WAZAZI WAOMBWA KUPELEKA VIJANA WAO CHUO CHA PETI
Na Alodia Dominick, Karagwe
WAZAZI na walezi wametakiwa kupeleka watoto wao katika chuo cha Perfect Education Training Institute Limited (PETI) chenye malengo ya kujenga stadi za maisha kwa vijana, uelewa na nidhamu katika jamii.
Hayo yamesemwa na mkurugenzi wa chuo hicho Mbeki Mbeki katika mahafali ya 29 ya chuo hicho kilichopo kitongoji cha Rukajange kijiji cha Kishao kata ya Bugene wilaya ya Karagwe mkoani Kagera yaliyofanyika Januari 09, 2026 ambapo amewasihi wazazi kuendelea kuleta vijana ili wapate maarifa chuoni hapo.
Mkurugenzi wa chuo cha PETI Mbeki Mbeki akizungumza na wageni waalikwa, wanachuo pamoja na wahitimu katika mahafari ya 29 chuoni hapo.
"Kila mzazi anatakiwa kumleta mwanaye chuo cha PETI, chuo chenye malengo ya kujenga vijana wenye stadi za maisha, nidhamu na uelewa katika jamii ili aweze kujiajili na kuwa raia mwema" amesema Mbeki.
Ameongeza kuwa chuo hicho kinawaandaa vijana waliofundishwa chuoni kuyaweka kwenye vitendo baada ya masomo yao, vijana hao wakakumbushwa nidhamu na utii kuwa ni nguzo kuu huko waendako katika maisha mapya ya mafunzo kwa vitendo.
Amezitaja kozi zinazofundishwa chuoni hapo kuwa ni pamoja na Uandishi wa habari na utangazaji, Utalii, Hotelia, Ualimu na ukalani.
Katika risala ya wahitimu iliyosomwa na Headingtone Ezron pamoja na Paskazia Isack imeeleza kuwa, wanachuo hao wameanza masomo yao mwaka 2023 wakiwa wanachuo 15 na wamehitimu wakiwa wanachuo wanane.
Wametaja changamoto zinazowakabili kuwa ni pamoja na gharama za kujifunza na maisha, upungufu wa vitendea kazi katika baadhi ya kozi mfano vifaa vya kufanyia mazoezi kwa vitendo, uhitaji wa maboresho zaidi katika hostel, viti na meza, uhaba wa kompyuta na mahitaji ya mafunzo ya kijasiliamali kwa vitendo.
"Tunapokabidhiwa vyeti vyetu tunaapa kuwa mabalozi wa chuo cha PETI popote tunapokwenda kwani tumeandaliwa kuwa viongozi waadilifu, wabunifu na wenye moyo wa kutatua changamoto za taifa na changamoto binafsi"
"Tutatumia elimu yetu kuleta suluhu katika jamii na mazingira na kazini kwetu na tumejifunza kuwa, bahari haivukwi kwa kuogelea tu bali kwa maarifa ujasili na maadili" wamesema wanachuo hao
Wameeleza kuwa, elimu waliyoipata ni bahari ambayo imewapa upepo, dira, lango na usukani na kuwa, safari yao ya maisha ya kitaaluma imeanza rasmi, wameomba viongozi, jamii na serikali kuendelea kuwaunga mkono ili wawe chachu ya maendeleo katika nchi hii.
Mmoja wa wajumbe wa bodi ya chuo hicho na diwani mstaafu Josephati Kinyina amewasihi wahitimu katika chuo hicho kutofungwa na kozi walizozipata bali waendelee kujiendeleza na kusomea kozi nyingine ambazo zitaweza kuwasaidia katika maisha ya kila siku kama ushonaji.
Mgeni rasmi katika mahafari hayo ambaye alikuwa afisa elimu kata ya Kayanga Benjamin Mazimba kwa niamba ya afisa elimu taaluma wilaya ya Karagwe Johnbosco Paul amesema kuwa, serikali imeanzisha shule ya amali watoto watasoma kidato cha nne na sita na watarudi vyuo vya kati kusoma elimu ya amali.
Mazimba amesema kuwa, wanachuo waliohitimu wasisubili kuajiliwa bali wajiajiri kutokana na fani walizosomea.
"Wanachuo mliohitimu leo na mnaoendelea na masomo hapa chuoni nawasihi kuweni na nidhamu maana nidhamu ni msingi mkubwa wa mafanikio sehemu yoyote masomoni na hata kazini" amesema Mazimba
Mazimba aliahidi kutoa meza tano kupunguza changamoto hiyo chuoni hapo.







Post a Comment