HEADER AD

HEADER AD

WANAPIGANA WENGINE, WENGINE TUNAUMIA


HII ndio historia, ambayo itabakia,

Katika yetu dunia, hata tukishaishia,

Yale tuliyopitia, bila ya kudhamiria,

Wanapigana wengine, wengine tunaumia.


Sababu zao si zetu, Irani wamevamia,

Huko ndiko chanzo chetu, mafuta twajipatia,

Sasa madhara ni yetu, bei zinajipandia,

Wanapigana wengine, wengine tunaumia.


Ingelikuwa sawia, madhara yakabakia,

Vita waloanzishia, ili wabaki walia,

Sasa wengine twalia, wao watuangalia,

Wanapigana wengine, wengine tunaumia.


Hii ni yetu dunia, ni kijiji nakwambia,

Hakuna wa kujisikia, peke atajifanyia,

Kwingine akisikia, huko yaweze bakia,

Wanapigana wengine, wengien tunaumia.


Israeli Marekani, Irani wamevamia,

Nchi muhimu njiani, meli zinakopia,

Mafuta zikisheni, yaweze kutufikia,

Wanapigana wengine, wengine tunaumia.


Sasa njia ya hatari, ngumu sana kupitia,

Meli zinatahadhari, shida isije ingia,

Sasa kwetu ni hatari, mafuta kujipatia,

Wanapigana wengine, wengine tunaumia.


Kweli twategemeana, katika yetu dunia,

Vema tukaelewana, yale tunajifanyia,

Siyo tukabebeshana, madhara haya jamani,

Wanapigana wengine, wengine tunaumia.


Russia na Ukraine, vita ilipoingia,

Ndipo hapo na wengine, ngano tuliijulia,

Alizeti na mengine, ndiko wanazalishia,

Wanapigana wengine, wengine tunaumia.


Mataifa yaelewa, twagemeana dunia,

Hili linapuuziwa, yale wanajifanyia,

Wengi twasababishiwa, kwenye shida kuingia,

Wanapigana wengine, wengine tunaumia.


Masuluhisho mbadala, vema kujitafutia,

Badala mafuta kula, gesi vema kutumia,

Tunanunua kwa gwala, si dola tunatumia,

Wanapigana wengine, wengine tunaumia.


Hii gesi asilia, yaweza tusaidia,

Shari kutupunguzia, mafuta kuagizia,

Vile twaizalishia, hapa kwetu Tanzania,

Wanapigana wengine, wengine tunaumia.


Mpango bora uwepo, hiyo kutusambazia,

Dar es Salaam ikiwepo, na mitaa mingi pia,

Na mikoani iwepo, hiyo itasaidia,

Wanapigana wengine, wengine tunaumia.


Siyo kisiwa dunia, hilo linatuingia,

Kwao wajipambania, na kwetu sasa twalia,

Bei zinavyozidia, za mafuta tunalia,

Wanapigana wengine, wengine tunaumia.


Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments