HEADER AD

HEADER AD

THRDC , MAIPAC YAWAHIMIZA WAANDISHI WA HABARI KUANDIKA HABARI ZA UCHUGUZI ZA MAZINGIRA


>>  Wajitosa kuwatetea waandishi wa habari za uchunguzi za mazingira watakaokumbana na vikwazo

>> Wakili Paul Kisabo akumbusha sheria , mikataba ya kimataifa,kanuni zinazotetea mazingira

Na Mwandishi  Wetu , Mwanza

SHIRIKA lisilo la kiserikali la kutetea na kulinda haki za Binadamu nchini Tanzania ( THRDC) kwa kushirikiana na Shirika lisilo la kiserikali nchini Tanzania la msaada wa vyombo vya habari za kijamii za asili na wafugaji ( MAIPAC) yamewahimiza waandishi wa habari nchini kuandika habari za uchunguzi zinazohusu utunzaji wa mazingira .

Mkurugenzi wa mipango na uendeshaji shirika la THRDC , Wakili Halima Sonda amesema kwamba waandishi wa habari wasiogope kuibua na kuandika habari za uchunguzi zinazohusu mazingira kwani haki ya uhai huwezi kuitenganisha na mazingira.

      Mkurugenzi wa mipango na uendeshaji shirika la THRDC , Wakili Halima Sonda akitoa elimu kwa waandishi wa habari za mazingira Kanda ya ziwa.

Wakili Halima ameyasema hayo wakati wa mafunzo ya siku mbili ya uandishi wa habari za uchunguzi za mazingira kutoka mkoa wa Mwanza, Mara, Shinyanga, Kagera, Simiyu na Geita.

Mafunzo hayo yamefanyika Mei, 19 - Mei, 20, 2026 katika ukumbi wa hoteli ya Adden Place , kata ya Pasiansi, wilaya ya Ilemela ,mkoani Mwanza, yaliyofadhiliwa na shirika la umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni ( UNESCO).

      Waandishi wa habari Kanda ya Ziwa wakiwa katika picha ya pamoja na wakufunzi wa masuala ya mazingira kutoka THRDC na MAIPAC .

Wakili huyo amesema kwamba Mazingira ni haki za Binadamu kwani ili mwanadamu aweze kupata haki zake halisi lazima aishi katika mazingira safi na salama.

" Tumetoa mafunzo haya kwa waandishi wa habari kama watetezi wa haki za Binadamu . Tunatamani waandishi wa habari wachuguze , waibue na kuripoti habari za mazingira kwa wingi kwani habari za mazingira hazijaripotiwa kwa upana wake.

" Msiogope kuandika sisi tupo tayali kuwatetea kwasababu haki ya uhai huwezi kuitenganisha na mazingira .  kuanzia sasa wakili wenu ni Paul Kisabo hivyo nendeni mkafanye kazi bila woga palipo na changamoto tuelezeni " amesema Wakili Halima .

Ameongeza kusema shirika hilo linafanya kazi za kulinda watetezi wa haki za Binadamu ikiwemo kutoa msaada wa kisheria na utetezi na uelimishaji .

Mratibu wa dawati la mazingira shirika la THRDC Agness Lukasola amesema mafunzo kwa waandishi wa habari za mazingira ni mkakati wa makusudi kuhakikisha jitihada zinazofanywa na watetezi wa haki za Binadamu, au  waandishi wa habari kwa upande wa mazingira zinaripotiwa kwenye vyombo vya habari .

Mratibu wa dawati la mazingira shirika la THRDC Agness Lukasola.

Amesema nia yao ni jamii na mamlaka mbalimbali wazione habari hizo na ziweze kuleta mafanikio chanya na ya muda mrefu kwani suala la mazingira ni la umma na linahusisha haki za watu na vizazi vijavyo.

Mwenyekiti wa Shirika lisilo la kiserikali nchini Tanzania la msaada wa vyombo vya habari za kijamii za asili na wafugaji ( MAIPAC) , Mussa Juma ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama cha wafanyakazi katika vyombo vya habari (JOWUTA), amesema wameona kuna umuhimu wa kuwajengea uwezo waandishi wa habari waweze kufanya uchunguzi kuhakikisha wananchi wanakuwa salama.

    Mwenyekiti wa Shirika lisilo la kiserikali nchini Tanzania la msaada wa vyombo vya habari za kijamii za asili na wafugaji ( MAIPAC) , Mussa Juma akizungumza na waandishi wa habari Kanda ya Ziwa.

" Tunaamini kuwa mtu akipata madhara kutokana na uharibifu wa mazingira tayali haki yake ya kuishi inakuwa imechukuliwa na mtu mwingine . Tunaamini Kanda ya Ziwa kuna waandishi wa habari wengi.  Tumetoa mafunzo kwa waandishi wa habari 35 .

" Tunaamini watakuwa mabalozi kwa wengine kuendeleza tuliyokubaliana kwenda kuandika habari za uchunguzi za kimazingira katika maeneo yetu.

Mwezeshaji wa mafunzo Edwin Soko ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama cha Waandishi wa habari mkoa wa Mwanza , na Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika – Tanzania, inayojihusisha na kutetea uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa kujieleza, na haki ya kupata taarifa nchini Tanzania amewasisitiza waandishi wa habari kuzingatia maadili ya taaluma ya uandishi wa habari.

           Mwezeshaji wa mafunzo Edwin Soko akiwafunda waandishi wa habari Kanda ya Ziwa .

Mwezeshaji wakili wa Shirika la THRDC, Paul Kisabo amesema kila mtu ana haki ya kuishi katika mazingira salama huku akiwakumbusha waandishi wa habari kujikumbusha kusoma sheria, mikataba ya kimataifa na kanuni mbalimbali zinazohusu usimamizi na ulinzi wa mazingira ili ziwasaidie wanapokuwa wanafanya chunguzi za habari za mazingira.

Amewataka kuibua athari zitokanazo na uharibifu wa mazingira ili hatua ziweze kuchukuliwa ikiwemo kuwafikisha mahakamani wasiowajibika kusimamia sheria, kanuni, katiba ya nchi na mikataba ya kimataifa juu ya uharibifu wa mazingira .

Mwezeshaji wakili wa Shirika la THRDC, Paul Kisabo akiwafunda waandishi wa habari Kanda ya Ziwa.

Waandishi wa habari Kanda ya Ziwa akiwemo Frankus Cleophace kutoka mkoani Mara, wameshukuru kujengewa uwezo wa kuandika habari za uchunguzi za mazingira na kuahidi watayatumia mafunzo hayo vyema kuibua na kuandika habari za uchunguzi.




Mwandishi wa habari Frankus Cleophace akichangia mada wakati wa mafunzo ya uandishi wa habari za mazingira.

       Baadhi ya waandishi wa habari wakiwa kwenye mafunzo ya uandishi wa habari za uchunguzi.









No comments