HEADER AD

HEADER AD

DC TARIME AWAOMBA WANANCHI KUJITOKEZA KLINIKI YA KUSIKILIZA MALALAMIKO ILIYOANZISHWA NA MGODI WA NORTH MARA

>> Aitaka kamati ya kusikiliza malalamiko kuwatagazia wananchi siku na muda wa kusikiliza malalamiko

>>Kamati ya utatuzi wa migogoro itanzunguka vijiji vyote 11 vinavyozunguka mgodi wa North Mara

Na Mwandishi Wetu, Tarime

MKUU wa wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele amewaomba wananchi katika vijiji 11 vinavyozunguka mgodi wa North Mara, kujitokeza kwa wingi kutoa malalamiko yao mbele ya kamati ya kusikiliza na kushughulikia malalamiko .

Ameyasema hayo Mei, 26, 2026 wakati akizindua kliniki ya kusikiliza na kushughulikia malalamiko vijiji 11vinavyozunguka mgodi wa Barrick North Mara iliyoundwa na mgodi huo, uzinduzi uliofanyika viunga vya stendi ya Nyamongo.

      Mkuu wa wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele.

Kamati hiyo iliyoundwa ya kushughulikia malalamiko imehusisha wadau mbalimbali kutoka ngazi za serikali za vijiji, kata, wilaya na mkoa , kampuni ya Barrick North Mara na watu wa haki za Binadamu .

Amewaomba wananchi kutumia fursa hiyo muhimu kujitokeza kusema malalamiko yao  yaweze kusikilizwa na kupatiwa majibu.



" Niwaombe wananchi kutumia fursa hii muhimu sana katika hii kliniki iliyojumuisha watu mbalimbali kuweza kupeleka malalamiko ambayo mnayo.

" Ninaamini yapo mambo ambayo yatatolewa ufafanuzi kupitia kliniki hii na wananchi wataelewa . Lakini yapo mambo yatahitaji kufanyika utatuzi wa kina ili kujenga jamii yenye ustawi mzuri na maelewano mazuri " amesema DC Gowele.

Ameiagiza kamati ya kusikiliza malalamiko kuwatangazia wananchi kwa wakati siku na muda wa kuwasili kwenye Kijiji kusikiliza malalamiko .

        Watendaji wa serikali na mgodi wa North Mara wakiwa kwenye mkutano wa kusikiliza malalamiko.

" Niwaombe wale wajumbe wa kamati hii ya kusikiliza malalamiko ambao mnaenda kufanya kazi, kwanza ni lazima muwatangazie wananchi kwasababu natambua mtazunguka vijiji 11.

" Mnapokwenda kwenye mikutano hiyo wananchi wapate taarifa ili kufahamu siku na muda wa kamati hiyo itasikiliza malalamiko ya wananchi ili isitokee mwananchi kusema kwamba hakusikia kama kuna kliniki ya utatuzi wa migogoro kwenye eneo lake" amesema DC Gowele.

Amesema kwamba wananchi wakipata taarifa na kushiriki kutoa malalamiko yao kliniki hiyo itakuwa imewasaidia viongozi wa serikali kuwapunguzia kero na changamoto ambazo wamekuwa wakizipokea kila wakati.

          Wananchi wakiwa kwenye mkutano wa kusikiliza malalamiko.

" Niwaombe sana viongozi wa ngazi za chini kwa maana ya vitongoji,vijiji na kata kwenda kuhamasisha wananchi kushiriki kwenye kliniki" amesema Gowele.

Diwani wa Viti maalum Ferista Range, amewaomba wananchi kuwa huru kutoa malalamiko yao kwamba yatasikilizwa na kutatuliwa hivyo kila mtu ajisikie kuuliza nini mgodi ufanye kwa wananchi.

Mwenyekiti wa kamati ya maendeleo ya jamii vijiji vinavyozunguka mgodi wa North Mara (CDC) ambaye ni Diwani wa kata ya Kemambo, Rashid Bogomba amesema ni vyema wananchi wakaitumia kliniki hiyo kutoa malalamiko yao.

Mwenyekiti wa kamati ya maendeleo ya jamii vijiji vinavyozunguka mgodi wa North Mara (CDC) ambaye ni Diwani wa kata ya Kemambo, Rashid Bogomba


" Hii ni kliniki tuliyoianzisha ni vizuri wananchi tukaitumia kuhakikisha tunapunguza malalamiko na migogoro iliyopo hata ikiwezekana tuimalize.

" Tutazunguka kwenye vijiji vyote 11 , tuitumie hiyo nafasi kuhakikisha tunakutana tunazungumza ili mwenye shida ya mgogoro wa ardhi aje na mchango wake ,ana shida lakini aje na mchango ni kwa namna gani tunaweza kumaliza huu mgogoro " amesema Diwani Bogomba.

Ameongeza kuwa migogoro hiyo ikimalizika kabisa mahusiano kati ya wananchi na mgodi yataimalika shughuli za maendeleo zitafanyika vizuri huku akiwaomba Viongozi wa vijiji kuitumia nafasi hiyo ili kupunguza migogoro ya ardhi kwenye maeneo yao.

Baadhi ya wananchi wameeleza kero zao miongoni mwao Juma Petro mkazi wa Kijiji cha Kewanja ametoa malalamiko yake ya kupigwa risasi na askari Polisi wanaolinda mgodi wakati akiwa anachunga ng'ombe, akiwa na umri wa miaka 12 . Hakulipwa fidia na kwamba mgodi ulimuahidi kumpatia ajira ili imsaidie katika maisha yake lakini hakuweza kumpatia.

        Mwananchi akitoa malalamiko yake ya serikali ya Kijiji cha Nyabichune kutaka kupora ardhi yake.

Mgodi waeleza kuanzishwa Kliniki

Meneja mkuu wa mahusiano mgodi wa Barrick North Mara, Francis Uhadi amesema kliniki hiyo ni jukwaa la pamoja la kusikiliza na kutatua changamoto ambapo serikali na mgodi hukutana na wananchi kusikiliza na kutatua malalamiko, kutoa ufafanuzi na kutafuta suluhu kwa pamoja na uwazi .
    Meneja mkuu wa mahusiano mgodi wa Barrick North Mara, Francis Uhadi akieleza malengo ya kuanzisha kliniki ya kusikiliza malalamiko.

Amesema lengo ni kuhakikisha kama kuna malalamiko yoyote yanayohusu upande wa serikali , mgodi kamati hiyo itaweza kusikiliza na kuyatafutia ufumbuzi.

" Ni utaratibu tuliojiwekea wa kila mwaka tunakuwa na kliniki ya kusikiliza malalamiko kutoka vijiji 11 vinavyozunguka mgodi . Tunaendelea kuimalisha zoezi hili kwa kushirikiana na serikali za vijiji na viongozi mbalimbali ili kuhakikisha wananchi wengi wanapata taarifa na wanajitokeza .

Francis ametoa wito kwa wananchi kutumia jukwaa hilo muhimu kujitokeza na kuwasilisha changamoto zao mbalimbali ili waweze kusikilizwa na kuweza kupatiwa ufumbuzi.

Wananchi wakiwa kwenye mkutano wa kusikiliza malalamiko.

" Mgodi unaendelea kuimalisha mahusiano na wananchi kama kuna malalamiko yoyote basi tuweze kuyasikiliza na kuyatafutia ufumbuzi " amesema Francis.

Amesema mwaka 2018 malalamiko yaliyowasilishwa Barrick yalikuwa 84, 2019 malalamiko 105, 2020 malalamiko 92, mwaka 2021 malalamiko 72, 2022 malalamiko 41, 2023 malalamiko 55, 2024 malalamiko 44 na mwaka 2025 malalamiko yalipungua hadi 16.

" Ofisi ya Kijiji tumeweka daftari la kupokea malalamiko na kuyawasilisha kwetu lakini pia tumeimarisha daftari kwenye ofisi ya DC kwasababu kuna watu wanapeleka malalamiko lakini pia ofisi ya mkuu wa mkoa .

" Tumetengeneza mahusiano ya pamoja kuhakikisha kwamba yanapotokea malalamiko yoyote yanayohusiana na mgodi tunapeana taarifa za haraka" amesema Uhadi.

Kuanzishwa kliniki ya malalamiko.

Francis amesema mgodi umeweka utaratibu wa kushughulikia malalamiko ili kuhakikisha kuwa kila lalamiko/ malalamiko yanashughulikiwa kwa wakati, kwa uwazi na kwa ushirikiano wa pande zote mbili ili kudumisha mahusiano mazuri kati ya mgodi na jamii.

Kutoa fursa kwa kila mtu mwenye lalamiko/malalamiko kusikilizwa kwa heshima , kwa uwazi, bila kujali hali yake ya kiuchumi, jinsi, dini au eneo analotoka.

" Kudumisha mahusiano mazuri kati ya mgodi na jamii kwa kuhakikisha kuwa kila lalamiko linashughulikiwa kwa wakati, kwa uwazi na kwa ushirikiano wa pande zote husika.

" Kuhakikisha kuwa malalamiko yanatumika kama chanzo cha kujifunza ili kuboresha utendaji wa mgodi na kuimalisha mifumo ya mawasiliano kati ya mgodi na jamii" amesema Francis.

Malalamiko yatakavyo shughulikiwa

Mgodi umeweka utaratibu wa kushughulikia malalamiko ambapo uwasilishwaji wa malalamiko; mlalamikaji anatakiwa kuwasilisha lalamiko lake kupitia njia rasmi zilizowekwa, uchunguzi wa chanzo cha lalamiko; Kamati huchunguza chanzo cha lalamiko kwa kushirikiana na mlalamikaji ili kubaini ukweli wa lalamiko husika.

          Wananchi wakiwa kwenye mkutano wa kusikiliza malalamiko.

Ufuatliaji wa lalamiko; Baada ya chanzo kubainika, hatua zinazofaa huchukuliwa ili kupata suluhisho stahili kwa pande zote zinazohusika.

Kutoa mrejesho ; Mlalamikaji hupatiwa mrejesho rasmi kuhusu matokeo ya uchunguzi na hatua zilizochukuliwa. Kukata rufaa ; Endapo mlalamikaji hataridhika na suluhisho lililotolewa awali, ana haki ya kukata rufaa na kusikilizwa kwa mara ya pili. Endapo mlalamikaji hataridhika na hatua mbili za awali anaruhusiwa kuwasilisha lalamiko kwenye mamlaka za serikali.

Njia za mawasiliano

Mgodi huo umetoa njia za mawasiliano katika kuwasilisha malalamiko ambazo ni kupitia viongozi wa Kijiji au kata husika, kupitia afisa uhusiano au Meneja wa uhusiano wa mgodi wa North Mara.

Wananchi wakiwa kwenye mkutano wa kusikiliza malalamiko

Pia kupitia mikutano mbalimbali ya jamii, kupiga simu bila malipo kwa namba 0800110123 au 0766211309 (WhatsApp) , kufika moja kwa moja katika ofisi ya mahusiano iliyopo nje ya mgodi, kutuma barua kwa njia ya posta kupitia northmaragrievances@barrick.com.

Kutumia barua kwa njia ya posta  kupitia S.L.P 422 Tarime, kuweka taarifa kwenye sanduku la maoni lililopo katika ofisi za vijiji husika, kupitia kamati za kupokea na kushughulikia malalamiko zilizopo katika ofisi ya mkuu wa wilaya ya Tarime na ofisi ya mkuu wa mkoa wa Mara.

Vijiji 11 vinavyozunguka mgodi wa North Mara vitakavyofikiwa na kamati ya kusikiliza na kutatua malalamiko ni Kijiji cha Nyangoto, Mjini Kati, Matongo, Kewanja, Nyabichune, Kerende, Msege, Nyakunguru, Nyamichere, Genkuru na Nyamwaga.





No comments