HEADER AD

HEADER AD

HALMASHAURI YA TARIME VIJIJINI YAADHIMISHA SIKU YA MALARIA , WATU 2059 WAKUTWA NA MAAMBUKIZI

                                      

>>Ni waliopimwa Mtana,Nkerege,Gibaso, Itandura,Nyarwana,Murito,Genkuru

>>DC Tarime ahimiza wananchi kutumia vyandarua

 

Na Mwandishi Wetu, Tarime

WANANCHI wapatao 5330, katika halamshauri ya wilaya ya Tarime, kati yao wanawake 3014 na wanaume 2316 wamejitokeza kupima ugonjwa wa Malaria huku watu 2059 wakikutwa na ugonjwa wa Malaria na kupatiwa dawa,Wanawake wakiwa ni 1188 na Wanaume ni 871.

Mkuu wa wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele amewahimiza wananchi kutumia vyandarua ili kujikinga na ugonjwa wa Malaria huku akisema kwamaba waathirika wakubwa wa Maralia ni wajawazito na watoto.

Mkuu wa wilaya ya Tarime Meja Edward Gowele akizungumza na                                                       wananchi wakati wa maadhimisho kuelekea kilele cha siku ya Malaria yaliyofanyika Aprili,24,2026 katika kijiji cha Murito Nyamongo .

DC Gowele ameyasema hayo Aprili, 24,2026 wakati wa maadhimisho ya kuelekea siku ya Malaria Duniani yaliyoadhimishwa na halmashauri ya wilaya ya Tarime katika viwanja vya shule ya msingi Nyabusara kijiji cha Murito, Kata ya Kemambo-Nyamongo. Amesema wananchi wote wanawajibu  kuhakikisha wanatumia vyandarua na kwamba mapambano dhidi ya Malaria inawezekana

Kaimu katibu Tawala wilaya ya Tarime, Matha Omahe ameipongeza halamshauri hiyo kupitia idara ya afya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, wananchi kuadhimisha siku ya Malaria huku akisisitiza jamii kuendelea kujitokeza kupima Maralia.

Mwenyekiti wa Kamti ya afya, elimu na maji ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Nyanungu Tiboche Richard amesisitiza wananchi kutunza mazingira katika hali ya usafi na kutumia dawa za kuua mazalia ya mbu.

     Mwenyekiti wa Kamti ya afya, elimu , maji ambaye pia ni Diwani wa                                                             Kata ya Nyanungu Tiboche Richard akizungumza na wananchi                                                                     katika maadhimisho kuelekea kilele cha siku ya Malaria yaliyofanyika                                                        Aprili,24,2026 katika kijiji cha Murito Nyamongo .

Mratibu wa Malaria katika Halmashauri hiyo, Zephania Sugwa akieleza hali ya Maralia katika halmashauri ya wilaya ya Tarime amesema halmashauri hiyo ni miongoni mwa Halmashauri tano zenye kiwango cha juu cha Malaria ndani ya mkoa wa Mara.

Zephania amesema Kiwango cha maambukizi ya ugonjwa wa Malaria (Malaria positivity rate) kwa ngazi ya Halmashauri kimefikia asilimia 30.7% kwa mwaka 2025 kilinganishwa na mwaka 2024 ambapo kiwango cha maambukizi kilikuwa asilimia 35.8%.

        Mratibu wa Malaria Halmashauri ya wilaya ya Tarime, Zephania                                                                    Sugwa akisoma taarifa wakati wa maadhimisho kuelekea kilele cha siku ya                                        Malaria yaliyofanyika Aprili,24,2026 katika kijiji cha Murito Nyamongo .

“. Kiwango cha maambukizi kinatofautiana kwa kata ambapo kata ya Bumera iliongoza kwa kuwa na kiwango cha juu cha maambukizi kwa asiliia 73.5% kwa mwaka 2025.

“ Hali ya Malaria kwa Halmahauri (Malaria prevalence rate) kwa mwaka 2025 ilifikia asilimia 29.4% ukilinganisha na mwaka 2024 ambapo ilikuwa asilimia 34.2 %” amesema Zephania.

Shughuli zilizofanyika wiki ya Malaria

Mratibu huyo wa Malaria amesema katika wiki ya kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku Malaria Duniani wamefanya zoezi la upimaji na matibabu ya Malaria kwa Vijiji saba (7), Gibaso, Murito, Genkuru, Nyakunguru, Nyarwana, Nkerege na Mtana.

“ Idadi ya wananchi waliojitokeza kupata huduma ya vipimo na matibabu katika Zahanati ya Mtana ni 446 kati yao wanawake ni 249 na wanaume ni 197. Waliokutwa na maambukizi ya Malaria na kupewa dawa ni jumla ni 132 kati yao wanawake ni 70 na wanaume ni 62.

“ Wananchi waliojitokeza kupata huduma ya vipimo na matibabu katika Zahanati ya Nkerege ni 590 kati yao wanawake ni 330 wanaume 260. Waliokutwa na maambukizi ya Malaria na kupewa dawa ni jumla ni 270 kati yao wanawake ni 154 wanaume ni 116.

“Wananchi waliojitokeza kupata huduma ya vipimo na matibabu katika Zahanati ya Gibaso ni 841 kati yao wanawake ni 551 wanaume 290. Waliokutwa na maambukizi ya Malaria na kupewa dawa ni jumla ni 384 kati yao wanawake ni 262 wanaume ni 122.

“Wananchi waliojitokeza kupata huduma ya vipimo na matibabu katika Kituo cha afya Genkuru ni 550 kati yao wanawake ni 278 wanaume 272 Waliokutwa na maambukizi ya Malaria na kupewa dawa ni jumla ni 103 kati yao wanawake ni 42 wanaume ni 61” amesema Zephania .

Amesema wananchi waliojitokeza kupata huduma ya vipimo na matibabu katika Zahanati ya Itandura ni 689 kati yao wanawake ni 406 wanaume 283 Waliokutwa na maambukizi ya Malaria na kupewa dawa ni jumla ni 305 kati yao wanawake ni 191 wanaume ni 114.

                          Wananchi kijiji cha Murito, kata ya Kemambo wakiwa kwenye                                                                     maadhimisho kuelekea kilele cha siku ya Malaria yaliyofanyika                        Aprili,24,2026 katika kijiji cha Murito Nyamongo .

“ Wananchi waliojitokeza kupata huduma ya vipimo na matibabu katika Zahanati ya Murito ni 874 kati yao wanawake ni 508 wanaume 366 Waliokutwa na maambukizi ya Malaria na kupewa dawa ni jumla ni 431 kati yao wanawake ni 252 wanaume ni 179.

Waliojitokeza kupima katika kituo cha afya Nyarwana ni 574 kati yao wanawake ni 295 wanaume 279,waliokutwa na maambukizi ya Malaria na kupewa dawa ni jumla ni 231 kati yao wanawake ni 121 wanaume ni 110 .

Ameongeza kuwa waliojitokeza kupima wakati wa maadhimisho yaliyofanyika shule ya msingi Nyabusara ni 766 kati yao wanawake ni 397 wanaume 369,waliokutwa na maambukizi ya Malaria na kupewa dawa ni jumla ni 203 kati yao wanawake ni 96 wanaume ni 107.

“ Leo tunapoadhimisha siku ya Malaria Duniani huduma za vipimo vya Malaria na matibabu zinatolewa, huduma za uchunguzi wa hali ya lishe na matibabu zinatolewa na zoezi la uchangiaji damu” amesema Zephania.

Mratibu huyo wa Malaria amesema kwamba siku ya Malaria duniani ilianzishwa na shirika la afya duniani,(WHO) mwaka 2007 ikiwa na lengo la kuongeza uelewa wa jamii juu ya ugonjwa wa Malaria, kuweka jitihada za pamoja juu ya mapambano dhidi ya Malaria na kuongeza uwekezaji na uwajibikaji wa kisiasa katika mapambano dhidi ya Malaria na kwamba Kaulimbiu ya mwaka huu inasema ‘TUMEDHAMIRIA KUTOKOMEZA MALARIA WAKATI NI SASA, TUNAWEZA’

Afua zinazotumika kupambana na Malaria

Mratibu huyo wa Malaria amesema kwamba Katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime huduma za vipimo na matibabu ya ugonjwa wa Malaria hutolewa bure katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya kwa kufuata miongoza ya Wizara ya afya.

Ameongeza kuwa vyandarua vyenye viuatilifu vya muda mrefu (LLIN), unyunyiziaji wa viuadudu (Biolarviciding), unyunyiziaji wa viuatilifu vya ukoko (IRS) na dawa kinga dhidi ya Malaria kwa wajawazito(SP)ndizo afua zinazotumika kudhibiti Malaria.

“ Kwa mwaka 2025 jumla ya vyandarua 17886 vilitolewa kwa akina mama wajawazito na vyandarua 11,554 Vilitolewa kwa watoto chini ya miaka mitano. Jumla ya wajawazito 51,696 walipata dawa kinga dhidi ya Malaria aina ya SP na jumla ya nyumba 16,180 zilizopo kwenye kaya 4548 katika kijiji cha Nkerege zilinyunyiziwa viuatilifu vya ukoko (IRS).

Viuadudu na matumizi yake

Zephania amesema Halmashauri ya wilaya ya Tarime ilipokea kiasi cha lita 3655 za viuadudu aina ya BACTIVEC (Bti) kutoka katika kiwanda cha kibaha kwa kushirikiana na Wizara ya afya na kwamba lita 2705.9 zimetumika kwenye mazalia 3361 yenye ukubwa wa mita za mraba 541164 yaliyopo katika kata za Nyamwaga, Matongo, Kiore, Kibasuka, Nyarukoba, Kwihancha, Kemambo, Gorong’a, Manga na Komaswa tangu kupokelewa Desemba,2025.

Tathimini ya ufanisi wa afua ya unyunyiziaji viuadudu

Mratibu wa Malaria amesema Mazalia 3361 yenye mita za mraba 541164 yalinyunyiziwa viuadudu kwa kipindi cha Januari –Desemba , 2025. Kabla ya unyunyiziaji (Baseline) viluilui aina ya Anopheles na Culex hatua ya awali kwa mazalia yote vilikuwa 93706 na hatua za mwisho vilikuwa 84564.

“ Wiki moja baada ya unyunyiziaji kufanyika viluilui vya hatua ya awali vya jamii ya Anopheles na Culex vilipungua kwa asilimia 91.3 na hatua ya mwisho vilipungua kwa asilimia 94.7. wiki ya nne baada ya unyunyiziaji viluilui vya hatua ya awali vilipungua kwa asilimia 99.7 na hatua ya mwishi vilipungua kwa asilimia 99.9.

“Matokeo ya ufanisi wa unyunyiziaji wa viuadudu kwenye kata zote kumi zilizonyunyiziwa kulipelekea kushuka kwa kiwango cha maambukizi kutoka asiliia 28.9% hadi kufikia asilimia 14.5% baada ya unyunyiziaji kwa kipindi cha siku 28.” Amesema Zephania.

Akizungumzia shughuli zilizofanyika katika wiki ya maadhimisho ya ugonjwa wa Maralia Mratibu wa Malaria amesema idara ya afya imeweza kufanya zoezi la upimaji na matibabu ya Malaria kwa Vijiji saba (7) ambavyo ni Gibaso, Murito, Genkuru, Nyakunguru, Nyarwana, Nkerege na Mtana.

Changamoto

Mratibu wa Malaria amezitaja changamoto katika kukabiliana na ugonjwa wa Malaria kuwa ni uhaba wa bajeti kwa ajili ya kutekeleza zoezi la unyunyiziaji vijiji vyote 88 vya Halmashauri, Ukosefu wa vifaa vya kielekroniki kama vile kompyuta, uhaba wa wadau wa Malaria, Kukosekana kwa usafiri wa uhakika kwa timu ya tathimini,Uwepo wa msimu mrefu wa mvua.

Mapendekezo

Zephania ametoa mapendekezo kwamba, Udhibiti wa mazalia ya mbu (LSM) uwe wa sekta mtambuka kama vile kilimo,mazingira, ujenzi n.k, Kuimarisha usimamizi wa sheria za mazingira, Kushirikisha wadau mbalimbali kwa ajili ya kuwezesha utekelezaji wa afua ya unyunyiziaji kama vile wachimbaji wakubwa na wakati wa madini waliopo ndani ya halmashauri kuliko ilivyosasa jambo hili kuachiwa mgodi wa Barrick North Mara pekee.

“ Kupatikana vifaa vya kielekroniki kwa ajili ya kukusanya na kuhifadhi taarifa na data za afua za Malaria, Kuwepo kwa usafiri wa uhakika kwa ajili ya timu ya ufuatiliaji na tathimini , kuanzisha tuzo kwa ajili ya washindi wa mapambano dhidi ya Malaria ndani ya Halmashauri (TARIME DISTRICT COUNCIL MALARIA CHAMPION AWARD)”amesema Zephania.

Mganga mkuu Halmashauri ya wilaya ya Tarime, Amin Vasomana amesema kuwa Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo na idara ya afya inatoa shukrani kwa Mgodi wa Barrick North Mara na Kampuni ya RIN kwa kuwa vinara wa kuwezesha Halmashauri kutekeleza Afua za mapambano dhidi ya Malaria.

Mganga mkuu Halmashauri ya wilaya ya Tarime, Amin Vasomana akizungumza wakati wa maadhimisho kuelekea siku ya Malaria yaliyofanyika Aprili,24,2026 katika kijiji cha Murito Nyamongo

“Kama idara tunatambua na kuthamini mchango wao kwani wanatekeleza kwa vitendo kauli ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya “KAZI NA UTU” amesema Amin.

Mratibu wa Huduma afya na matibabu mgodi wa Barrick North Mara, Robert Mazengo amesema amesema mgodi unaendelea kuwa mshirika na serikali na jamii na ushirika huo umekuwa chanya na kwamba kampeni iliyofanyika ya siku saba imekuwa na lengo la kuimarisha afya kwa jamii ambapo Madaktari Bingwa kutoka hospitali ya Rufaa Bugando wamefika na kutoa huduma za vipimo mbalimbali wakiwemo watoto.

Katika maadhimisho hayo wameshiriki watu mbalimbali wakiwemo watendaji kutoka mgodi wa Barrick North Mara, wafanyakazi kampuni ya ujenzi ya RIN, viongozi wa serikali  ya kijiji cha Murito,na Kata ya Kemambo pamoja na wananchi ya kijiji cha Murito.

                                         Mratibu wa Huduma afya na matibabu mgodi wa Barrick North Mara, Robert Mazengo akizungumza na wananchi katika maadhimisho kuelekea siku ya Malaria yaliyofanyika                                            Aprili,24,2026 katika kijiji cha Murito Nyamongo.  
  
                                 
                                                









No comments