JUMUIYA YA WAZAZI PWANI YAADHIMISHA MIAKA 49 YA KUZALIWA CCM KWA KUTOA MSAADA KWA WAHITAJI
Na Gustaphu Haule, Pwani
JUMUIYA ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kibaha Mjini kwa kushirikiana na Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Pwani, Februari 04/2026 wameadhimisha miaka 49 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi kwakufanya matendo ya huruma katika jamii mbalimbali iliyopo Kata ya Tangini Manispaa ya Kibaha.
Katibu wa Jumuiya ya Wazazi mkoa wa Pwani Yusuf Masombora ndiye alikuwa mgeni rasmi katika kuongoza shughuli za maadhimisho hayo akiwa na uongozi wa Jumuiya hiyo kutoka Wilaya ya Kibaha Mjini chini ya Mwenyekiti Yahaya Mtonda.
Makabidhiano msaada wa vifaa vya watoto, Wajawazito na wagonjwa katika zahanati ya Tangini hafla iliyofanyika Februari 04 baina ya Jumuiya ya Wazazi na wataalamu wa afya.
Wengine walioshiriki maadhimisho hayo ni Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Kibaha Mjini Latifa Semwaza, Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Kibaha Vijijini Nyongo Ramadhani,Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Bagamoyo Halima Dossa, mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Kata ya Tangini Jeremiah Komba ,diwani wa Kata ya Tangini Anthony Milao na wanachama kwa ujumla .
Katika maadhimisho hayo timu ya viongozi hao ilifika nyumbani kwa bibi Catherine Januari anayeishi Shina namba 5 Mtaa wa Yombayomba kwa ajili ya kumshika mkono mtoto Catherine Adam Felician ambaye ni mlemavu wa viungo.
Diwani wa Kata ya Tangini Anthony Milao akipanda katika Shule ya Msingi Tangini katika maadhimisho ya miaka 49 ya kuzaliwa kwa CCM.
Mtoto huyo mwenye umri wa miaka 12 amekuwa mlemavu wa miguu,mikono na shingo ambapo hadi hivi sasa hawezi kutembea,hawezi kukaa,hawezi kuongea,na kwamba kila kitu anafanya kwa usaidizi wa bibi yake Catherine Januari .
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Kibaha Mjini Yahaya Mtonda amesema aligundua mateso anayopitia mtoto huyo kipindi cha mbio za bendera zilizokuwa zinafanywa na vijana wa UVCCM Kibaha Mjini ambapo baada ya kupita nyumbani anapoishi mtoto na bibi huyo aliahidi kufanya jambo la kumsaidia.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Kibaha Mjini Yahaya Mtonda akipanda mti katika Shule ya Msingi Tangini ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 49 ya kuzaliwa kwa CCM .
Mtonda amesema kupitia maadhimisho ya miaka 49 ya kuzaliwa kwa CCM ameona ni vyema wakatumia siku hiyo kwa ajili ya kusaidia kile alichoahidi huku akisema bado anafanya mpango kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha mtoto huyo anapata bima ya afya ili iweze kumsaidia kupata matibabu kwa urahisi.
Mtonda ametoa kiasi cha Sh.100,000 kwa ajili ya kumsaidia mtoto huyo fedha ambayo ilikabidhiwa na Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Pwani Yusuf Masombora kwa bibi wa mtoto Catherine Januari ambapo hatahivyo ameahidi kuendelea kushirikiana na wadau wengine katika kuhakikisha mtoto Catherine Felician anapata huduma muhimu.
Ametumia nafasi hiyo kuwaomba wadau mbalimbali kujitokeza kumsaidia mtoto huyo kwa kiwango chochote wanachoweza ili kusudi mtoto huyo aweze kuishi kwa furaha kama ambavyo watoto wengine wanaishi.
Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Kibaha Mjini Latifa Semwaza akipanda mti Shule ya Msingi Tangini ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 49 ya kuzaliwa kwa CCM.
Mbali na kumsaidia mtoto huyo lakini pia viongozi hao walipita nyumbani kwa Mzee Burhan Lehani ambaye ni mlemavu wa miguu kwa kumshika mkono na kumpatia fedha kiasi cha Sh .80,000 ili aweze kujipatia mahitaji muhimu.
Awali Jumuiya ya Wazazi kupitia viongozi hao walipanda miti katika Shule ya Msingi Tangini na kisha kutembelea zahanati ya Tangini na kutoa msaada wa sabuni ,pampasi kwa ajili ya watoto, Wajawazito na wagonjwa mbalimbali.
Akizungumza na wanachama wa CCM pamoja na Jumuiya ya Wazazi wa Kata ya Tangini Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Pwani Yusuf Masombora amewataka viongozi kuhakikisha kila mmoja anawajibika katika eneo lake.
Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Pwani Yusuf Masombora akipanda mti katika Shule ya Msingi Tangini Kata ya Tangini ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 49 ya kuzaliwa kwa CCM hafla iliyofanyika Februari 04/2026.
Amesema wanachotakiwa kufanya kwa sasa ni kutoka ofisini ili washuke kwa wanachama na Wananchi ili waweze kusikiliza kero na changamoto na kisha kuzipatia ufumbuzi wake kwakuwa kila mmoja akiwajibika chama kitasimama imara.
Masombora amesema kuwa wanapoadhimisha miaka 49 ya kuzaliwa kwa CCM malengo yake ni kukipeleka chama karibu na wananchi lakini pia kuonyesha kuwa CCM inachaguliwa kwakuwa kinafanyakazi ya kuleta maendeleo bila ubaguzi.
Amesema viongozi wa Wilaya wanatakiwa kushuka kwa viongozi wa Kata na viongozi wa Kata wanatakiwa kushuka kwa viongozi wa matawi kwahiyo wanatakiwa kuhakikisha wanatenga siku angalau mbili kwa wiki kwa ajili ya kuwasikiliza changamoto za Wananchi.
Aidha, Masombora alisisitiza kulinda amani kwa nguvu zote kwakuwa ikipotea Tanzania haiwezi kukalika na watu watakosa sehemu ya kukimbilia.
Amesema Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama wamefanyakazi kubwa ya kulinda amani na kwamba kila mmoja lazima ajitoe kuungana na Rais na hata vyombo vya dola kuhakikisha amani inazidi kuimarika nchini.







Post a Comment