Home
/
HABARI KITAIFA
/
THRDC, TLS WALAANI KUTESWA KWA JUMBE, BODABODA WALIOFUATILIA GARI LILILOMBEBA WAPONGEZWA
THRDC, TLS WALAANI KUTESWA KWA JUMBE, BODABODA WALIOFUATILIA GARI LILILOMBEBA WAPONGEZWA

>> Watu zaidi ya 300 wametekwa
>> Serikali lawamani
MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), wamelaani vikali tukio la kutekwa na kuteswa kwa David Joseph Mghanja (Jumbe ) ambaye ni msaidizi wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na maendeleo ( CHADEMA ) Taifa,
Tundu Lissu pamoja na matukio yote ya utekaji yanayaoendelea hapa nchini.
Hayo yameelezwa katika barua ya tarehe 22, 5, 2026 iliyosainiwa na
Mratibu wa Kitaifa Mtandao wa
Watetezi wa Haki za Binadamu
Tanzania (THRDC), Wakili Onesmo Olengurumwa pamoja na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi .
Imeelezwa katika barua hiyo kwamba, kwa mujibu wa maelezo ya Jumbe mwenyewe pamoja na taarifa mbalimbali zilizowekwa
hadharani, Jumbe alitekwa usiku wa tarehe 20 , Mei, 2026 majira ya saa nne usiku akiwa anakaribia kufika nyumbani kwake Bunju, Dar es Salaam.
Akiwa ndani ya gari pamoja na
rafiki yake Allan Macha, walivamiwa na watu wasiopungua watano waliokuwa na silaha za moto, ambao walijitambulisha kuwa ni askari polisi na kumchukua ndugu Jumbe kwa nguvu na kutokomea naye kusikojulikana.
Maelezo ya Jumbe yanaonesha kuwa baada ya kutekwa alifungwa pingu, alipigwa na kuteswa kwa ukatili mkubwa hali iliyopelekea kuvuja damu kichwani, usoni na mikononi pamoja na kupata maumivu makali mwili mzima.
Aidha, Jumbe ameeleza kuwa watekaji
hao walikuwa wakibishana iwapo wampeleke katika Kituo cha Polisi Mbweni au wafuate maelekezo ya mkubwa wao aliyekuwa akitaka apelekwe kwake ili akamalizane naye.
Mtandao wa Watetezi wa haki za Binadamu na chama cha wanasheria wamesema kwamba kauli hizo ni nzito, za kutisha, na zinaibua maswali makubwa kuhusu usalama wa
wananchi.
Katika barua hiyo imeelezwa kwamba, kwa muda mrefu kumekuwa na tuhuma za wazi kuhusu uwepo wa mtandao wa utekaji unaosadikika kufadhiliwa na unaofanya kazi kwa karibu na baadhi
vyombo vya usalama na baadhi ya watu wenye mamlaka.
Imeelezwa tuhuma hizo zimekuwa
zikisemwa na watu wengi waliowahi kutekwa na wamekuwa wakitoka hadharani na kutamka wazi wazi bila hatua zozote kuchukuliwa.
Watetezi hao wamesema vitendo vya utekaji havikubaliki katika nchi
inayojinasibu kuongozwa kwa misingi ya Katiba, sheria, haki na utu wa binadamu.
Wakati huohuo , TRHDC na TLS wamewapongeza vijana waendesha pikipiki (bodaboda ) na wananchi waliojitokeza kwa ujasiri mkubwa kufuatilia gari lililombeba Jumbe baada ya kutekwa, hatua iliyochangia kwa kiasi kikubwa kuokoa maisha yake.
Imeelezwa kuwa, kitendo hicho kinaonesha mshikamano wa wananchi dhidi ya vitendo vya utekaji vinavyoendelea kutishia maisha ya Watanzania.
Watetezi hao wa haki za Binadamu na chama cha wanasheria wamewasihi
watanzania kuendelea na mshikamano huo katika kukabiliana na matukio ya utekaji nchi nzima.
" Kwa mujibu wa takwimu zetu, watu zaidi ya 300 wameshatekwa na kupotea katika mazingira kama haya kwa kipindi cha miaka 7 iliyopita yanayohusisha wanasiasa, wanaharakati, waandishi wa habari na makundi mengine ya kijamii yanayokuwa mstari wa mbele kutetea haki za binadamu, utawala bora na demokrasia.
" Takwimu za hivi karibuni zilotolewa na Tume ya Jaji Chande zinaonyesha kuwa jumla ya watu waliotekwa na kupotea ni zaidi ya 800" imeeleza barua hiyo.
" Sisi tunaamini sehemu kubwa ya watu hawa wametekwa na kupotezwa kwa sababu za kisiasa, kwa sababu ya kusimamia misingi ya haki na demokrasia nchini, kinachotusikitisha zaidi ni kuwa hakuna hatua zozote zinazochukuliwa kutokomeza matukio haya" .
THRDC na TLS wamesikitishwa kuwepo matukio ya utekaji, kupotezwa kwa watu, mateso, vitisho na ukandamizaji wa kisiasa na kwamba hayawezi kuwa jambo la kawaida katika taifa
linalofuata misingi ya utawala wa sheria.
Imeelezwa kwamba, Serikali ina wajibu wa kulinda maisha, usalama na uhuru wa kila mwananchi bila kujali itikadi zake za kisiasa.
" Tumekuwa tukitoa mapendekezo mengi lakini hakuna hata moja linalofanyiwa kazi na kupelekea kuongeza imani kwa watu kuwa makundi haya ya utekaji yanapata baraka zote katika nchi hii kufanya haya yanayoendelea kutokea" Barua imeeleza.
Kutokana na tukio hilo wito umetolewa kwamba kuwe na uchunguzi huru katika suala la Jumbe kwa kuwa tayari Jeshi
la Polisi na vyombo vyingne vya dola vinatuhumiwa kuhusika. Kuwe na chombo huru cha kiraia kitakachochunguza swala hilo pamoja na matukio yote ya utekaji
hapa nchini.
" Polisi hawawezi kufanya uchuguzi huru kwa kuwa ni sehemu ya watuhimiwa katika swala hili kwa muda mrefu. Baada ya uchunguzi wahusika wote wawajibishwe.
" Serikali itoe kauli ya wazi na madhubuti kulaani vitendo vya utekaji, mateso na
kupotezwa kwa watu, na ichukue hatua za dhati kurejesha imani ya wananchi juu ya usalama wao" Imeelezwa katika barua.
" Tunatoa wito kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuridhia haraka mkataba wa umoja wa mataifa dhidi ya mateso na vitendo vingine vya kikatili, visivyo vya kibinadamu au vya kudhalilisha hadhi ya Binadamu, pamoja na mkataba wa kimataifa wa kulinda watu wote dhidi ya kupotezwa kwa nguvu, ili kuimarisha ulinzi wa haki za binadamu, uwajibikaji wa vyombo vya dola, na kuzuia vitendo vya utekaji, mateso na kupotezwa kwa watu vinavyoendelea kutikisa taifa letu.
Wananchi wametakiwa kuendelea kuwa wamoja, kutoa taarifa, kusaidiana na kukataa vitendo vya utekaji na ukiukwaji wa haki za binadamu. Wananchi waunde vikundi vya ulinzi shirkishi (polisi jamii) katika kukabiliana na matukio yote ya utekaji.
" Tunasisitiza kuwa haki haiwezi kujengwa juu ya hofu, ukatili na utekaji. Taifa letu linahitaji sheria zitawale, si nguvu wala vitisho. Kimya dhidi ya matukio haya ni kuhalalisha ukatili na kuisaliti Katiba ya nchi yetu" Imeelezwa.
Post a Comment