HEADER AD

HEADER AD

MBUNGE HAWA AKOSHWA NA UTENDAJI KAZI WA DED KIBAHA KATIKA KUSIMAMIA UKUSANYAJI MAPATO

Na Gustaphu Haule, Pwani

MBUNGE wa Viti maalum Hawa Mchafu amepongeza juhudi zilizofanywa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa pamoja na watumishi wa Halmashauri hiyo kwa kuhakikisha wanasimamia vizuri ukusanyaji wa mapato ya ndani na kupelekea Halmashauri hiyo kushika nafasi ya pili ya ukusanyaji wa mapato Kitaifa.

Ametoa kauli hiyo wakati akifunga sherehe za maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani zilizofanyika Machi 06/2026 katika viwanja vya stendi ya zamani Mailimoja vilivyopo katika Manispaa ya Kibaha.

        Mbunge wa viti maalum Hawa Mchafu ( Kulia mwenye Mkoba wa rangi nyeusi) akinunua bidhaa kwa wajasiriamali walishiriki maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika Kibaha Mailimoja.

Mchafu amesema kuwa kazi iliyofanywa na watumishi wa Manispaa hiyo inapaswa kuungwa mkono na kuwatia moyo watumishi hao ili waweze kufanya vizuri zaidi na ikiwezekana kipindi kijacho waweze kushika namba moja.

Amesema kuwa kinachotakiwa kwa sasa ni kuhakikisha wanaanzisha miradi ya maendeleo ambayo itakuwa inachangia ongezeko la mapato hayo na kufanya Kibaha kuwa na maendeleo makubwa zaidi .

Amesema sehemu yoyote yenye mafanikio lazima kuna mchango wa Mwanamke na anaamini kuwa hata mafanikio ya ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri hiyo yana mchango wa watumishi Wanawake.



"Nitumie nafasi hii kumpongeza Mkurugenzi na timu yake kwa kushika nafasi ya pili kwa ukusanyaji wa mapato kati ya Halmashauri 184 zilizopo nchini lakini nimepata faraja zaidi baina ya kuona Halmashauri ya Kibaha Vijijini ndiyo imeshika nafasi ya kwanza kwahiyo niseme Wilaya ya Kibaha tumepiga hatua kubwa kwa ukusanyaji wa mapato nchini,"amesema Mchafu.

Kuhusu maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani Mchafu amesema kuwa lengo la kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani ni kupima utekelezaji wa maazimio ya kikanda na Kimataifa na maadhimisho hayo yanasaidia kutambua haki na umuhimu wa Mwanamke katika jamii.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa amesema kuwa mafanikio ya Halmashauri hiyo kushika nafasi ya pili Kitaifa kwa ukusanyaji mapato yanatokana na mchango wa watumishi Wanawake .

        Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dkt . Rogers Shemwelekwa akizungumza katika maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani.

Shemwelekwa amesema kuwa asilimia 70 ya watumishi wa Halmashauri hiyo ni Wanawake ambao wamekuwa wakijitoa muda wote kwa ajili ya kufanya kazi za Halmashauri huku akisema anawapongeza Wanawake hao na kuwatia moyo katika shughuli zao za kila siku wanapokuwa kazini.

Amesema kuwa wakati anakuja Kibaha alikuta mapato ya Halmashauri hiyo yamefikia Sh.bilioni 7 na baadae yakapanda hadi kufikia Sh. bilioni 13 na sasa yamefikia Sh.bilioni 18 na kusema bado wanaendelea kuweka mipango mizuri zaidi ili kuhakikisha mapato yanapanda zaidi.

       Maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya stendi ya zamani ya Mailimoja katika Manispaa ya Kibaha Mkoa wa Pwani.

Dkt.Shemwelekwa amesema kuwa Kibaha wanatekeleza kwa vitendo maagizo ya Rais Dkt .Samia Suluhu Hassan na moja ya maagizo hayo ni kuwajali Wanawake na ndio maana mwaka huu Manispaa ya Kibaha imeona katika maadhimisho hayo iwasaidie Wanawake katika kutatua changamoto za ardhi kupitia mpango maalum wa Mama Samia Ardhi Kliniki.

Afisa Maendeleo ya Jamii wa Manispaa ya Kibaha Leah Lwanji amesema Halmashauri inaendelea kutekeleza agizo la Serikali la utengaji wa fedha  asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa kila mwaka kwa ajili ya makundi ya Wanawake,Vijana na watu wenye ulemavu.

      Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Leah Lwanji ( wa kwanza kushoto)akimuongoza Mbunge wa viti maalum kukagua mabanda ya Wanawake wajasiriamali walioshiriki maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya stendi ya zamani MailiMoja Kibaha.

Lwanji ,amesema kuwa kwa mwaka 2025/2026 Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha imetenga zaidi ya Sh.bilioni 1.1 na bakaa ya mwaka 2024/2025 jumla ya Sh .bilioni 2.136  na imetoa mikopo yenye thamani  zaidi ya Sh .bilioni 2.160 kwa vikundi 436 na watu binafsi 21 wenye ulemavu.

Hatahivyo, Lwanji amesema kati ya vikundi hivyo, vikundi 275 ni vya Wanawake ambao walipata Sh.bilioni 1.097,350,000 ikiwa ni asilimia 94 ambapo amesema hatahivyo maombi ya mikopo yanaendelea kupokelewa kwa ajili ya utoaji wa mikopo ya robo ya tatu ikiwa ni Januari hadi Machi 2026.

         Sherehe za maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya stendi ya zamani Mailimoja Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha.

        Mbunge wa Viti maalum Hawa Mchafu akiwa katika moja ya Banda la Wanawake wajasiriamali katika maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika Machi 6/2026.



No comments