HEADER AD

HEADER AD

MWENYEKITI CCM KIBAHA ATAKA MIRADI YA MAENDELEO IKAMILIKE KWA WAKATI

Na Gustaphu Haule, Pwani

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kibaha Mjini Mwajuma Nyamka ametoa maelekezo kwa watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha kuhakikisha wanaisimamia kikamilifu miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Manispaa hiyo ili hiweze kukamilika kwa wakati.

Nyamka ametoa maelekezo hayo katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM Kibaha Mjini uliofanyika Machi 27 /2026 kwa ajili ya Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson Saimon kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ilani katika kipindi cha Julai  hadi Desemba 2025.

Amesema  Halmashauri Kuu ya CCM imempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha nyingi za utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Manispaa ya Kibaha  kwani bila Rais kutoa fedha Kibaha kusingekuwa na miradi ya maendeleo.

Nyamka amesema Halmashauri Kuu ya CCM Kibaha Mjini imeridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo kwakuwa ilifanya ziara ya kuitembelea na imeona namna ambavyo miradi ilivyotekelezwa vizuri japokuwa ipo baadhi ya miradi ambayo bado haijakamilika.

 Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kibaha Mjini  Mwajuma  Nyamka akizungumza na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, wakati wa Kikao cha utekelezaji wa Ilani kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2025 iliyowasilishwa na Mkuu wa Wilaya Kibaha Nickson Siamon Machi  27/03/2026.

Amesema miradi ambayo bado haijakamilika ni lazima watumishi wa Manispaa ya Kibaha chini ya Mkurugenzi wake Dkt. Rogers Shemwelekwa wahakikishe miradi hiyo inakamilika kwa muda uliopangwa na ikiwezekana mkandarasi asimamiwe kufanyakazi usiku na mchana kama ambavyo Wachina wanafanya.

"Sisi Halmashauri Kuu ya CCM Kibaha Mjini tumeridhishwa na utekelezaji wa ilani katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2025 iliyowasilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson Saimon lakini tunatoa maelekezo kuwa miradi ambayo bado kukamilika isimamiwe kikamilifu ili hiweze kukamilika kwa muda uliopangwa,"amesema Nyamka.

Pia Nyamka amesema Halmashauri Kuu imempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa kwa kazi nzuri ya usimamizi wa ukusanyaji wa mapato na kuiwezesha Manispaa hiyo kushika nafasi ya pili Kitaifa.

Amesema wakati mkurugenzi huyo anaingia Kibaha alikuta mapato yanayokusanywa ni Sh.bilioni 7 lakini hadi sasa amefikisha ukusanyaji wa mapato kwa zaidi ya Sh.bilioni 17 huku akiwa na malengo ya ukusanyaji wa mapato hayo hadi kufikia Sh.bilioni 30.

Aidha,mbali na kumpongeza Mkurugenzi wa Manispaa lakini pia amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson Saimon kwa kufanya kazi nzuri ya usimamizi wa miradi ya maendeleo.

Watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha na Wana CCM wakiwa katika kikao cha uwasilishaji wa taarifa ya utekelezaji wa ilani katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2025 kilichofanyika Machi 27/2026.

Amesema Wilaya ya Kibaha imefanya vizuri kwa ukusanyaji wa mapato kwani Katika Halmashauri ya Kibaha Vijijini ndio imekuwa ya kwanza Kitaifa katika ukusanyaji wa mapato ikifuatiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha iliyoshika nafasi ya pili na kwamba kwa ujumla Wilaya ya Kibaha ndiyo Wilaya iliyoongoza kwa mapato.

Amesema wana CCM wamepokea vizuri utekelezaji huo wa ilani na ndio maana hapakuwa na shida katika kupokea kwakuwa walipoletewa utekelezaji huo kitu cha kwanza ilikuwa ni kuhakikisha unawafikia viongozi wote wa Kata ili waweze kupitia.

Mkuu Wilaya ya Kibaha Nickson Saimon amesema  anawashukuru wajumbe wa Halmashauri Kuu kwa kupitisha ilani hiyo kwani kitendo cha kupokea ni mwanzo wa mafanikio mengine ya kimaendeleo katika Manispaa ya Kibaha.

         Mkuu wa Wilaya Kibaha  Nickson  Saimon akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya kuanzia mwezi Julai hadi Desemba 2025 kwa wajumbe wa Halmashauri  Kuu ya CCM kibaha Mjini.

Amesema kuwa ilani hiyo ilianza kujadiliwa katika ngazi ya Kata na maeneo mbalimbali lakini jambo kubwa katika ilani hiyo lilikuwa ni ukusanyaji wa mapato kwani ilikadiriwa kukusanya bilioni 13 lakini hadi kufikia Desemba Manispaa ilikuwa tayari imekusanga Sh.bilioni 17 ambapo ukusanyaji huo imesaidia Manispaa kushika nafasi ya pili Kitaifa.

Amesema ukiangalia Manispaa ya Kibaha imekuwa ikienda vizuri kwani wakati ameingia Kibaha alikuta mapato yanayokusanywa ni Sh.bilioni  5 lakini kwasasa mapato hayo yamefika Sh.bilioni  17 .

Saimon  amewapongeza watumishi wa Manispaa ya Kibaha kwa kazi nzuri na amewaomba kuhakikisha wanaendelea kufanyakazi zao kwa mujibu wa Sheria na utaratibu huku akisema kinachotakiwa ni kuwekeza nguvu katika usimamizi wa miradi ya maendeleo.

Amesema anatambua kuwepo kwa hoja nyingi katika eneo la barabara huku akisema Manispaa ya Kibaha ina barabara zenye ukubwa wa Kilomita 93 na katika kukabiliana na changamoto hiyo tayari Manispaa imetenga kiasi cha Tsh.milioni 50 .

      Watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha wakiwa katika kikao cha uwasilishaji wa taarifa ya utekelezaji wa ilani katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2025 kilichofanyika Machi 27/2026.

Amesema fedha hizo zitapelekwa kila Kata kwa ajili ya kukarabati barabara zake na mpango huo utaanza utekelezaji wake fedha  katika bajeti ya mwaka 2026/2027.

Kuhusu changamoto ya migogoro ya ardhi  Saimon amesema changamoto hiyo imejitokeza  kila Kata lakini tayari Manispaa imeweka mpango wa kuhakikisha maafisa ardhi wanapita kila Kata kwa ajili ya kumaliza migogoro hiyo.

Hata hivyo,Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Mawazo Nicas amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Kibaha kwa kazi kubwa aliyoifanya na wao kama madiwani wapo tayari kufuata maelekezo ya chama lakini watafanyakazi bila kumuangalia mtu usoni .



No comments