huu.

Aliyevaa miwani mieusi (katikati) ni Meneja wa Wakala wa Barabara Tanroads mkoa wa Kagera Joel Mwambungu akizungumzia ujenzi wa miradi ya madaraja mkoani humo.

"Hii miradi yote ya Bilioni 45.6 inatekelezwa na wakandarasi wazawa hivyo fedha zote zimebaki hapa Kagera na wakandarasi wamepata uwezo, kipindi cha nyuma madaraja kama haya tulikuwa tunafikiri hayawezi kutekelezwa na wakandarasi wa ndani hii imejenga imani kwa serikali na kwa wakandarasi kuwa tunaweza kufanya kazi wenyewe tukijipanga" amesema Mhandisi Mwambungu

Ametaja faida za ujenzi wa madaraja hayo kuwa ni ajira kwa wananchi pamoja na kuchochea uchumi mkoani hapa kupitia myororo wa thamani kwa mazao na mali ambazo zinapatikana Kagera kwa kurahisisha na kupunguza muda wa usafiri kutoka sehemu  moja kwenda nyingine.


Akizungumzia mradi wa daraja la Kanoni Mhandisi Mwambungu ameeleza kuwa,  daraja lina urefu wa mita 30 na barabara za maingilio zinazojengwa kwa kiwango cha rami mita 600 na gharama yake ni sh. Bilioni 5.5 linatekelezwa na mkandarasi Abemulo, daraja la Kyetema lenye urefu wa mita 45 maingirio ya barabara kilomita moja gharama yake ni sh. Bilioni 8.5 linajengwa na  kampuni ya Gemen Enginearing Constraction Ltd.

Amesema daraja la Kyanyabasa lina urefu wa mita 105, barabara za maingilio zenye urefu wa mita 600, gharama za mradi ni sh. bilioni 9.8 unatekelezwa na kampuni ya Gemen.


"Mradi mwingine ni daraja la Kalebe ambalo lina urefu wa mita 60 na barabara za Maingirio kilomita 1.5 gharama za mradi ni sh. bilioni 9.3, unatekelezwa na Kampuni ya Milembe Constraction Ltd na daraja la Kamishango lenye urefu wa mita 45, gharama zake ni sh.bilioni 12.6 madaraja yote barabara za maingilio ni za kiwango cha rami" ameema Mhandisi Mwambungu

Baadhi ya wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo wameshukuru TANROADS na  Serikali kupitia Wizara ya ujenzi kwa kuwaamini na kuwakabidhi miradi hiyo waijenge na kuwa wanaahidi kuendelea kufanya vizuri na kuikamilisha miradi hiyo kwa wakati.

Mkurugenzi wa kampuni ya ujenzi wa Milembe Constractions inayotekeleza ujenzi wa daraja la Kalebe Osca Byabato ametaja changamoto inayowakabili kuwa ni mvua ambazo zimekuwa zikinyesha na kusababisha ujenzi kusimama.

Mmoja wa wananchi wanaotumia daraja la Kyanyabasa Anameri John amesema kuwa, kabla daraja kujengwa walikuwa wakitumia kivuko ambacho kilikuwa kinafungwa saa 12:00 jioni jambo ambalo lilikuwa linakwamisha safari zao.

            Mkurugenzi wa Milembe Constraction Osca Byabato akizungumza katika mradi wa ujenzi wa daraja la Kalebe lililopo Halmashauri ya Bukoba.

"Tulikuwa tukifika Kyanyabasa tukakuta kivuko kimefungwa tulikuwa tunatumia mtumbwi kuvuka au tunalazimika kuzunguka kupitia barabara ya Ibwera, lakini kwa sasa tunaishukuru Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kujenga daraja ambalo limemaliza kero yetu" amesema John

Amesema kukamilika kwa daraja la Kyanyabasa kutakuwa ni mkombozi kwa wananchi hao ambao wameteseka miaka mingi wakitumia kivuko kutoka upande mmoja kwenda upande wa pili.



No comments