SPIKA BARAZA LA WAWAKILISHI ZANZIBAR ATOA MAELEKEZO KIWANDA CHA ROSTAR KUTOA AJIRA KWA WAZAWA
Na Gustaphu Haule, Pwani
SPIKA wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Zubeir Maulid ametoa maelekezo kwa mwekezaji wa kiwanda cha kuunganisha magari cha Rostar Tanzania kilichopo Kata ya Kerege Wilayani Bagamoyo kuhakikisha wanatoa kipaumbele cha ajira kwa wazawa.
Maulid,ametoa kauli hiyo Aprili 23 /2026 wakati akizungumza na viongozi wa Serikali,taasisi za Serikali na binafsi ,wafanyakazi , wananchi walioshiriki katika ufunguzi wa kiwanda hicho.
Spika Maulid ambaye alimwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar Dk.Hussein Mwinyi amesema uwepo wa viwanda nchini Tanzania ni miongoni mwa fursa kwa Watanzania kupata ajira,pamoja na kukuza mapato ya Taifa.
Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Zubeir Maulid wa pili kutoka kulia akikagua kiwanda cha kuunganisha magari aina ya Faw cha Rostar Tanzania kilichopo Kata ya Kerege Wilayani Bagamoyo alipofika kiwandani hapo kwa ajili ya kukizindua Aprili 23/2026.Amesema ufunguzi wa kiwanda hicho ni ishara ya Mapinduzi makubwa ambayo yanakwenda kufungua milango ya uchumi Afrika na mashariki ya Kati ikiwa ni pamoja na kupunguza gharama za kuagiza magari aina ya malori nje ya nchi na kuongeza fedha za kigeni.
Amesema kiwanda hicho kikubwa kinatarajia kuzalisha magari 5000 kwa mwaka na masoko yake yanapatikana nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania,Zambia,Kongo Burundi , Malawi na Madagascar ambapo uzalishaji huo utapunguza kuagiza magari hayo kutoka nje.
Pia amesema Tanzania ni sehemu nzuri ya uwekezaji barani Afrika ambapo ametumia nafasi hiyo kuwakaribisha wawekezaji wengine kutumia fursa hiyo kuja kuwekeza Tanzania.
Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Zubeir Maulid akiwa na viongozi mbalimbali wakitembelea kiwanda cha kuunganisha magari cha Rostar Tanzania kilichopo Kata ya Kerege Wilayani Bagamoyo ikiwa ni sehemu ya uzinduzi wa kiwanda hicho katika hafla iliyofanyika Aprili 23/2026.Aidha Maulid amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na kwamba bado Tanzania inafursa kubwa za uwekezaji bila usumbufu.
Awali akizungumza katika hafla hiyo kwa niaba ya mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Shaibu Ndemanga amesema kiwanda hicho ni miongoni mwa viwanda vilivyojengwa kipindi cha uongozi wa Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Amesema ni kielelezo kizuri na tafsiri sahihi ya jitihada za Serikali ya awamu ya sita katika kuvutia Uwekezaji, kukuza uchumi na kuboresha maisha ya watanzania.
Kadhakika amebainisha kwamba vipo viwanda vikubwa 71 vinavyouza bidhaa zake nje ya Nchi ambapo zaidi ya tani 20,000,000 za bidhaa mbalimbali husafirishwa kwa mwaka.
Kwa mujibu wa Ndemanga viwanda hivyo vimetoa ajira za moja kwa moja 22,289 na zisizo za moja kwa moja zaidi ya 62,000 na pia zipo Kongani na maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya ujenzi wa viwanda 34 yenye ukubwa wa hekta 116,718.39 ikiwa ni moja ya fursa zinazovutia uwekezaji katika Mkoa wa Pwani.
Ndemanga amesema Serikali inaendelea na ujenzi na uimarishaji wa miundombinu ya msingi na saidizi katika Mkoa wa Pwani ikiwemo umeme, mawasiliano, maji, na usafirishaji kwa njia ya barabara na reli ambavyo vyote kwa ujumla wake vimekuwa ni kichocheo na kivutio cha uwekezaji.
Amesema kwa kipindi cha miaka sita Mkoa huo umepokea Sh. Trilioni 1.561 zilizotumika kujenga miundombinu mbalimbali ya barabara hususani katika maeneo ya uwekezaji wa viwanda.
Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Zubeir Maulid( kushoto) akizindua kiwanda cha kuunganisha magari cha Rostar Tanzania kilichopo Kata ya Kerege Wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani na Kulia ni meneja wa kiwanda hicho Bai xing Guo.Msaidizi wa Mkurugenzi wa kiwanda hicho Juddy Liu amesema uwekezaji huo umegharimu dola za Kimarekani Milioni 20 na kwamba wamepanga kuongeza uwekezaji huo hadi kufikia dola milioni 60 .
Amesema kwasasa kitakuwa ni miongoni mwa viwanda vikubwa Afrika Mashariki kwa kuunganisha magari ambapo kiwanda hicho kitakuwa kinaunganisha magari 5,000 kwa mwaka na kitatoa ajira za moja kwa moja 300 na zizizo rasmi zaidi ya 150.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bagamoyo Abubakar Mlawa ambaye alimuwakilisha Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Pwani ameomba wawekezaji kuweka nembo kwenye bidhaa zao ili zitambulishe eneo zinapozalishwa.
Baadhi ya magari yanayotengenezwa na kiwanda cha Rostar Tanzania kilichopo Kata ya Kerege Wilayani ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani."Pwani kumekuwa na viwanda vingi vinavyozalisha bidhaa mbalimbali na sasa ni wakati wa kuhakikisha bidhaa hizo zinawekwa chapa na kuonyesha mahali zinapotengenezwa( Made in Bagamoyo) na hata kuonyesha maeneo mengine ya Mkoa wa Pwani,"amesema Mlawa.
Mlawa ,amesema kuwa anamshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mzuri Wilayani Bagamoyo kwakuwa uwekezaji huo umekuja kufuatia mazingira mazuri ya uwekezaji.
Hatahivyo,Mlawa amesema Wilaya ya Bagamoyo wameridhika na uwekezaji huo kwakuwa umekuwa na manufaa makubwa kwao ikiwemo kuongeza mapato na ajira hususani kwa vijana wa Bagamoyo huku akisema CCM ipo pamoja na Serikali kwa ajili ya kuwahakikishia wawekezaji mazingira mazuri.






Post a Comment