SERIKALI YA KIJIJI MRITO YAMTETEA KIKONGWE ALIYEBOMOLEWA NYUMBA, YAKANUSHA KUMPATIA ARDHI MWEKEZAJI SAMWEL NGOCHO
>>Kikongwe aliyebomolewa nyumba hasikii vizuri, hajui kuongea Kiswahili, Kijana wake mkubwa ni bubu
>> Serikali ya Kijiji imesema ilimuonesha Mwekezaji ardhi kwa ajili ya utafiti wa madini ya Malumalu na si kumiliki
>>Samwel Ngocho asema serikali ya Kijiji ilimmilikisha ardhi
Na Mwandishi Wetu, Tarime
HOFU imetanda kwa wakazi wa Kijiji cha Murito ,Kata ya Kemambo- Nyamongo, wilaya ya Tarime mkoani Mara, baada ya kushuhudia ubomoaji wa nyumba tano za mzee wa Mila, Chacha Wansinyo Chango mwenye umri wa miaka 90, mkazi wa Kitongoji cha Miriminsi , Kata ya Kemambo .
Nyumba za Chacha Wansinyo zilizobomolewa kwa kibali cha mahakama ya ardhi na nyumba wilaya ya Tarime, mkoani Mara.
Nyumba hizo zimebomolewa kwa amri ya mahakama ya ardhi na nyumba wilaya ya Tarime , baada ya mlalamikaji Samwel Ngocho mkazi wa Kijiji cha Kerende katika kata hiyo kushinda kesi ya ardhi dhidi ya Chacha Wansinyo . Samweli Ngocho alifungua kesi ya ardhi dhidi ya Chacha mwaka 2016 na kutolewa hukumu mwaka 2018.
Samwel alikazia hukumu mwaka 2025 huku akidai kuwa Chacha Wansinyo alivamia na kujenga nyumba kwenye ardhi yake aliyopewa na Serikali ya Kijiji cha Mrito kwa ajili ya uwekezaji wa madini ya Malumalu na madini ya dhahabu .
Madini ya malumalu ni mawe ya asili yenye rangi mbalimbali (kama kahawia, kijivu, nyekundu au mchanganyiko wa rangi) yanayotumika sana katika ujenzi wa nyumba, hasa kwa kuta na mapambo.
Tarehe ,28,2026 , siku ya jumatano majira ya saa tisa alasiri ni siku ya majonzi ambayo haitasaulika katika maisha ya familia ya Chacha Wansinyo baada ya gari aina ya tingatinga maarufu Greda kufika nyumbani na kubomoa nyumba zao.
Gari hilo likiendeshwa na dereva , ndani ya gari akiwemo Samwel Ngocho na dalali wakiwa wamesindikizwa na askari Polisi waliokuwa katika gari la Polisi. Walifika nyumbani kwa mzee Wansinyo, punde si punde zoezi la ubomoaji wa nyumba likatekelezwa huku wananchi wakishuhudia.
DIMA Online , ilifika nyumbani kwa mzee Wansinyo na kushuhudia nyumba zilizobomolewa huku baadhi ya vitu vikiwa vimefunikwa na undogo baada ya kuangukiwa na nyumba zilizobomolewa.
Familia yazungumza
Akiwa anatembea huku akiwa ameinama mkononi akiwa ameshika mkongojo , mzee Kikongwe Chacha Wansinyo anazipiga hatua kuelekea katika nyumba zake zilizobomolewa.
Mzee huyo asiyesikia vizuri na asiyejua kuongea kiswahili anazungumza kwa lugha ya Kikurya , kijana wake wa pili kuzaliwa ambaye pia ni mzee wa Mila analazimika kuwa mkalimani anatafsiri maneno hayo ya Kikurya kwa lugha ya Kiswahili.
Kikongwe huyo anaeleza maumivu anayoyapata baada ya kubomolewa nyumba zake katika ardhi yake anayodai kuimiliki tangu mwaka 2009 lakini sasa amenyang'anywa na Samwel Ngocho .
" Mimi nina wake watatu na watoto zaidi ya 20 na wajukuu kadhaa , kila mke anaishi kwenye eneo lake, hapa palipobomolewa ni kwa mke wangu wa tatu. Nilikuja kuishi hapa pakiwa ni pori sikukuta mtu yeyote aliyekuwa akiishi hapa.
" Mimi na watoto wangu tuliishi wenyewe katika eneo hili ,majirani zetu vilikuwa vichaka, miaka ya baadae ndio wakaja watu wachache wakajenga nikapata majirani , alafu anatokea mtu kutoka Kijiji jirani anasema eneo hili ni lake eti aliuziwa na Kijiji !.
" Rais Samia , awali nilikuwa naishi kwenye nyumba za nyasi, lakini nilipambana kupitia shughuli za kilimo na ufugaji nikajenga nyumba nne za bati na moja ya nyasi .
" Watu wasio na huruma bila kujali umri wangu wamenibomolea nyumba zangu kwenye ardhi yangu. Rais Samia nisaidie myonge naonewa, nimebomolewa nyumba zangu ambazo nimezijenga kwa tabu kupitia kilimo na ufugaji " anasema Chacha.
Akizungumzia mwenendo wa kesi aliyofunguliwa na Samwel Ngocho, anasema alihudhulia mara chache kwenye kesi yake . Kutokana na yeye kutosikia vizuri hakuweza kufahamu tarehe za kesi na hivyo kutohudhuria kila tarehe iliyopangwa jambo lililopelekea kesi kusikilizwa upande mmoja.
" Ntakwighwa bhuya, amatwi ghalibha ,ntamanyere ghusumancha ighiswahili ntakukighwa, Serikali mtanturya, mkuu wa wilaya tanturya , ( Sisikii vizuri masikio yangu yameziba, sijui kuongea kiswahili , serikali nisaidieni , mkuu wa wilaya nisaidie, ) anasema Chacha.
Anasema wakati nyumba zinaanza kubomolewa hakuwa nyumbani, alifika na kuwaona askari polisi nyumbani kwake wakisimamia ubomoaji wa nyumba zake" Nyumba zangu zilibomolewa chini ya ulinzi wa Polisi wanane kama sijakosea , nimekuta hadi TV yangu imeharibika ikiwa imeangukiwa na nyumba. Vyombo, vitanda vilifunikwa vyote hawakutupatia muda wa kutoa vyombo ndani"anasema.
Anaongeza " Samwel Ngocho alinishitaki kuwa nimevamia ardhi yake wakati si kweli, tangu aliponishtaki imepita miaka tisa. Nilikuwa naenda Tarime kusikiliza kesi ,wakati mwingine sikuijua tarehe ya kesi kwasababu nilikuwa sisikii wanachokiongea na wakati mwingine nilipofika mahakamani niliishia kukaa nje sikujua kinachoendelea .
"leo hii wamekuja kubomoa nyumba zangu, mke wangu na watoto tutaishi wapi natolewa kwenye ardhi niliyoishi peke yangu na familia yangu kwenye mazingira haya ya porini ." anasema.
Mzee huyo anaiomba serikali na wanasheria kuingilia kati ili haki itendeke arejee kwenye ardhi yake na kulipwa fidia ya uharibifu wa mali.
Mwita Chacha Wansinyo mwenye miaka 39 mkazi wa Kitongoji cha Nyabihero anasema " Mzee alikuja kuishi hapa Miriminsi kwa sababu ya mifugo ipate malisho. Alikuwa na ng'ombe wengi ,wengine aliwauza akajenga nyumba za bati ili asinyeshewe na mvua lakini zimebomolewa kwa amri ya mahakama.
"Samwel Ngocho alikuja Kitongoji cha Miriminsi kufanya utafiti wa vigae, na eneo aliloonyeshwa ni lile pale lakini cha ajabu akaenda kufanya anavyojua na kuja kusema kwamba eneo la mzee ni la kwake wakati si eneo lake yeye ndo mvamizi.
" " Sisi kama familia tulikuwa tunafuatilia kujua je ni kweli Samwel ana vibali vya kumiliki hili eneo, wakati tukiwa kwenye ufuatiliani tumeshangaa nyumba zinabomolewa . Mimi binafsi sijawahi kuona notes ya mahakama zaidi ya kuona zoezi la ubomoaji" anasema kijana wa Chacha Wansinyo.
Ghati Chacha mke wa mzee Chacha Wansinyo , anaiomba serikali kuingilia kati " Nyumba zangu zimebomolewa ,nina watoto 8 hatuna pakuishi, serikali tusaidie tunanyanyaswa" anasema Ghati.
Roma Mlange mwenye umri wa miaka 38 mkazi wa Kitongoji cha Miriminsi jirani na mzee Chacha Wansinyo anasema walimkuta mzee huyo katika eneo hilo ambaye kwa sasa amepakana na mwekezaji Kampuni ya Jafuro ya Waarabu ya uchimbaji wa dhahabu.
" Tumehamia hapa tukamkuta mzee Wansinyo akiishi hapa . Sisi tulihamia hapa mwaka 2012 tukamkuta huyu mzee ambaye amepakana na mwekezaji Kampuni ya Jafuro ya waarabu walioletwa na mwenyeji aitwaye mzee Matiko Nyamang'we .
" Tunaiomba serikali iingilie kati imsaidie huyu mzee anaonewa, walichokifanya ni ujanja ujanja. Huu mgogoro wa ardhi umekuwa ni mgogoro wa pili kwenye hiki Kitongoji .Serikali imsaidie huyu mzee maana amewahi kuuawa mzee mmoja anaitwa Marwa Masiaga alichinjwa na chanzo ilikuwa mgogoro wa ardhi " anasema Roma .
Kijiji chamkingia kifua Kikongwe
Serikali ya Kijiji cha Mrito imekana kumpatia ardhi Samweli Ngocho kwa ajili ya uchimbaji wa madini ya dhahabu na Malumalu na kwamba ardhi hiyo anayoishi Chacha Wansinyo ni eneo tengefu la Kijiji.
Mjumbe wa serikali ya Kijiji cha Murito tangu mwaka 2009 hadi sasa ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya ardhi halmashauri ya Kijiji, Jaston Matiko anasema " Serikali ya Kijiji haikumpatia Samwel ardhi isipokuwa ilimuonesha eneo kwa ajili ya kufanya utafiti wa madini ya mawe ya asili maarufu vigae (Malumalu) .
" Samwel alikuja akasema anataka kufyatua tofali za vigae kwamba ameona eneo karibu na daraja la mto Mara. Kamati ya ardhi ikaenda kuona hilo eneo analotaka .
" Tukapiga hatua hilo eneo alilotaka kufanya utafiti wa vigae . Mimi ndiye niliyekuwa nakanyaga hatua za miguu , urefu hatua 550 na upana hatua 300. Eneo la huyu mzee halikuwa ndani ya hatua za utafiti lilikuwa nje , nashangaa Samwel anasema ni la kwake na kumbomolea nyumba zake.
Jaston anaongeza kusema " Kila Mwenyekiti wa Kijiji anayeingia hukataa habari za huyo Samwel na barua zake za kugushi, serikali iingilie kati hili jambo wanyonge nao wana haki wasionewe " anasema Jaston .
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Miriminsi, Mwita Marwa Masero anasema" nimekuwa Mwenyekiti wa Kitongoji hiki tangu mwaka 2014 hadi sasa . Huyu mzee Chacha wakati anajenga nyumba kwenye hili eneo hapakuwa na mtu yeyote aliyekuwa anaishi hapa.
" Samwel alifungua kesi ambayo hukumu yake ilitolewa mwaka 2018 alishinda kesi mahakama ikaamuru Chacha apishe kwenye eneo. Mwaka 2025 mwezi wa nne Samwel akaleta Notes iliyoletwa na dalali ikimtaka mzee Chacha ahame kwenye eneo hilo ndani ya siku 14 .
" Lakini Kijiji kilikataa kwasababu Chacha ndiye mwenye eneo na si Samwel , miezi michache kupita nikaona greda linabomoa nyumba za Chacha Wansinyo. Niliomba nione barua ya notes ilikuwa ni ya tarehe 3/11/2025 na wao wamekuja kubomoa tarehe 28/1/2026.
Mwenyekiti mstaafu Kijiji cha Mrito , Joseph Mangure anasema kwamba Samwel Ngocho aliomba serikali ya Kijiji aoneshwe eneo kwa ajili ya kufanya utafiti tu haikumpatia ardhi ya kumiliki na kwamba alichokifanya ni udanganyifu.
Mwenyekiti mstaafu Kijiji cha Mrito , Joseph Mangure akionesha nyumba za Chacha Wansinyo zilizobomolewa.
" Mwaka 2011 Samwel Ngocho alifika ofisini nikiwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Mrito akiomba apewe eneo kufanya utafiti wa kuchimba vigae vya ujenzi . Serikali ya Kijiji ilimwonesha eneo afanye utafiti kwa miezi mitatu na baada ya hapo atupatie mrejesho wa utafiti wake .
" Chakushangaza alikaa miezi sita bila kuleta taarifa zozote za mrejesho wa utafiti wake . Ilibidi tumuite maana hilo eneo lilikuwa ni tengefu la serikali ya kijiji kwa ajili ya malisho. Alipofika alisema ana barua na vibali kutoka kwa afisa madini mkoa wa Mara vya kumruhusu kumiliki ardhi hiyo.
" Tulimuomba atuoneshe hizo barua ,tukamuuliza wewe tumekupa kibali cha kufanya utafiti wewe unakuja na barua za umiliki ardhi nani aliyekupa hiyo ardhi? manaa ardhi ni ya Kijiji ili itolewe kwa mtu kuna taratibu zake ukiwemo mkutano mkuu wa wananchi ndo wenye maamuzi ya kumruhusu mwekezaji kuwekeza kwenye ardhi ya Kijiji .
" Tuligundua ni tapeli tukamwambia aondoe mitambo yake aondoke na mkutano mkuu wa Kijiji ulimkataa . Eneo la utafiti lilikuwa ni ekari 2 ,lakini sasa amepora ardhi inayokadiliwa kuwa ekari 50 akidai ni eneo lake alilomilikishwa na ofisi ya madini .
Mwenyekiti huyo anasema barua za Samwel Ngocho ni za kugushi " Kwenye serikali yangu hakukuwa na hiyo kesi baina yake na Chacha Wansinyo , Hata Mwenyekiti wa Kijiji aliyefuata Yakobo alimfukuza alipogusia suala la hiyo ardhi.
"Wenyeviti wote wa vijiji katika serikali zao walimfukuza hata Mwenyekiti Mahati alimfukuza na mimi nilimfukuza kutokana na mambo yake ya utapeli.
" Tunaiomba serikali iingilie kati huyu mzee Chacha apate haki yake . Anaishi eneo tengefu lakini kutokana na kukaa miaka mingi hatukumfukuza kwasababu lile eneo ni tengefu bado tulikuwa na uwezo wa kutenga maeneo ya makazi" anasema Joseph.
Anaongeza kusema " Huyu mzee anatia huruma ana miaka zaidi ya 90, ana watoto zaidi ya 20 na wajukuu . Anamtunza kijana wake mkubwa ambaye ni bubu . Serikali ya Kijiji haimtambui Samwel kama mwekezaji wala haina barua ya Samwel Ngocho ya umiliki wa ardhi. Serikali ndiyo ina ardhi sasa yeye kapewa na nani ardhi? " anauliza.
Mwenyekiti wa sasa wa Kijiji cha Mrito Joseph Manga anasema alipigwa simu kutoka Polisi Nyamwaga wakimtaka kufika katika eneo hilo la mgogoro kwa ajili ya utekelezaji wa ubomoaji wa nyumba za Chacha Wansinyo.
Mwenyekiti wa sasa wa Kijiji cha Mrito Joseph Manga
" Nilipigiwa simu na OCD wa Nyamwaga nikaenda kituo cha Polisi Mrito wakaniambia kuna hati ya ubomoaji wa nyumba . Mimi nikasema hilo jambo silifahamu sitaenda. OCD akasema kama sitaki kwenda niandike barua iende mahakamani ilibidi tu niende.
" Tulipofika kwenye tukio tulikuta Samwel ametangulia eneo la mgogoro akiwa kwenye greda . Nilimuomba Samwel asibomoe akasema kama tunamzuia turudishe gharama alizoleta greda ,Polisi, madalali. Tukamuuliza ni sh. ngapi? akasema mpaka afikilie .
" Muda mfupi tulishtukia nyumba zinabomolewa nikishuhudia mwanzo hadi mwisho. Walibomoa nyumba za bati 3 za Magongo wa tembo, slop moja na nyumba moja iliyoezekwa kwa nyasi. Vitu vyote, vyombo, vilifukiwa ndani ya udongo " anasema Manga.
Mwenyekiti huyo anasema awali baada ya Samwel Ngocho kutoonesha nyaraka za umiliki wa ardhi alisema hamtambui kama mwekezaji .
" Mwaka jana mwezi wa nne Samwel Ngocho alifika ofisini kwangu akiwa na barua ya hukumu ya kesi na barua ya notes akiwataka hawa watu waondoke .
" Nilimwambia anipe nyaraka za barua zinazomtambulisha kuwa ni mmiliki halali wa ardhi ikizingatiwa huo mwaka 2011 anaosema kuwa Kijiji kilimpatia ardhi mimi nilikuwa ni mjumbe wa halmashauri ya Kijiji na nafahamu hakupewa ardhi.
" Alinionesha kopi ya barua ya kamati ya ardhi aliyodai ilipima ardhi tarehe 13,10,2011. Baada ya kunionesha niliomba anipe muhtasari wa halmashauri ya Kijiji, muhtsari wa mkutano mkuu wa Kijiji uliomuhidhinisha lakini hakutoa " anasema Mwenyekiti.
Mwenyekiti huyo wa Kijiji cha Mrito anaiomba serikali iingilie kati imtake Samwel Ngocho aoneshe nyaraka zinazomuhalalisha kuchukua eneo ambalo anaishi Chacha Wansinyo.
Ameiomba serikali kuangalia kwa jicho la pili kwani mzee Chacha ameishi katika eneo hilo kwa miaka mingi imsaidie ili apate sehemu ya kuishi.
Ngocho asema Kijiji kilimpatia ardhi
Mwekezaji Samwel Ngocho anasema anashangaa kusikia kwenye vyombo vya habari kuwa serikali ya Kijiji cha Mrito inakana kutompatia ardhi kwamba ilimpatia kibali cha kufanya utafiti wa madini ya Malumalu jambo ambalo si la kweli anachokifahamu yeye halmashauri ya Kijiji ilimpatia ardhi ya juu mwaka 2011 kwa ajili ya uchimbaji wa madini.
Anasema kuwa, Chacha Wansinyo alivamia eneo lake alilolimiliki mwaka 2011 na ana leseni ya umiliki ya uchimbaji wa madini ya dhahabu na madini ya Malumalu .
Anasema kuwa eneo hilo lilikuwa ni pori kubwa ,halikuwa eneo tengefu la Kijiji bali wananchi walikuwa akijitwalia eneo kulingana na ukubwa anaoutaka.
" Nashangaa kusikia viongozi wa serikali ya Kijiji cha Mrito wanasema kwamba hawakunipatia eneo la uchimbaji bali ilinionesha eneo kwa ajili ya uchimbaji tu. Nakanusha kauli hiyo si ya kweli waliniruhusu kuwekeza katika uchimbaji wa dhahabu na vigae (Malumalu).
" Mwaka 2011 nilikuja kuomba eneo kwa ajili ya kuchimba vigae wakati huo lilikuwa ni pori , watu walikuwa wanajishikia maeneo . Nilikuta watu wawili tu waliokuwa wanaishi kwenye eneo hilo ambao ni mzee Cosmas na Mwita Mwikwabe ambao wapo kwenye ile ramani ya ardhi niliyopewa kwa ajili ya uchimbaji wa madini.
Anaongeza kusema " Huyo Chacha Wansinyo alihamia kwenye eneo langu mwaka 2014 kama wanabisha waulizwe majirani wawaambie nani alimtangulia mwenzake ,kwa sababu hata ndugu zake wengine waliovamia na kuishi kwenye eneo langu waliondoka kwa hiari .
" Istoshe, mimi nilipenda ardhi iliyokuwa karibu na mto Mara lakini wao walinipeleka kwenye eneo walilodai halina mtu ni la Kijiji. Kijiji hakina mamlaka ya kutoa kibali cha utafiti isipokuwa ofisi ya madini wao wanatoa tu ardhi ya juu. Nilienda ofisi ya madini kuomba kibali cha leseni wakaniambia siwezi kupewa bila kupata kibali cha ardhi ya juu.
" Nilienda halmashauri ya Kijiji , kamati ya ardhi ilitumwa kunionesha eneo na ilinipatia ardhi ekari 12 , na siku wananipatia eneo walikuwa na kitabu cha sheria wakanisomea wakasema kamati ya ardhi inauwezo wa kutoa ardhi ekari 1-49, ikivuka hapo mkutano mkuu ndio wenye mamlaka ya kutoa ardhi " anasema Samwel.
Samwel anaiomba serikali kuchunguza nani mmiliki halali wa ardhi ikiwa ni pamoja na kupitia vilelelezo na kwamba isisikilize maneno ya mdomoni tu lakini pia kila mjumbe aitwe mmoja mmoja ahojiwe kupata ukweli wa ardhi hiyo.
Itaendelea
Mzee Chacha Wansinyo wa kwanza kulia akiwa na vijana wake

















Post a Comment