JIJI LA MWANZA LINAVYOFAA KUWA MWENYEJI WA MICHUANO YA AFCON 2027
>>Waeleza kwanini wanatamani michuano ya soka Barani afrika ifanyike jijini Mwanza
Na Nashon Kennedy, Mwanza
KUFUATIA Tanzania kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa michuano ya kubwa Soka barani Afrika (AFECON- 2027), baadhi ya wadau wa Soka jijini Mwanza wametoa maoni yao juu ya jiji la Mwanza kufikiriwa kuwa mwenyeji wa michuano.
Wametoa maoni yao hivi karibuni jijini Mwanza walipozungumza na DIMA Online , wakieleza kuwepo kwa fursa za kiuchumi na kuimarika kwa miunombinu .ni moja ya sababu ya kuipeleka AFCON jijini Mwanza.
Wanasema sababu hizo zafaa michuano hiyo kufanyika jijini Mwanza huku wengine wakisema kwamba Uwanja wa CCM Kirumba pamoja na uwekezaji katika sekta za hoteli, uboreshaji wa usafiri wa anga na nchi kavu na huduma za jamii ni moja ya mambo yanayostahili kuwepo michuano ya AFCON.
Mdau wa Soka na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda akizungumza wakati wa hafla ya kuipongeza Timu ya Pamba Jiji ya Mwanza kurejea ligi kuu.
Mdau wa Soka, Hamduni Mariseli anasema Tanzania imepata bahati ya kuwa miongoni mwa mataifa matatu yatakayokuwa mwenyeji wa michuano mikubwa ya soka barani Afrika, maarufu kama Africa Cup of Nations (AFCON).
Anasema kufanyika kwa mashindano hayo jijini Mwanza mbali ya kuleta burudani ya soka, yataimarisha huduma za kiuchumi na kuliweka jiji la Mwanza katika ramani ya soka duniani.
“Jiji letu ni kituo kikubwa cha kibiashara kwa nchi za maziwa makuu, AFCON ikifanyika Mwanza inalipa kwa sababu mashabiki watatoka mikoa yote ya kanda ya ziwa na mikoa mingine kuja kushuhudia lakini hata kwa nchi jirani za Kenya, Uganda na Rwanda,” anasema Hamduni.
Mwenyekiti wa Chama cha Soka mkoa wa Mwanza (MZFA), Vedastus Lufano anasema jiji la Mwanza limekaa kimkakati na ni kivutio kwa nchi za maziwa makuu na kwa raslimali watu, fedha na uboreshaji wa miundombinu bila kusahau vivutio lukuki vya utalii, hivyo linastahili kuwa mwenyeki wa michuano hiyo muhimu.
Mwenyekiti wa MZFA Vedastus Rufano akifafanua jambo.
“Kwa rasilimali zake za watu, wingi wa mashabiki wenye uwezo wa kifedha, miundombinu iliyoboreshwa na vivutio vingi vya utalii, tunastahili kuwa wenyeji wa mechi za AFCON.
“Mashabiki huleta msisimko(vibe), mvuto utakaongeza hamasa ya mashindano kama haya ya AFCON. " anasema Vedastus
Anaongeza kusema " Hata Mkuu wetu wa mkoa, Said Mtanda anaamini jiji letu linapaswa kuwa mwenyeji wa mechi za AFCON kwa sababu ina jamii kubwa ya wapenda soka" amesema.
Mdau wa Soka, Bhiko Kotecha, anasema michuano ya AFCON inastahili kufanyika jijini Mwanza kwa sababu Mwanza ni eneo lenye wadau wengi wa soka kutoka mikoa jirani na pia italeta hamasa kubwa ya soka na burudani kwa wananchi na wadau wa michezo.
“Kwa vile muda bado upo wa kufanya mabadiliko, naziomba Mamlaka zinazohusika na Soka, Shirikisho la mpira wa Miguu(TFF) na Serikali wafikirie uwezekano wa kuileta AFCON Mwanza" anasema
Bhiko anasema kuwa endapo michuano hiyo itafanyika jijini Mwanza wageni na wanamichezo watakaofika watatembelea mbuga ya eanyama ya Serengeti na Kisiwa cha Rubondo na hivyo kuhamasisha utalii wa ndani na nchi kupata mapato.
Mchezaji wa zamani wa timu ya Pamba Fumo Felician (1987-1992) na baadaye timu ya Yanga na timu ya Taifa Fumo Felician, anasema endapo michuano ya Afcon itafanyika jijini Mwanza ni dhahiri itainua uchumi wa jiji na taifa kupitia shughuli za kiuchumi.
Anasema jiji la Mwanza pia lina historia kubwa ya soka nchini, akitoa mfano kwamba mwaka 1984 timu ya Pamba wana TP lindanda mwaka 1984 ilijizolea umaarufu na kwamba kufanyika kwa AFCON Mwanza ni dhahiri kutaendeleza historia nyingine ya soka iliyoko jijini Mwanza.
“Serikali ingeona uwezekano wa kulipatia jiji la Mwanza Kituo kwa ajili ya michuano hii muhimu maana jiji litapata manufaa makubwa hata Uwanja wa CCM Kirumba baada ya michuano ungekarabatiwa zaidi,” anasema Felician.
Kuhusu AFCON
AFCON ni mashindano makubwa ya soka barani Afrika. Kwa Tanzania ni fursa adimu, mashindano haya yataibua vipaji vya soka.
Mashindano haya huzileta pamoja timu za taifa kutoka kote barani Afrika na huvutia uwekezaji na utalii.
Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki imekuwa na historia ya kuwa mwenyeji wa mashindano makubwa ya soka.
Kila mara mashindano ya kitaifa au kimataifa yanapofanyika nchini, mashabiki hujitokeza kwa wingi wakiwa na ushabiki(vibe) katika mchezo wa soka.
Aidha imeweza pia kung’ara katika michuano ya kimataifa pale ilipokuwa mwenyeji, ikishinda na kushindwa baadhi ya mechi.
Soka kikanda
Muundo wa soka nchini umeganyika katika kanda tano: Kanda ya Mashariki, Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Kusini, Kanda ya Kati na Kanda ya Ziwa.
Kanda ya Mashariki inajumuisha mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Lindi na Tanga, huku Kanda ya Ziwa ikijumuisha Mwanza, Kagera, Geita, Shinyanga, Mara na Tabora.
Miongoni mwa kanda hizi, Kanda ya Ziwa inatambulika sana kama moja ya maeneo yenye mashabiki wenye shauku kubwa ya soka nchini Tanzania.
Hata hivyo, miji iliyoteuliwa kuwa mwenyeji wa mechi za AFCON ni Dar es Salaam, Zanzibar, Arusha na Dodoma, hii ina maana kuwa Kanda ya Ziwa imeachwa nje.
Fursa adimu
Kanda ya Ziwa ikipata fursa hiyo adimu itafungua mkoa huo na jiji la Mwanza kiuchumi kwa uwekezaji kwa maelfu ya wageni kutoka Bara la Afrika.
Endapo Jiji la Mwanza likikosa fursa hiyo, vyakula maarufu vya samaki wa Ziwa Victoria na mandhari ya kuvutia ya ziwa hilo vitakosa nafasi ya kuuzika na kuwavutia watazamaji wa soka wa kimataifa.
Mashabiki kutoka nchi jirani kama Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Burundi, Kenya na Uganda zote zikiwa karibu na Mwanza pia watakosa nafasi ya kushuhudia AFCON ambapo itakuwa karibu kwenye mashindano hayo na kwa gharama nafuu.
Tanzania imekuwa na ndoto ya kuwa mwenyeji wa mashindano hayo ya kifahari ya AFCON, ambayo kufanyika kwake hapa nchini sio tu burudani ya soka bali pia huchochea shughuli za kiuchumi, huvutia wawekezaji na huhamasisha utalii wa ndani kwenye miji itakayoshiriki.
Moja ya faida kwa jiji la Mwanza kushiriki AFCON ni nafasi yake ya kijiografia. Liko katika ukanda wa maziwa makuu na linaunganisha Tanzania na nchi jirani za CONGO- DRC, Rwanda, Uganda, Kenya na Burundi.
Kwa ukaribu huo, mashabiki wa soka kutoka nchi hizo wanaweza kusafiri kwa urahisi kwa barabara au kwa usafiri wa maji kuvuka Ziwa Victoria kuhudhuria mechi za AFCON.
Inaelezwa kwamba iwapo timu ya taifa ya DRC -CONGO ingepangwa kucheza AFCON katika Uwanja wa CCM Kirumba, maelfu ya mashabiki kutoka mashariki mwa Kongo wangesafiri kwa barabara kuja kushuhudia mchezo huo na kituo cha Mwanza kingeweza kuwa na idadi kubwa ya mashabiki wa soka kuliko vituo vingine.
Jiji pia lina uwanja wa ndege wenye shughuli nyingi za kiuchumi na kwa mujibu wa takwimu za anga, uwanja huo hufanya takribani safari 20 za ndani kwa siku, jambo linaloliweka katika nafasi nzuri ya kupokea mashabiki wa soka kutoka sehemu mbalimbali.
Jiji linapakana pia na mikoa yenye uchumi mkubwa na idadi kubwa ya mashabiki kama Simiyu, Geita, Shinyanga na Mara, na miji ya Kahama na Katoro yenye utajiri wa madini.
Uzoefu wake wa kuwa mwenyeji wa mashindano ya kimataifa kwa miaka ya nyuma unaonyesha kwamba, jiji la Mwanza sio lazima liwe na viwanja vya ndege vya kimataifa.
AFCON nje ya Mwanza
Wakati wa AFCON 2024 iliyofanyika nchini Ivory Coast, miji kadhaa ikiwemo San-Pédro haikuwa na viwanja vya ndege vya kimataifa.
Badala yake, ndege zilizobeba timu na wageni ziliwasili Abidjan kabla ya kuunganisha safari hadi kwenye miji iliyokuwa wenyeji wa AFCON.
Kwa wakati huo, Tanzania tayari ilikuwa na uwezo wa wa kuandaa vituo vya soka vya aina hiyo, na leo miundombinu ya usafiri imeboreshwa zaidi.
Hivyo jiji la Mwanza inastahili kupewa Kituo kwa ajili ya michuano hiyo ya AFCON kwa sababu katika soka, uwezo wa kifedha wa mashabiki huchangia sana kuleta hamasa, mazingira bora na mafanikio ya kiuchumi ya michuano yoyote ile ya soka.
Utalii ni faida nyingine yenye kuvutia. Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ipo chini ya kilomita 100 kutoka Jijini Mwanza, ikimaanisha wageni wangeweza kufika moja ya vivutio maarufu vya wanyamapori duniani kwa takribani saa mbili.
Timu na mashabiki wanaohudhuria mechi za AFCON wangeweza kwa urahisi kuchanganya soka na kujifunza utalii wa ndani kupitia mbuga zetu za Wanyama.
Kutokana na sababu hizo, viongozi wenye dhamana katika michezo bado wana muda wa kufanya maamuzi upya ili kuwezesha jiji la Mwanza kupata kituo kwa ajili ya AFCON.
Kwa takribani miezi saba iliyosalia kabla ya mashindano, ukarabati wa Uwanja wa CCM Kirumba bado unaweza kukarabatiwa na kukamilika kwa wakati.
Kwanini Mwanza?
Wakati wa AFCON 2023 nchini Ivory Coast, mechi zilichezwa katika viwanja sita vilivyoko Abidjan, Bouaké, Korhogo, San-Pédro na Yamoussoukro.
Mdau wa Soka na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda akizungumza wakati wa hafla ya kuipongeza Timu ya Pamba Jiji ya Mwanza kurejea ligi kuu.
Miongoni mwa viwanja hivyo, ni uwanja mkuu wa Abidjan pekee uliokuwa na uwezo wa watazamaji takribani 60,000, huku vingine vikibeba takribani 44,000 au chini ya hapo.
Uwanja wa Laurent Pokou ulioko San-Pédro, kwa mfano, unachukua takribani watazamaji 20,000 lakini uliteuliwa kuwa mwenyeji wa AFCON, ilhali kwa kulinganisha, Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza unaweza kuchukua zaidi ya watazamaji 25,000.
Iwapo San-Pédro ilistahili kuwa mwenyeji wa mechi za AFCON, basikwa nini Jiji la Mwanza lisipewe nafasi hiyo kwa kupatiwa kituo?
Historia ya soka
Kihistoria, Jiji la Mwanza limekuwa mwenyeji wa mechi muhimu za kimataifa hata kabla ya kujengwa kwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Moja ya mechi za kukumbukwa katika Uwanja wa CCM Kirumba ilifanyika mwaka 2007 wakati Taifa Stars ya Tanzania ilipokutana na Senegal katika mchezo uliovutia sana na kuisha kwa sare.
Mechi hiyo iliwashirikisha wachezaji maarufu kimataifa kama El Hadji Diouf na Mamadou Niang na rekodi ya mahudhurio ya Kirumba kutoka mchezo huo haijawahi kuvunjwa.
Mchezo mwingine wa kihistoria ulitokea mwaka 1985 wakati Simba SC iliishinda Al Ahly ya Misri kwa mabao 2–1 katika Uwanja wa Kirumba.
Ushindi huo unabaki kuwa moja ya mafanikio ya klabu ya Tanzania dhidi ya moja ya timu kubwa zaidi barani Afrika na mabao ya Simba yalifungwa na Mtemi Ramadhan na Zamoyoni Mogella.
Soka si mchezo pekee, bali pia ni siasa, uchumi utamaduni na ni kichocheo cha uchumi.
Wadau wanasema hakuna shaka Jiji la Mwanza linastahili kupewa kituo na kuwa mwenyeji wa michuano ya AFCON ili kutoa raha ya burudani ya soka kwa wadau wa soka kwa nchi za maziwa makuu ikiwemo Tanzania.


Post a Comment