RC PWANI AWATAKA WATENDAJI TAASISI ZA BARABARA KUTENGENEZA BARABARA KWA KUZINGATIA MAHITAJI YA JAMII NA UCHUMI
Na Gustaphu Haule,Pwani
MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge,amewataka watendaji wanaosimamia taasisi za barabara ndani ya mkoa huo kuhakikisha wanatengeneza barabara kwa kuzingatia tija na mahitaji ya Jamii na kiuchumi.
Ametoa kauli Machi, 04/2026 wakati akifungua kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Pwani kilichowashirikisha wajumbe mbalimbali pamoja na watendaji kutoka Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini ( TARURA) pamoja na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Pwani.
Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akizungumza wakati akifungua kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Pwani kilichofanyika Machi 04/2026 Kibaha.Kunenge amesema kuwa kama wanataka kutengeneza barabara ni vyema wakaangalia mahitaji ya sehemu husika na mahitaji ya Mkoa pamoja na kufuata vigezo ambayo vinaweza kuleta tija katika utengenezaji wa barabara hizo.
Amesema kinachotakiwa ni kuangalia namna ya kuufungua Mkoa kiuchumi na huduma za kijamii na kwamba wanapotoa mapendekezo ya barabara waangalie kama kunakuwa na tija katika barabara husika ili kuweza kumsaidia Rais katika kufikia malengo yake.
Kunenge ameongeza kuwa mkoa wa Pwani ni mkoa unaoongoza kwa viwanda kwahiyo lazima kuhakikisha miundombinu ya barabara inakuwa mizuri na yenye kupitika muda wote ili kuwasaidia wawekezaji kusafirisha bidhaa zao kwa urahisi zaidi.
Wajumbe wa Bodi ya Barabara Mkoa wa Pwani katika kikao kilichofanyika Machi 04/2026.Amesema mkoa wa Pwani hadi sasa unajumla ya viwanda 1,688 na katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kumejengwa viwanda 301 ambapo kati ya hivyo viwanda vikubwa na vya kati ni 235.
Amesema haiwezekani kuwe na uwekezaji mkubwa kiasi hicho halafu miundombinu ya barabara ikiwa mibovu jambo ambalo haliwezi kukubalika ambapo amewaomba watendaji wa taasisi hizo mbili kuongeza juhudi katika ujenzi wa barabara.
"Naamini meneja wa TARURA mkoa wa Pwani Ibrahim Kibassa na Meneja wa TANROADS mkoa wa Pwani Mhandisi Baraka Mwambage watafanyakazi vizuri ili kuendana na matarajio ya Rais Samia na mimi niwaombe tutengeneze barabara zetu kwa tija ," amesema Kunenge
Amesema anamshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya kwa mkoa na Taifa na Mkoa wa Pwani amehupa kipaumbele kikubwa kutokana na uwekezaji mkubwa wa viwanda kwahiyo lazima kazi ifanyike sawasawa na matarajio yake.
Waziri wa ujenzi Abdallah Ulega amesema kuwa vipaumbele vya ujenzi wa barabara vya kila Wilaya vimechukuliwa lakini hoja kubwa ni kuunganisha Mkoa wa Pwani ili kufungua fursa za kiuchumi na kijamii.
Waziri wa ujenzi Abdallah Ulega akizungumza katika kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Pwani kilichofanyika Machi 04/2026 .Ulega amesema anatambua ipo barabara ya kutoka Kibaha hadi Mapinga inayounganisha Bagamoyo na Dar es Salaam lakini pia ipo barabara ya kutoka Bagamoyo kwenda Mlandizi,Makofia hadi Mzenga na barabara ya Kibaha hadi Kiluvya pamoja na barabara zingine muhimu .
Amesema atahakikisha barabara hizo anaziwekea fedha na zipate wakandarasi ili zianze kujengwa huku akisema pia atatoa kipaumbele kwa miradi mikubwa ya kimkakati yenye sura ya Kitaifa ukiwemo ujenzi wa barabara ya Kibaha ambayo kwa hatua ya awali itajengwa Kilomita 3.6 ambapo kukamilika kwake kutatoa sura nzuri na muonekano uliobora kwa Manispaa ya Kibaha.
Hata hivyo, Mbunge wa viti maalum Hawa Mchafu amesema barabara ya Kongowe - Soga inayoelekea katika kituo cha reli ya mwendokasi( SGR) imekuwa ni kero na changamoto kubwa kwa wananchi wanaotumia barabara hiyo hasa katika kipindi cha mvua.
Mbunge wa viti maalum Hawa Mchafu akizungumza katika kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Pwani kilichofanyika Machi 04/2026.Mchafu ameiomba Tanroads kuichukua barabara hiyo kutoka mikononi mwa Tarura ili waweze kuifanyiakazi kwa wakati kwakuwa ni moja ya barabara ya kimkakati kama ambavyo wameichukua barabara ya Mlandizi hadi katika kituo cha reli ya mwendokasi SGR cha Ruvu stesheni.





Post a Comment