DC TARIME , MWENYEKITI MATERA WAWAKATAA WAKANDARASI WABABAISHAJI MIRADI YA CSR
>>DC ataka mgodi kutowapa kazi wakandarasi wazembe
>> Mwenyekiti Tarime Vijijini asema ni muda wa kuachana na Wakandarasi wasio waaminifu
Na Mwandishi Wetu, Nyamongo
SERIKALI wilayani Tarime, mkoa wa Mara ,imesema haitawavumilia wakandarasi wababaishaji wanaochelewesha ama kujenga chini ya kiwango miradi ya maendeleo, inayojengwa kwa fedha za uwajibikaji wa makampuni kwa jamii (CSR) .
Mkuu wa Wilaya ya Tarime , Meja Edward Gowele amesema kwamba mgodi wa dhahabu wa Barrick North Mara uliopo Nyamongo, umekuwa ukitekeleza miradi ya maendeleo kupitia fedha za CSR.
Mkuu wa Wilaya ya Tarime Meja Edward Gowele (wa pili kulia), Meneja mkuu Mgodi wa Barrick North Mara , Apolinary Lyambiko ( wa kwanza kulia) Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Tarime, Matera Chacha (Wa pili kushoto), Diwani wa Kata ya Matongo kupitia chama cha Mapinduzi (CCM) Godfrey Kegoye (wa kwanza kushoto) wakiwa kwenye kikao cha kujadili Maendeleo vijiji 11 vinavyozunguka mgodi.
Miradi hiyo ikiwemo ya elimu, afya, maji inajengwa na wakandarasi mbalimbali lakini amebaini kuwepo kwa wakandarasi wazembe wasiowaaminifu wanaokwamisha miradi na kutokamilika kwa wakati na kwa ubora.
DC Gowele ameyasema hayo katika kikao kilichofanyika mgodini Februari , 20, 2026, kilichoandaliwa na mgodi wa Barrick North Mara , kilichowakutanisha viongozi wa serikali za vijiji na baadhi ya watendaji wa halmashauri ya wilaya ya Tarime. Mwenyekiti wa kikao hicho akiwa ni DC Gowele .
Viongozi wa serikali za vijiji 11 vinavyozunguka mgodi wa Barrick North wakiwa kwenye kikao cha kujadili maendeleo kilichofanyika ndani ya mgodi wa Barrick North Mara, Februari, 20, 2026.
" Mimi nilishaanza kukimbizana nao najua taarifa mnayo na niliongea na Meneja wa mgodi hatuhitaji wakandarasi Wababaishaji , tutaenda nao sambamba hatuwahitaji tutachukua hatua . Ambaye anakuja kufanya kazi ya ubabaishaji atafute sehemu nyingine " amesema DC Gowele.
" Mgodi unatoa fedha kwa wakati mkandarasi unapewa fedha alafu unachelewa kumaliza kazi. Hatuwezi kukubali na mimi nitatoa ushirikiano , kwahiyo Mwenyekiti wa halmashauri ukiona kuna sehemu kuna chengachenga tuonane " amesema Mkuu wa Wilaya.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Tarime Matera Chacha , amesema kuna miradi inayojengwa kwa fedha za CSR imekwama haijakamilika kutokana na wakandarasi wasio waaminifu baada ya kupokea fedha hawaonekani .
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Tarime ambaye pia ni Diwani Kata ya Manga, Matera Chacha akizungumza kwenye kikao cha kujadili Maendeleo vijiji 11 vinavyozunguka mgodi wa Barrick North Mara.
" Naomba hili niliweke wazi kwenu mlifanyie kazi . Ni muda wa kuachana na Wakandarasi wasio waaminifu na wasiochapa kazi waondolewe ili miradi iendelee iweze kukamilika na kusaidia wananchi " amesema Matera .
Ameongeza kuwa ,wao kama halmashauri wamekuwa na ushirikiano na mgodi wa Barrick North Mara katika kutekeleza miradi mbalimbali ya CSR .
" Tumetekeleza miradi mbalimbali , miradi mingi imekamilika imebaki michache yenye changamoto. Lakini kupitia kikao hiki nilikuwa natoa wito kwa wadau wetu Barrick wasiwape kazi wakandarasi wazembe .
" Nitaendelea kutoa ushirikiano wa karibu kama halmashauri kuhakikisha mipango yote ya Barrick na halmashauri inakwenda vizuri "amesema Matera.
Mbunge wa Jimbo la Tarime vijijini , Mwita Waitara ameongeza kusema " Kwanini miradi inakwama wakati mgodi unatoa pesa na wao ndio wanaleta wakandarasi? . Naomba miradi iwe ya kipaumbele cha wananchi ibuliwe na wananchi ili ilete manufaa " amesema Waitara .
Mbunge wa Jimbo la Tarime vijijini , Mwita Waitara akizungumza kwenye kikao cha kujadili Maendeleo vijiji 11 vinavyozunguka mgodi wa Barrick North Mara.
Afisa anayehusika na miradi inayojengwa kwa fedha za uwajibukaji wa makampuni kwa jamii( CSR)kutoka mgodi wa Barrick North Mara, Hermence Christopher Lulah, ameeleza changamoto katika miradi ya maendeleo ikiwemo ucheleweshaji wa ukamilishaji wa miradi .
Amesema kwamba , baadhi ya wakandarasi spidi yao haiendani na malengo ya ukamilishaji miradi katika muda unaotakiwa.
Afisa anayehusika na miradi inayojengwa kwa fedha za uwajibikaji wa makampuni kwa jamii( CSR) Hermence Christopher Lulah, akiwaeleza viongozi wa vijiji 11 vinavyozunguka mgodi wa Barrick North Mara utekelezaji wa miradi ya CSR .
" Pia ubora, baadhi ya wakandarasi wasimamizi wao wa miradi sio wenye uelewa mzuri kuhusu ujenzi, hivyo kufanya baadhi ya wakandarasi kulazimika kubomoa majengo na hii ni moja ya changamoto kubwa.
" Suala la usimamizi tunategemea kutoka halmashauri,tumekubaliana kuajiri mtu ambaye atasimamia utekelezaji wa miradi . Kwa hiyo tutakuwa na injinia muda sio mrefu. Miradi ni mingi usimamizi unakuwa ni changamoto" amesema Hermence.
Ameongeza kuwa katika maeneo mengine ucheleweshaji wa miradi umetokana na changamoto ya miundombinu ya barabara isiyo rafiki .
" Kuna sehemu wakandarasi wamechelewa kukamilisha miradi kutokana na changamoto ya miundombinu hasa katika kufikisha vifaa kutokana na mvua kuwa nyingi imechangia wachelewe kumamiza miradi na mabadiliko ya miradi yamechangia miradi kutokamilika kwa wakati" amesema.
Afisa huyo wa miradi ya CSR amesema miradi inayoendelea hadi sasa ni miradi 134 yenye thamani jumla ya Bilioni 13.7 inayotekelezwa na Wakandarasi mbalimbali.


.jpg)



.jpg)


.jpg)

Post a Comment