MALALAMIKO YANAYOWASILISHWA BARRICK NORTH MARA YAPUNGUA KUTOKA MALALAMIKO 105 HADI 16
>> Meneja mkuu Barrick North Mara asema chanzo ni mabadiliko chanya ya kimahusiano
Na Mwandishi Wetu, Nyamongo
IMEELEZWA kuwa malalamiko ya watu mbalimbali dhidi ya mgodi wa Barrick North Mara, yameeendelea kupungua ikilinganishwa na miaka ya nyuma iliyopita.
Meneja mkuu wa mgodi wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko amesema chanzo cha malalamiko kupungua ni kutokana na mahusiano makubwa chanya kuzidi kuhimarika baina ya mgodi na jamii inayouzunguka.
Meneja mkuu Mgodi wa Barrick North Mara , Apolinary Lyambiko akizungumza na viongozi wa serikali za vijiji 11 vinavyozunguka mgodi wa Barrick North Mara katika kikao cha kujadili maendeleo Februari, 20, 2026
Apolinary ameeleza hayo wakati wa kikao cha Barrick North Mara cha hivi karibuni , kilichowakutanisha viongozi wa serikali za vijiji 11 vinavyozunguka mgodi huo, baadhi ya Madiwani na watendaji wa halmashauri .
Wengine ni Mwenyekiti wa wachimbaji wadogo wa madini mkoa wa Mara, David Bitta, Afisa madini mkoa wa Mara, Daniel Mapunda , mbunge wa Jimbo la Tarime vijijini , Mwita Waitara ambapo Mwenyekiti wa kikao hicho alikuwa ni mkuu wa wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele .
" Kuna mabadiliko makubwa chanya ya kimahusiano katika mgodi na jamii inayouzunguka. Tunajivunia mazungumzo ya wazi yameongezeka , ushirikiano kati ya mgodi , viongozi wa serikali, jamii umeongezeka .
" Imani pande zote imeendelea kukua, migogoro mingi imepatiwa ufumbuzi kwa njia ya mazungumzo.
Mgodi unaendelea kufanya shughuli zake bila muingiliano kutoka kwenye jamii " amesema Apolinary.
Ameongeza kuwa ujenzi wa miradi mbalimbali inayojengwa kwa fedha za mgodi zikiwemo fedha za uwajibikaji wa makampuni kwa jamii (CSR) kutoka mgodi wa Barrick North Mara , ikiwemo miradi ya afya, maji, elimu, kilimo, zabuni kwa wazawa ,miundombinu ya barabara imekuwa ni chachu katika kujenga mahusiano mazuri baina yao na vijiji vinavyozunguka mgodi .
" Mgodi umekuwa ukiendelea kutekeleza miradi mbalimbali , mingine imekamilika na mingine inaendelea kutekelezwa kama vile ujenzi wa madarasa, vyoo, nyumba za watumishi ,ujenzi na maboresho vituo vya afya ,miundombinu ya barabara na miradi mingine .
" Lengo letu si kuchimba tu dhahabu bali kusaidia kuboresha maendeleo ndani ya jamii na hii imezi kuleta mabadiliko chanya ya mahusiano" amesema Apolinary.
Meneja Mahusiano mgodi wa Barrick North Mara, Francis Uhadi, amesema mgodi umekuwa ukipokea malalamiko na kuyatafutia ufumbuzi na hivyo malalamiko kuendelea kupungua.
Meneja Mahusiano mgodi wa Barrick North Mara, Francis Uhadi akizungumza na viongozi wa serikali za vijiji 11 vinavyozunguka mgodi wa Barrick North Mara katika kikao cha kujadili maendeleo Februari, 20, 2026.
Amesema mwaka 2018 malalamiko yaliyowasilishwa Barrick yalikuwa 84, 2019 malalamiko 105, 2020 malalamiko 92, mwaka 2021 malalamiko 72, 2022 malalamiko 41, 2023 malalamiko 55, 2024 malalamiko 44 na mwaka 2025 malalamiko yalipungua hadi 16.
" Ofisi ya Kijiji tumeweka daftari la kupokea malalamiko na kuyawasilisha kwetu lakini pia tumeimarisha daftari kwenye ofisi ya DC kwasababu kuna watu wanapeleka malalamiko lakini pia ofisi ya mkuu wa mkoa .
" Tumetengeneza mahusiano ya pamoja kuhakikisha kwamba yanapotokea malalamiko yoyote yanayohusiana na mgodi tunapeana taarifa za haraka .
Ameongeza " Mwaka jana tulianzisha Kliniki ya malalamiko tunayoendelea nayo . Tunatambua malalamiko yanaweza yakawa yanahusu serikali au yanahusu mgodi . Kwahiyo tumetengeneza kamati ya pamoja ambayo tunashirikiana katika kushughulikia malalamiko" amesema Francis.
Afisa anayehusika na miradi inayojengwa kwa fedha za uwajibikaji wa makampuni kwa jamii ( CSR)kutoka mgodi wa Barrick North Mara, Hermence Christopher Lulah, amesema utekelezaji wa miradi ya CSR imepunguza malalamiko.
Afisa anayehusika na miradi inayojengwa kwa fedha za uwajibikaji wa makampuni kwa jamii( CSR) Hermence Christopher Lulah, akiwaeleza viongozi wa vijiji 11 vinavyozunguka mgodi wa Barrick North Mara utekelezaji wa miradi ya CSR Februari, 20, 2026.
" Mgodi hutoa kila mwaka CSR kwa ajili ya utekelezaji wa miradi . Mwaka 2019-2024 mgodi umeshatoa fedha kiasi cha Bilioni 26 zilizokwenda kutekeleza miradi ya maendeleo zaidi ya 250 .
" Miradi mingi ipo kwenye sekta kama vile maji, barabara , afya, elimu na mingineyo . Asilimia kubwa ya miradi ni kwenye elimu ya msingi na sekondari . Tumekuwa tukitekeleza takwa la kisheria lakini pia tunatoa fedha nje ya CSR.
" Wakati mwingine tunashirikiana na jamii au viongozi pale dharura zinapojitokeza mgodi uchagia . Miradi inayoendelea kwa sasa ni 103 ambayo iko kwenye sekta tofauti tofauti . Utekelezaji wa miradi hii gharama yake ni Bilioni 13. 7 ambazo mgodi unatekeleza baada ya zile kanuni kutolewa 2023 ambazo zilitaka mmiliki wa leseni kutekeleza miradi .
Ameongeza kusema " miradi iliyokamilika ni 51 , na mingine tunaendelea kukabidhi kwa jamii tukishirikiana na halmashauri. Miradi viporo ni 31 inaendelea kutekelezwa na halmashauri.
Mmoja wa Viongozi wa serikali za vijiji 11 vinavyozunguka mgodi wa Barrick North akizungumza kwenye kikao cha kujadili maendeleo kilichofanyika ndani ya mgodi wa Barrick North Mara, Februari, 20, 2026
" Walihitaji nyongeza ya fedha tuliongeza kiasi karibu Tsh. Milioni 800 ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika, ukijumlisha miradi yote inayoendelea hadi sasa ni jumla ya miradi 134 yenye thamani ya Bilioni 13.7 " amesema Hermence.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Tarime, Matera Chacha ameushukuru mgodi huo kuwakutanisha viongozi wa vijiji vinavyozunguka mgodi .
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Tarime ambaye pia ni Diwani Kata ya Manga, Matera Chacha akizungumza kwenye kikao cha kujadili Maendeleo vijiji 11 vinavyozunguka mgodi wa Barrick North Mara Februari, 20, 2026.
Ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa karibu kama halmashauri kuhakikisha mipango yote ya Barrick na halmashauri inaendelea vizuri.
Mkuu wa wilaya ya Tarime, Edward Gowele ameushukuru uongozi wa mgodi kufanya kikao cha pamoja na wenyeviti wa vijiji 11 vinavyozunguka mgodi, viongozi wa dini, Madiwani , maafisa tarafa , watendaji kutoka kata zinazozunguka mgodi pamoja na viongozi wengine ngazi ya halmashauri na mkoa wa Mara.
Mkuu wa Wilaya ya Tarime , Meja Edward Gowele , akizungumza wakati wa kikao cha Mgodi wa Barrick North Mara, kilichowakutanisha viongozi wa serikali za vijiji 11 vinavyopakana na mgodi, kilichojadili masuala mbalimbali ya maendeleo, Februari 20,2026.
" Tangu nifike hapa ndio kikao changu cha kwanza cha kuwakutanisha wenyeviti wote wa vijiji vinavyozunguka mgodi hayo ni mahusiano mema . Afisa mahusiano nakupongeza sana unafanya kazi nzuri
" Changamoto zilizokuwepo huko nyuma ni tofauti na sasa. Tuendelee kushirikiana tutatue kero za wananchi, tuendelee kuwa na mahusiano mazuri na ushirikiano. Nimeona miradi mingi imetekelezwa , hii ni kwasababu ya uwepo wa mgodi .
Mkuu huyo wa wilaya ameomba vikao viwe endelevu kwakuwa ni vikao shirikishi na kwamba wasisite kumwalika kwenye vikao huku akisisitiza ushirikiano baina ya vijiji na mgodi na kuwataka wenyeviti wasisite kutatua migogoro na wasiwe sehemu ya kutengeneza migogoro.

.jpg)


.jpg)















.jpg)





Post a Comment