HEADER AD

HEADER AD

KUFULI

Kufuli nimenunua, iwe kinga mlangoni,
Funguo ya kufungua, ninayo mi mfokoni,
Wezi inawazuia, naeleza si utani,
Kufuli yangu ya shaba ni imara madhubuti.

Watu wanaitamani, kufuli yangu jamani,
Hata mkiitamani,kwangu inaniamini,
Kufuli naithamini, tena kutoka moyoni,
Kufuli yangu ya shaba ni imara madhubuti.

Wengi wanaililia, wataka kuichukua,
Kila mbinu metumia, hata kwa uchawi pia,
Kufuli imekataa, mlangoni kusogea,
Kufuli yangu ya shaba ni imara madhubuti.

Kufuli naisifia, kwa yake nzuri tabia,
Mengi imevumilia, imara imetulia,
Kufuli najivunia, heshima menipatia,
Kufuli yangu ya shaba ni imara madhubuti.

Heshima yanipatia, kufuli yangu hakika,
Nami naifurahia, imenitoa mashaka,
Macho wanaitolea, kwa lazima waitaka,
Kufuli yangu ya shaba ni imara mathubuti.

Ulaya nimeitoa, kwa gharama na rupia,
Ghali nimeinunua, fedha nyingi metumia,
Kuileta tanzania, gharama nimeingia,
Kufuli yangu ya shaba ni imara mathubuti.

Mwishoni nimefikia,  nahitimisha safari,
Mengi nimeelezea, kupitia kwa shairi,
Kufuli najivunia, inayo mengi mazuri,
Kufuli yangu ya shaba ni imara madhubuti.

Mtunzi sir Dody.
Simu, 0671159555
Mudio islamic

No comments