HEADER AD

HEADER AD

DIWANI MILAO AFANYA ZIARA MATAWI YA CCM , AWASHUKURU WANACCM KUKIPANBANIA CHAMA KUHAKIKISHA KINASHINDA

>> Awaomba kuondoa tofauti zilizojitokeza wakati wa uchaguzi 

Na Gustaphu Haule, Pwani 

DIWANI wa Kata ya Tangini Anthony Milao ameanza ziara ya kuwashukuru wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa jinsi ambavyo walijitoa kuhakikisha CCM inashinda katika uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.

Milao,ameanza ziara hiyo Machi 07/2026 kwa kuwakutanisha wanaCCM wa matawi matatu ikiwemo tawi la Tangini, Tamco na Gunewe ambapo wenyeji wa mkutano huo walikuwa ni wanaCCM wa tawi la Gunewe.

         Diwani wa Kata ya Tangini Anthony Milao akichangia kiasi cha Sh.200,000 kwa Umoja wa wazee wa tawi la Gunewe kwa ajili ya ujenzi banda la kuuzia Kahawa mradi unaomilikiwa na wazee hao.

Akizungumza katika mkutano wake na wanaCCM hao ,Milao amesema kuwa  wanaCCM wa Kata ya Tangini wamefanyakazi kubwa ya kuhakikisha Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan anashinda, Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka pamoja na yeye kupata ushindi wa kuwa diwani wa Kata hiyo.

Amesema ameona ni  vyema akaanza kuwashukuru wanachama hao kwakazi kubwa waliyoifanya na mara baada ya kumaliza ziara ndani ya chama atatoka nje kufanya mikutano ya Wananchi ili kusikiliza kero na kuona namna ya kuzitafutia ufumbuzi.

"Nimekuja kwenu ndugu zangu kuwashukuru wanaCCM wenzangu kwa jinsi ambavyo mlipambana kwa ajili ya chama chetu ,kwanza mlipambana kumpata Rais,mlipambana kumpata Mbunge Silvestry Koka na pia mkapambana kunipata mimi Anthony Milao kuwa diwani wenu kwahiyo nawashukuru sana,"amesema Milao.

Amesema yapo mambo ambayo walikwazana wakati wa uchaguzi lakini kwasasa uchaguzi umepita na kwasasa wanatakiwa kuwa kitu kimoja kwa ajili ya kuwatumikia Wananchi hususani katika kutatua changamoto zinazowakabili.

      Baadhi ya Wanachama wa CCM wakimsikiliza diwani wa Kata ya Tangini Anthony Milao katika mkutano uliofanyika Machi 07/2/2026.

Amesema pamoja na kuwashukuru lakini pia anawatia moyo juu ya yale yaliyotokea wakati wa uchaguzi ambapo amewatoa hofu na kuwataka kwasasa waendelee na utaratibu wa kawaida wa kichama na vikao viendelee kufanyika kwa kushirikiana na mabalozi kwa ajili ya kufanyakazi ya chama na hususani katika kuwatumikia Wananchi.

"Nawasisitiza kuwa kipindi cha hofu kimepita na sasa mabalozi endeleeni kuchapa kazi na hakikisheni bendera zinakuwa juu ili ziweze kupepea na kutoa ishara kuwa Chama Cha Mapinduzi ( CCM)kipo imara kwa ajili ya kuwaletea Wananchi maendeleo,",amesema Milao.

Amewaomba viongozi wa Jumuiya za Chama Cha Mapinduzi ukiwemo Umoja wa Vijana,Umoja wa Wanawake ( UWT) na Jumuiya ya Wazazi washirikiane katika kuimarisha chama kwakuwa jumuiya hizo zikiungana kila kitu kitakuwa sawa.

Amesema Jumuiya ya Wazazi ni ndio Jumuiya ambayo ina mambo mengi ya kufanya ambapo ametaka kuanzia sasa waweke mipango ya kudhibiti hali ya matukio na vitendo viovu katika jamii ikiwemo unyanyasaji wa kijinsia, ubakaji ,ulawiti na mambo mengine yasiyo na msingi katika jamii.

       Diwani wa Kata ya Tangini Anthony Milao akiwa katika kikao cha kuwashukuru wanaCCM kwa kumchagua.

Milao,ameongeza kuwa yeye kama diwani anapenda kuwashukuru kwa kumuamini kwakuwa wamemtoa nafasi moja kwenda nafasi nyingine na kazi yake kubwa ni kuchapakazi kwa faida ya Wananchi wa Tangini na CCM kwa ujumla .

Kuhusu masuala ya maendeleo aliyoyafanya ndani ya miezi mitatu Milao amesema katika kipindi hicho tayari amefanikisha kutatua changamoto ya maji katika Shule ya Msingi Kilimahewa huku akisema anatambua changamoto ya maji ni kubwa kwa wananchi wake.

Amesema , anawaomba wananchi kuendelea kuwa watulivu kwakuwa anajua maji yaliyopo sasa hivi hayana nguvu na sasa wanasubiri mradi mkubwa wa maji unaotekelezwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia na ukishakamilika maji yatapatikana muda wote.

Kuhusu suala la miundombinu ya barabara Milao amesema miongoni mwa changamoto kubwa inayoikabili Kata ya Tangini ni barabara lakini zipo hatua tayari zimeanza kuchukuliwa kwa kukarabati sehemu korofi na hata kujenga karavati kwa maeneo ambayo yalikuwa hayapitiki.

Milao amesema kuwa pamoja na jitihada zake binafsi lakini amepambana kuhakikisha Tangini inapata barabara za lami ambapo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2026/2027 Kata ya Tangini baadhi ya barabara zitaanza kujengwa kwa kiwango cha lami.

Milao,amesema Tangini kuna barabara zenye  urefu wa Kilomita 13 zinazotarajiwa kujengwa kwa kiwango cha lami lakini kwa awamu ya kwanza itajengwa barabara ya Loliondo hadi kuunganisha na barabara ya Pangani pamoja na barabara ya kutoka Loliondo kuelekea Mailimoja Shuleni.

Amesema barabara hizo zinajengwa kwa awamu kutokana na changamoto ya fedha za ulipaji wa fidia kwa Wananchi wanaopaswa kubomolewa nyumba zao kwani wafadhili wa ujenzi wa barabara hizo wao wanatoa fedha za ujenzi wa barabara lakini suala la kulipa fidia Wananchi linahusu Serikali ya Tanzania.

Amesema kufuatia hali hiyo tayari hadi sasa zimepatikana kiasi cha Sh.milioni 580 kwa ajili ya kulipa fidia Wananchi waliopitiwa na barabara zinazoanza kujengwa na kisha baadae zitatolewa fedha nyingine za fidia kulingana na ujenzi wa barabara husika.

Kwa upande wake mwenyekiti mstaafu wa Serikali ya Mtaa wa Tangini Pirmini Gama amempongeza diwani huyo kwakazi nzuri aliyoanza kuonyesha huku akisema wapo tayari kushirikiana nae kwakuwa wameona diwani huyo amekuwa na malengo mazuri ya kuijenga Kata ya Tangini.

Nae diwani mstaafu wa Kata ya Mailimoja Hassan Lugano ambaye kwasasa ni mwenyekiti wa umoja wa wazee Kata ya Tangini amempongeza diwani Milao  kwa kazi nzuri hususani katika kuhakikisha anatatua changamoto ya ukosefu wa maji katika Shule ya Msingi Kilimahewa.

Hatahivyo,Louis Philipo Mkazi wa Mtaa wa Tangini amempongeza diwani huyo kwa juhudi zake kwakuwa anaona kazi ya barabara inafanyika na anaimani juhudi za diwani huyo zitazaa matunda.

       Diwani wa Kata ya Tangini iliyopo katika Manispaa ya Kibaha Anthony Milao ( Kulia) akizungumza na mmoja wa Wananchi wa Mtaa wa Gunewe mara baada ya kumalizika kwa kikao maalum kilichoitishwa na diwani huyo Machi 07/2026 kwa ajili ya kuwashukuru wanaCCM kwa kumchagua.


No comments