HEADER AD

HEADER AD

TUCTA YAWATAKA VIONGOZI WA JOWUTA KUSHIRIKIANA NA SERIKALI ILI KUIMARISHA CHAMA

Na Gustaphu Haule, Pwani 

RAIS wa Shirikisho la vyama vya Wafanyakazi Tanzania ( TUCTA) Tumaini Nyamuhokya amewataka viongozi wa Chama Cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) kuhakikisha wanashirikiana na Serikali ili kuweza kukiimarisha chama hicho.

Nyamuhokya amesema miaka ya zamani kulikuwa na chama Cha wafanyakazi Waandishi wa habari Tanzania ( TUJ) lakini chama hicho kilikufa kutokana na kukosa ushirikiano baina ya Serikali na vyama vingine kwahiyo hapendi kuona JOWUTA kinaishia njiani.

       Rais wa Shirikisho la vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) Tumaini Nyamuhokya akifungua kikao kazi kati ya WCF na Jowuta kilichofanyika Mei 25/2026 Jijini Dar es Salaam .

Aidha , Nyamuhokya amesema TUCTA itaendelea kushirikiana na Jowuta katika  kila hatua ili kuhakikisha changamoto za wafanyakazi wa vyombo vya habari zinapata ufumbuzi ikiwemo suala la mikataba na ajira.

Nyamuhokya ametoa kauli hiyo Mei 25/2026 wakati akifungua mafunzo kuhusu mfuko wa fidia kwa wafanyakazi (WCF) yaliyofanyika Sinza Jijini Dar es Salaam chini ya maandalizi ya Jowuta kwa ufadhili wa WCF.

Amesema Jowuta ni chama muhimu kinachowaunganisha Waandishi wa habari nchini kwahiyo lazima chama hicho kizidi kuimarishwa ili kuwasaidia Waandishi wa habari na Taifa kwa ujumla.

    Waandishi wa habari wa Pwani na Dar es Salaam wakiwa katika kikao kazi cha Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kilichofanyika Mei 25/2026 .

Nyamuhokya amewapongeza viongozi wa Jowuta kwa kusimamia chama hicho hadi kuhakikisha kinakuwa mwanachama wa Tucta na kwamba lazima sasa waunganishe nguvu kati yao na Serikali ili kukipa nguvu na uimara wa kusongambele.

Ameupongeza uongozi wa mfuko wa fidia kwa wafanyakazi (WCF) kwa kuwakutanisha pamoja wafanyakazi wa Jowuta na kwamba mfuko huo umekuwa na mfano wa kuigwa kwakuwa ni mfuko wa kwanza kuamua kukutana na wafanyakazi Waandishi wa habari kupitia chama chao.

        Rais wa Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA)Tumaini Nyamuhokya akimpa zawadi mfanyakazi bora wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) Mhasibu Mwandamizi Omary Omary katika kikao kazi kuhusiana  na huduma za mfuko kwa chama cha Wafanyakazi wa vyombo vya habari Tanzania (JOWUTA) Mei 25/2026 Dar es Salaam.

Amesema Tanzania imekuwa na bahati kubwa ya kuwa na mifuko mingi ya Wafanyakazi kama vile WCF, PSSSF, NSSF na mengine lakini WCF imeonyesha mfano mzuri wa kujenga mashirikiano na Jowuta huku akiiomba mifuko mingine kuiga mfano huo.

Amesema mfuko wa WCF umefanya jambo nzuri kutoa   elimu kwa Waandishi wa habari na kwamba ni wajibu wa kila Mwandishi wa habari kuhakikisha anakwenda kutumia chombo chake na kalamu yake kuelimisha jamii kujiunga na mfuko huo.

Ameomba uongozi wa WCF kupitia Kaimu Mkurugenzi wake Laura Kunenge ambaye pia ni Mkuu wa Mahusiano wa WCF kuhakikisha wanaendeleza ushirikiano huo ikiwa pamoja na kuwafikia Waandishi wa habari wengi zaidi waliopo Mikoani.

"WCF ni sehemu ya ukombozi wa wafanyakazi nchini kwakuwa wanatoa mafao ya kuumia na kuugua ukiwa kazini kwahiyo ni vyema Waandishi wa habari wakaelimisha jamii hususani wafanyakazi ili waweze kujiunga na mfuko huo,"amesema Nyamuhokya.

Mwenyekiti wa Chama Cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari nchini (JOWUTA) Mussa Juma ameushukuru Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kwa kukubali kutoa mafunzo kwa Waandishi wa habari wa Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani.

       Mwenyekiti wa Chama Cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari nchini (JOWUTA) Mussa Juma.

Juma ,amesema JOWUTA inawanachama 400 kote nchini na anategemea wataendelea kushirikiana na WCF katika kuhakikisha mafunzo hayo yanaendelea kutolewa Kikanda na hivyo kuwafikia wanachama wote.

Amesema JOWUTA ni wanachama wapya wa Tucta waliojiunga mwaka 2025 na tangu wamejiunga Tucta yapo mabadiliko yameonekana na anaimani Jowuta itaendelea kushirikiana na Tucta katika kutatua migogoro ya wafanyakazi Waandishi wa habari.

Amesema ameishukuru Serikali kwakuwa imekuwa ikitoa ushirikiano mkubwa hadi sasa japo changamoto kubwa ya Waandishi wa habari wengi ni kukosa mikataba na ajira kwani wapo Waandishi wa habari wamefanyakazi miaka zaidi ya 10 lakini hawana ajira.

Nae Mkuu wa Mahusiano wa WCF Laura Kunenge amewaomba Waandishi wa habari kwenda kuwa mabalozi wa mfuko wa fidia kwa wafanyakazi (WCF)juu ya kuelimisha jamii umuhimu wa mfuko huo.

          Mkuu wa Mahusiano wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) Laura Kunenge akizungumza katika kikao kazi cha mafunzo ya Waandishi wa habari kutoka Jowuta kilichofanyika Mei 25/2026 Jijini Dar es Salaam.

Amesema Serikali inalipa fidia kwa wafanyakazi pale wanapoumia na kuugua kazini lakini hatahivyo yapo mafao mbalimbali ambayo mfanyakazi anaweza kufaidikanayo ikiwa pamoja na huduma za matibabu.

"WCF ipo kwa ajili ya wafanyakazi, Watanzania na jamii kwa ujumla kwahiyo niwaombe Waandishi wa habari kuhakikisha taarifa juu ya Mfuko huu zinawafikia waajiri ili waweze kutoa nafasi kwa wafanyakazi wao kujiunga na WCF,"amesema Laura.

Hatahivyo Laura amesema kuwa WCF itaendelea kushirikiana na Jowuta katika kuhakikisha wanatoa mafunzo hayo mara kwa mara ili kuwafikia wanachama wote lakini lengo ni kufungua fursa kwa wafanyakazi kutambua umuhimu wa WCF.

      Waandishi wa habari wakiwa katika kikao kazi cha WCF na Jowuta Mei 25/2026.


No comments