HEADER AD

HEADER AD

BARRICK NORTH MARA KUANZA UJENZI SOKO LA DHAHABU LA GHOROFA 3 NYAMONGO


>> Diwani Kata ya Matongo akerwa ucheleweshwaji wa miradi

>> Mwaka 2023 DIMA Online iliripoti kero ya wafanyabiashara ya madini Nyamongo kutumia jengo finyu wakitaka wajengewe soko la madini la kisasa

Na Mwandishi Wetu, Nyamongo.

MGODI wa Dhahabu uliopo Nyamongo wilayani Tarime mkoa wa Mara, upo mbioni kujenga soko la dhahabu jengo la ghorofa tatu ambalo ujenzi wake utaanza mwezi , Aprili ,2026.

Hayo yameelezwa katika kikao kilichofanyika Februari , 20, 2026, kilichoandaliwa na mgodi wa Barrick North Mara , kilichowakutanisha viongozi wa serikali za vijiji na baadhi ya watendaji wa halmashauri ya wilaya ya Tarime, ambapo Mwenyekiti wa kikao hicho alikuwa mkuu wa wilaya ya Tarime Meja Edward Gowele .

Afisa anayehusika na miradi inayojengwa kwa fedha za uwajibikaji wa makampuni kwa jamii( CSR) Hermence Christopher Lulah, ametoa ufafanuzi kuchelewa kuanza kwa mradi wa ujenzi wa soko la dhahabu.

Afisa anayehusika na miradi inayojengwa kwa fedha za uwajibikaji wa makampuni kwa jamii( CSR) Hermence Christopher Lulah, akiwaeleza Mara utekelezaji wa miradi ya CSR , Viongozi wa serikali za vijiji 11 vinavyozunguka mgodi wa Barrick North .

" Huu ni mradi mkubwa wa kimkakati tulikuwa na hatua za usanifu, tulitafuta mtaalam wa usanifu ambaye alifanya usanifu na amekaribia kumaliza. Kumekuwa na marekebisho ya mara kwa mara ili mradi uweze kutekelezeka.

" Mara ya kwanza mchoro ulifanyika gharama zikaonekana ni kubwa sana tukarudi tena kuanza upya . Uchorongaji umefanyika mtaalam amechukua sampo ili kwenda kupima udongo , kuna vibali vya kuomba mamlaka mbalimbali " amesema Hermence .

Ameongeza kuwa mradi huo ulichukua muda mrefu kulingana na ukubwa wa jengo la ghorofa tatu na kwamba kwa awamu ya kwanza ujenzi utagharimu Tsh. Milioni 800.

      Viongozi wa serikali za vijiji 11 vinavyozunguka mgodi wa Barrick North wakiwa kwenye kikao cha kujadili maendeleo kilichofanyika ndani ya mgodi wa Barrick North Mara, Februari, 20, 2026.

" Jengo hili litakuwa na vyumba vya kupangisha , eneo la soko la dhahabu. Kwa ujumla awamu ya kwanza tupo asilimia 90 na tumeshakubaliana ujenzi utaanza mwezi wa nne .

Ameongeza kuwa mradi wa stendi ya Nyamwaga awamu ya kwanza ujenzi utagharimu Tsh. Milioni 327.5 , jengo litakalokuwa na maduka 79, jengo la kupumzikia abiria na eneo la maegesho ya magari.

Awali akizungumza katika kikao hicho ,Diwani wa Kata ya Matongo kupitia chama cha Mapinduzi ( CCM) Godfrey Kegoye, alitaka kufahamu ni lini miradi ya kimkakati ambayo ni soko la dhahabu katika kata ya Matongo, soko na stendi ya magari katika kata ya Nyamwaga itajengwa ?.

         Mkuu wa Wilaya ya Tarime Meja Edward Gowele (wa kwanza kulia), katikati ni Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Tarime, Matera Chacha , Diwani wa Kata ya Matongo kupitia chama cha Mapinduzi (CCM) Godfrey Kegoye (wa kwanza kushoto) wakiwa kwenye kikao cha kujadili Maendeleo vijiji 11 vinavyozunguka mgodi.

Diwani Godfray amesema kwamba katika Kijiji cha mjini kati kulikuwa na soko la jamii la bidhaa mbalimbali lakini lilibomolewa ili kupisha ujenzi wa soko la dhahabu lakini imepita miaka miwili bila ujenzi huo kuanza.

Amesema hali hiyo imekuwa ikilalamikiwa na wananchi kubomolewa soko lakini hawaoni utekelezaji wowote wa soko la madini.

" Tuliwabomolea soko wakazi wa Kata ya Matongo ili wapishe ujenzi wa soko la dhahabu lakini wananchi wamekuwa wakilalamika kwa kubomolewa soko lao na hawaoni mradi unaoendelea huu ni mwaka wa pili.

" Pale Nyamwaga tuliweka mradi wa stendi na soko lakini hadi leo mradi haujaanza, miradi hiyo tuliipitisha kuwa itajengwa kupitia fedha za CSR" amesema Diwani Godfray.

Mkuu wa Wilaya ya Tarime Meja Edward Gowele, akiwa Mwenyekiti wa kikao alitoa fursa kwa viongozi wa serikali za vijiji 11 kutoa maoni na changamoto zao ambazo ziliweza kupata majibu kupitia uongozi wa mgodi na watendaji wa halmashauri ya wilaya ya Tarime.

Rejea 
 >> Desemba, 13, 2023 chombo hiki cha habari kiliripoti habari yenye kichwa cha habari isemayo ' Wafanyabiashara soko la dhahabu Nyamongo wataka wajengewe soko la kisasa' 

 https://www.dimaonline.co.tz/2023/12/wafanyabiashara-soko-la-dhahabu.html?m=1

    Jengo la soko la madini Nyamongo ambalo ni finyu.

Mwenyekiti soko la dhahabu Nyamongo, Mwita Samson pamoja na wafanyabiashara ya madini walisema haiwezekani waendelee kutumia jengo finyu lisilo na upana linalowapa kero na kubanana hilihali serikali inakusanya fedha nyingi zitokanazo na madini ya dhahabu Nyamongo .

       Mwenyekiti soko la dhahabu Nyamongo, Mwita Samson akieleza kero soko la dhahabu Nyamongo, miaka mitatu iliyopita.

Wafanyabiashara ya madini walitoa kero zao wakati walipotembelewa ofisini kwao na Mwenyekiti wa wafanyabiashara ya madini Tanzania , Stephen Masumbuko , mwanasheria wa shirikisho la vyana vya wachimbaji wa madini Tanzania (FEMATA), Majina Owino .

Wengine ni maafisa kutoka Tume ya madini makao makuu Dodoma , Katibu msaidizi wa wachimbaji wadogo wa madini mkoa wa Mara na maafisa wa madini mkoa wa Mara.

    Mwenyekiti wa wafanyabiashara ya madini Tanzania , Stephen Masumbuko akitoa elimu ya umuhimu wa vitambulisho vya wachimbaji wa madini, wachenjuaji na wafanyabiashara ya madini ,miaka mitatu iliyopita.

Viongozi hao walifika ofisini kutoa elimu ya umuhimu wa wachimbaji wa madini, wachenjuaji  na wafanyabiashara ya madini kuwa na vitambulisho vya uchimbaji na hivyo wafanyabiashara kutumia nafasi hiyo kueleza kero zao.

      Mwanasheria wa shirikisho la vyana vya wachimbaji wa madini Tanzania (FEMATA), Majina Owino akisikiliza kero za wachimbaji na wafanyabiashara ya madini, miaka mitatu iliyopita .


No comments