HEADER AD

HEADER AD

KESI YA MAUAJI YA RHODA JONATHAN YAPIGWA KALENDA HADI JUNI 9


Na Mwandishi Wetu , Musoma

KESI ya mauaji inayowakabili washtakiwa watatu Mwita Maginga( 47) mkazi wa Tarime,  Marco Maginga (45) ambaye ni mwalimu wa shule ya Msingi jijini Mbeya na Simon Ruhinda (55) ambaye ni muhudumu  wa ofisi katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti mkoani Mara yapigwa kalenda hadi Juni, 9,  2026 .

Washtakiwa wanakabiliwa na kesi ya mauaji ya Rhoda Jonathani mkazi wa Kitongoji cha Burunga , Kata ya Uwanja wa Ndege wilayani Serengeti, mkoa wa Mara aliyekuwa mke wa Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA), mkoani Kagera, Mhandisi Wilson Charles aliyeuawa akiwa nyumbani kwake Oktoba, 23,2025 .

      Rhoda Jonathani aliyeuawa 

Mbele ya Hakimu mkazi mkuu wa Mahakama ya Hakimu mkazi Musoma, Eugenia Rujwahuka , Mwanasheria wa Serikali , Joyce Matimbwi amesema upelelezi bado na akaiomba mahakama hiyo kupanga tarehe nyingine ya kutajwa.

Hakimu Rujwahuka ameahirisha kesi hiyo hadi Juni , 9, 2026 itakapotajwa tena. 

Kwa mara ya kwanza mtuhumiwa wa kwanza na wa pili walifikishwa katika  mahakama hiyo Desemba 12, 2025 na kufunguliwa shauri lenye namba 23/12/2025 kabla ya mtuhumiwa wa tatu kuunganishwa na wenzake Februari 3,2026.

Washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo  kinyume cha sheria za kanuni ya adhabu kifungu cha 196 na 197 ambapo wote wamerudishwa rumande kutokana na kesi hiyo kutokuwa na dhamana sambamba na mahakama hiyo ya hakimu mkazi kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

No comments