DC , DMO TARIME WATINGA KITUO CHA AFYA NYANGOTO BAADA YA MALALAMIKO YA WANANCHI

>>Ni kile kituo cha afya Nyangoto maarufu Sungusungu kilichopo Nyamongo kinacholalamikiwa kwa ukiukwaji haki za afya
>> Rushwa ,chuki, visasi, huduma mbovu pasua kichwa
Na Mwandishi Wetu , Tarime
SERIKALI ya wilaya ya Tarime, mkoani Mara imesema itashughulika na watumishi wa afya wazembe, wasiofuata maadili ya utumishi huku ikiwataka wananchi wakiwemo wajawazito kutoa taarifa za kweli juu ya huduma ya afya wanayoipata ili ziweze kufanyiwa kazi.
Akizungumza Juni, 8, 2026 wakati alipokitembelea kituo cha afya Nyangoto, Mkuu wa wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele ameahidi kuwachukulia hatua wale watumishi wanakiuka taratibu za utumishi.
" Niwapongeze watoa huduma za afya kwa kazi wanayoifanya lakini najua kuna baadhi ya changamoto ndogondogo zipo. Kwa wanaoamua kuchafua nao tutashughulika nao.
" Watumishi ngazi ya afya wanatakiwa kufanya kazi kwa Waledi . Kama kuna mtumishi ana lugha mbovu kwa wananchi huyo hatufai.
" Tunachohitaji wananchi wapate huduma bora . Tunapata wagonjwa kutoka nchi za nje wanakuja kutibiwa hapa , tunataka kweli waje wakute haya kwasababu ya mtumishi mmoja ? watakuwa wanachafua taswira ya nchi " amesema DC Gowele.
DC Gowele amewaomba wananchi kutoa taarifa za kweli ikiwemo kwa viongozi serikali ya Kijiji ili huduma za afya ziendelee kutolewa inavyostahili.
" Niwaombe kama kuna mama mjamzito anatendewa ndivyo sivyo nipate taarifa mapema , wewe nipigie simu hata saa 8 usiku nitahangaika nae huyo mtu ili kuhakikisha mjamzito anahudumiwa vizuri .
" Bahati nzuri madiwani namba zao ziko wazi, viongozi wa chama ambao ndio wenye ilani kama mambo hayaendi ndivyo sivyo watachukua hatua. Sisi ni wauza duka tunatekeleza ilani kwahiyo toeni taarifa " amesema DC Gowele.
Huduma wajawazito ni bure
Mganga mkuu Halmashauri ya Wilaya ya Tarime , Amin Vasomana , amesema gharama za matibabu kwa mjamzito ni bure wakiwemo wanaojifungua na watoto.
" Gharama za mama mjamzito ni bure, tukishajua ni mjamzito tunamchukulia kwa uzito wa aina yake mpaka anajifungua. Hakuna gharama zozote kwa mjamzito " amesema Vasomana.
Marufuku kutoza kadi , kutoa kopi
Amin ameongeza kuwa kadi za kliniki kwa wajawazito na watoto ni bure " Kuna kadi za aina tatu ya mjamzito , mtoto wa kike na wa kiume . Ni vitabu , na tulishatoa maelekezo kwenye vituo vyote Kwamba vituo vyetu sasa hivi hatutumii kadi tena za kutoa copy .
" Ni marufuku kutoa kopi kadi na kama wanaendelea ndilo hilo jambo tunataka kulimaliza , hatutaki mzaa mzaaa. Msikibali kupewa kadi za copy ,tuna kadi kama vitabu hazina gharama .
Sasa hivi hakuna malipo ya taslimu mteja utalipa pesa kwa njia ya mfumo ya control namba . Hatutaki watumishi wachukue pesa mkononi .
" Mtu akikuomba pesa usimpatie nenda kalipe mwenyewe kwa kontro namba upate matibabu . Hatutegemei tuone malipo ya taslimu" amesema Amin .
Siku hiyo Juni, 8 ,majira ya saa tatu asubuhi baadhi ya ndugu waliokuwa na wagonjwa wao katika Kituo hicho cha afya Nyangoto akiwemo Ghati Marwa wanasema siku hiyo huduma ilitolewa vizuri kwani ndiyo siku aliyokuwa anawasili mkuu wa wilaya katika Kituo hicho cha afya.
" Leo huduma hapa Sungusungu ni nzuri ,tulitangaziwa kuwa anakuja mkuu wa wilaya kutembelea wagonjwa. watoa huduma wakikuona wanakuchangamkia vizuri unaulizwa unaendeleaje mama? tukusaidie nini ? .
" Yaani ukarimu huu ungekuwepo siku zote hakuna mwananchi angelalamikia kituo hiki wala kwenda kupata huduma hospitali binafsi. Tunatamani mkuu wa wilaya awe anatembelea kila mara hiki kituo maana wakijua anakuja wanatoa huduma nzuri siku hiyo utahudumiwa kama mfalme " amesema Ghati.
Mwezi Mei, 31, 2026 ,Chombo hiki cha habari kiliripoti malalamiko ya wananchi kuhusu huduma mbovu katika Kituo cha afya Nyangoto, ikiwemo vitendo vya rushwa ili kupata huduma, gharama kubwa za matibabu, wajawazito na watoto kutozwa gharama za matibabu .
Kwa undani wa makala ya malalamiko ya wananchi iliyoripotiwa katika chombo hiki cha habari, tembelea www.dimaonline.co.tz
Post a Comment