UPELELEZI KESI YA MAUAJI YA RHODA JONATHAN BADO UNAENDELEA
>> Kesi itatajwa Aprili, 13,2026
>> Wakili anayefuatilia mwenendo wa kesi asema upelelezi unafanyika kwa weledi ili haki ipatikane
Na Mwandishi Wetu, Musoma
KESI ya mauaji ya Rhoda Jonathani, inayowakabili washtakiwa watatu Mwita Maginga( 47) mkazi wa Tarime, Marco Maginga (45) ambaye ni mwalimu wa shule ya Msingi jijini Mbeya na Simon Ruhinda (55) ambaye ni muhudumu wa ofisi katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti mkoani Mara itatajwa tena Aprili, 13, 2026.
Hakimu mkazi mkuu wa mahakama ya Hakimu mkazi Musoma, Eugenia Rujwahuka, akizungumza mahakamani hapo Machi, 31, 2026 amesema kesi hiyo iliyokuja kwa ajili ya kutajwa upelelezi wake bado unaendelea .
" Shauri bado linapelelezwa ,upelelezi wake bado haujakamilika hivyo kesi hii itatajwa tena Aprili,13 " amesema Hakimu Eugenia.
Kwa upande wa Jamhuri mawakili ni Joyce Matimbwi akisaidiana na Matha Mbosori ambapo wakili Joyce ameiomba mahakama hiyo kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kesi hiyo kutajwa kwakuwa upelelezi bado haujakamilika.
" Washtakiwa watatu wote wapo, shauri limekuja kwa ajili ya kutajwa . Hali ya upelelezi bado haijakamilika. Tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa " amesema Wakili Joyce.
Washtakiwa wanakabiliwa na kesi ya mauaji ya Rhoda Jonathani aliyekuwa mkazi wa Kitongoji cha Burunga , Kata ya Uwanja wa Ndege wilayani Serengeti, mkoani humo.
Washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo siku ya alhamisi, tarehe ,23, Oktoba, 2025 majira ya kati ya saa moja na saa mbili usiku nyumbani kwa marehemu.
Askari wa Jeshi la Polisi mkoani Mara wakiwapeleka washtakiwa kesi ya mauaji ya Rhoda Jonathani aliyeuawa baada ya kuvamiwa usiku nyumbani kwake Oktoba, 23, 2025 wilayani Serengeti.
Kwa mara ya kwanza washtakiwa wa kwanza na wa pili walifikishwa katika mahakama hiyo Desemba 12, 2025 na kufunguliwa shauri lenye namba 23/12/2025 kabla ya mtuhumiwa wa tatu kuunganishwa na wenzake Februari 3,2026.
Washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo kinyume cha sheria za kanuni ya adhabu kifungu cha 196 na 197 ambapo wote wamerudishwa rumande kutokana na kesi hiyo kutokuwa na dhamana sambamba na mahakama hiyo ya hakimu mkazi kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Wakati huo huo , Wakili Linus Amri anayefuatilia mwenendo wa kesi ya mauaji ya Rhoda , amesema kuwa kesi za mauaji zina mlolongo mrefu hivyo si kwamba upelelezi umechelewa bali upelelezi unafanyika kwa kina ili haki ipatikane.
" Bado upelelezi unaendelea kwa mujibu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwasababu kuna vitu vingi ambavyo vinatakiwa vikamilishwe kwenye upelelezi . Awali watuhumiwa walikuwa wawili sasa ni watatu kwahiyo tunaona upelelezi bado unaendelea .
" Kesi ya mauaji ni kesi kubwa sana na ni kesi iliyogusa hisia za jamii kutokana na mauaji yale ya kikatili hivyo sio kesi nyepesi. Kesi inapelelezwa kwa weledi ili haki ipatikane. Kesi ya mauaji inahusisha vitu vingi .
Rhoda enzi ya uhai wake alikuwa ni mke wa Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA), mkoani Kagera, Mhandisi Wilson Charles .



Post a Comment