TUME INAYOCHUNGUZA VURUGU KABLA NA BAADA YA UCHAGUZI MKUU 2025 YA SEMA IKO HURU HAIJAINGILIWA
MWENYEKITI wa Tume ya kuchunguza vurugu za uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, Jaji Othman Chande, amesema tume hiyo iko huru na haikuingiliwa na mamlaka yoyote, akikanusha madai kuwa muda wa kazi yake umeongezwa ili kuruhusu kuhaririwa kwa ripoti yake.
Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam leo, Jaji Chande amesema kuwa tume hiyo ina mamlaka kamili ya mwisho juu ya ripoti yake na haitoi nafasi kwa mtu yeyote kuingilia kazi yake.
"Tume inajitegemea kwa kila kitu. Tume yenyewe ndiyo mhariri, na mamlaka iliyotupa jukumu tutakutana nayo wakati wa kukabidhi ripoti ya mwisho, hatuna mtu yoyote katikati, hatuna dalali," alisisitiza.
Kumekuwa na madai kutoka kwa baadhi ya wadau hasa wanaharakati mitandaoni nchini Tanzania wanaoona kwamba kuongezwa kwa muda wa tume hiyo mara mbili kunalenga kutoa nafasi kwa mamlaka fulani 'kuchakachua' yaliyomo kwenye ripoti hiyo.
Hata hivyo, Jaji Chande ameeleza kuwa sababu kuu ya kuongeza muda ni kupanuka kwa wigo wa kazi pamoja na ongezeko la ushahidi unaokusanywa.
"Awali tulipanga kutembelea mikoa sita, lakini baadaye tukapanua na kufikia mikoa 11 na wilaya 22," amesema.
Ameongeza kuwa tume imepokea ushahidi mwingi kutoka kwa wananchi na wadau mbalimbali, pamoja na ushauri wa kitaalamu ambao unahitaji kuchambuliwa kwa kina kabla ya kukamilisha ripoti.
"Tunachambua ushahidi kwa kina ili kuhakikisha ripoti yetu inakuwa na ubora unaotakiwa, na pia itatolewa kwa lugha ya Kiswahili na tafsiri ya Kiingereza," amefafanua.
Chanzo : BBC

Post a Comment