MBUNGE KOKA: UCHAGUZI UMEPITA KILICHOBAKI NI KUWAHUDUMIA WANANCHI
Na Gustaphu Haule,Pwani
MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka ameanza utekelezaji wa majukumu yake kwa kishindo huku akisema uchaguzi umepita na kilichobaki kwasasa ni kuwahudumia wananchi wote bila kujali nani alimpigia kura na nani hakumpigia kura.
Amesema kuwa yeye ni mbunge mzoefu aliyekaa madarakani miaka 15 na akifika mwaka 2030 atakuwa amekaa madarakani miaka 20 kwahiyo anajua anachokifanya.
Amewaomba wanachama wa CCM kuacha kusikiliza propaganda za watu wachache wasiokuwa na nia njema na Jimbo la Kibaha Mjini na badala yake wajenge ushirikiano katika kuhakikisha Kibaha inapata maendeleo zaidi.
Ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na viongozi wa CCM kutoka Kata mbalimbali katika kikao maalum cha Halmashauri Kuu ya CCM Kibaha Mjini kilichofanyika Februari 21/2026 katika ukumbi wa Kibaha Mall kilichofanyika kwa ajili ya kufanya mapokezi ya Mbunge huyo.
Mbunge wa Kibaha Mjini Silvestry Koka apokea boksi la zawadi kutoka kwa viongozi wa CCM Kata ya Mkuza katika hafla ya mapokezi yake yaliyofanyika Februari 21/2026 Kibaha Mall.Amesema wakati wa kampeni za uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 CCM kupitia Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, wabunge na madiwani walitoa aadi nyingi kwahiyo kipindi hiki ni kipindi cha kuhakikisha kazi zinafanyika ili kurudisha imani kwa Wananchi waliowachagua.
Amesema kuwa anawashukuru wanaCCM na Wananchi kwa ujumla kwa kazi kubwa waliyoifanya kuhakikisha wanamchagua kuwa mbunge japokuwa hakuwepo Kibaha kutokana na changamoto ya kiafya lakini kwasasa amerudi Jimboni na kazi itaendelea kama kawaida.
Amesema Oktoba 2025 alipata changamoto ya kiafya na kulazimika kusafiri kwenda Marekani katika Jimbo la Texas kwa ajili kupata matibabu yakibingwa lakini kipindi hayupo Wananchi walimpigania na kufanikiwa kushinda kwa asilimia 94 huku Rais Samia akishinda kwa asilimia 98.
Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka (katikati) akiwa amevalishwa zawadi ya Mgoroli kutoka kwa Wanawake wa UWT Kibaha Mjini.Mbunge huyo amesema kazi hiyo ni kubwa na imempa faraja kuona jinsi ambavyo Wananchi wamejitoa kwa ajili yake kwahiyo hana chakuwalipa zaidi ya kuhakikisha changamoto zote anazifanyiakazi ikiwemo suala la maji na barabara.
"Naomba kutumia fursa hii kuwashukuru ninyi wote ambapo mmenipa ushirikiano tangu naanza kugombea ubunge Jimbo la Kibaha Mjini hadi katika uchaguzi wa mwaka 2025 na kwasasa ninyi ni ndugu zangu tutaendelea kushirikiana hadi kieleweke,"amesema Koka
Koka amesema kwakuwa viongozi wa CCM alioanzanao wapo na yeye yupo lakini kama kutoka basi watoke wote huku akisema kwasasa anajipanga kuanza ziara ya chama kwa ajili ya kuwashukuru viongozi wa Chama na baadae kufanya ziara ya nje kwa ajili ya kuwashukuru Wananchi na kutatua changamoto zao.
Katika Mkutano huo,Koka alipokea zawadi mbalimbali kutoka kwa viongozi wa Kata hizo ikiwemo Mbuzi,Vitenge,Kuku na vitu vingine mbalimbali ambapo hatahivyo Koka alishukuru zawadi hizo na kusema kwake ni deni kubwa katika kuwatumikia Wananchi .
Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka (kushoto) akipokea zawadi ya Kuku kutoka kwa Mwenyekiti wa CCM Kata ya Mailimoja Mathayo Mkayala katika hafla ya mapokezi ya Mbunge huyo yaliyofanyika Februari 21/2026 Kibaha mall.Hata hivyo katika kikao hicho Koka alimpokea mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)Kata ya Mkuza John Kirumbe aliyeamua kuhamia CCM kwa madai kuwa maamuzi ya kuhamia CCM yametokana kauli ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan yakusema "Wananchi watii Mamlaka",.
Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka ( kushoto)akimpokea aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema Kata ya Mkuza John Kirumbe baada ya kuhamia CCM Februari 21/2026 katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Kibaha Mjini.Mwenyekiti wa CCM Kibaha Mjini Mwajuma Nyamka amesema kuwa amefurahi kuona mbunge huyo yupo salama kwakuwa wakati mbunge hayupo alikuwa akiulizwa maswali mengi magumu.
Nyamka amesema hata aliporudi watu waliona picha za mapokezi yake na watumishi wa Manispaa ya Kibaha lakini bado waliuliza na yeye akajibu hajarudi lakini alipoapishwa ndipo akapata majibu sahihi kuwa mbunge amerudi
"Leo natangaza rasmi kuwa mbunge amerudi Bungeni, Mbunge amerudi Jimboni, na mbunge amerudi kazini, kwahiyo kila kitu kitaenda sawa na ninachowaomba ni kuendelea kumpa ushirikiano Mbunge ili aweze kutekeleza majukumu yake sawasawa,",amesema Nyamka.
Mwenyekiti wa CCM Kibaha Mjini Mwajuma Nyamka ( Kulia) akimkabidhi zawadi ya Kitenge Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka katika hafla ya mapokezi iliyofanyika Februari 21/2026 Kibaha mall.





Post a Comment