HALMSHAURI KIBAHA YATOA ZAIDI YA MILIONI 991 KWA VIKUNDI

Na Gustaphu Haule, Pwani
HALMASHAURI ya Manispaa ya Kibaha imetoa mikopo yenye thamani ya Sh. milioni 991.5 kwa vikundi 51 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ikiwa ni sehemu ya fedha za mapato ya ndani ya asilimia 10 .
Utoaji wa mikopo hiyo ni robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/2026, hatua inayolenga kuongeza fursa za kiuchumi, kupanua biashara na kupunguza umaskini kwa wananchi.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa wa kwanza kushoto, Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka wa pili kutoka kushoto,Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Mawazo Nicas watatu na wanne Naibu Meya wa Manispaa ya Kibaha Aziza Mruma katika hafla ya kutoa mikopo kwa wajasiriamali wa Manispaa ya Kibaha.Mikopo hiyo imetolewa katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ambapo jumla milioni 359 zilitolewa kwa vikundi 17 vya wanawake, Sh. milioni 557 kwa vikundi 25 vya vijana na Sh. milioni 75 kwa vikundi tisa vya watu wenye ulemavu.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini, Silvestry Koka, amesema mikopo hiyo ni nyenzo muhimu ya kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi hasa kwa kuzingatia kuwa wengi hukosa mitaji kutokana na masharti magumu ya taasisi za kifedha.
Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka akizungumza katika hafla ya kutoa mikopo kwa wajasiriamali iliyofanyika Juni 10/2026.Koka amesema kuwa Halmashauri inapaswa kuendelea kutoa mafunzo ya ujasiriamali na usimamizi wa fedha ili kuhakikisha walengwa wanatumia mikopo hiyo kwa tija na kurejesha kwa wakati.
“Wapo wananchi wenye uwezo wa kufanya biashara lakini wanakosa mtaji kutokana na kutotimiza vigezo vya mikopo ya taasisi za fedha na kupitia mikopo hii ya Halmashauri tunaendelea kufungua milango ya fursa na kupunguza umaskini kwa wananchi wetu,” amesema Koka.
Mbunge huyo amebainisha kuwa zaidi ya Sh. bilioni 4.5 ziko katika mzunguko wa mikopo iliyotolewa na Halmashauri hali inayochochea ukuaji wa biashara, kuongeza ajira na kupanua wigo wa mapato ya ndani ya Manispaa.
Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Mhe. Nickson Simon John, aliwataka wanufaika kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha na kuhakikisha mikopo hiyo inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa wa kwanza kulia akiteta jambo na Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Mawazo Nicas ( katikati) pamoja Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka wa kwanza katika hafla ya kukabidhi mikopo kwa wajasiriamali iliyofanyika Juni 10/2026.“Fedha ni kama damu katika uchumi Zinapozunguka kwa usahihi huleta uhai wa biashara, huongeza uzalishaji na kuinua maisha ya wananchi,ni muhimu mikopo hii ikatumike kwa shughuli za maendeleo badala ya matumizi yasiyo na tija,” amesema.
Awali, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha, Dkt. Rogers Shemwelekwa, amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2025/2026 Halmashauri tayari imetoa jumla ya Sh.bilioni 2.1 kwa vikundi 457 vya Wanawake,Vijana na Walemavu.
Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka (katikati) akikabidhi mfano wa hundi ya Sh.milioni 991 kwa wajasiriamali wa vikundi vya Wanawake, Vijana na Walemavu katika hafla iliyofanyika Juni 10/2026 katika Manispaa ya Kibaha .Amefafanua kuwa kati ya fedha hizo, Tsh. Bilioni 1.09 zimetolewa kwa vikundi 275 vya wanawake, Sh.milioni 904.5 kwa vikundi 161 vya vijana na Sh.milioni 158.8 kwa vikundi vya watu wenye ulemavu.
Utoaji wa mikopo hiyo unaendelea kuthibitisha dhamira ya Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha ya kutumia mapato ya ndani kuwawezesha wananchi kiuchumi, kuongeza ushiriki wao katika shughuli za uzalishaji na kujenga msingi wa maendeleo jumuishi yanayowanufaisha makundi mbalimbali ya jamii.
Baadhi ya wajasiriamali wakiwa katika hafla ya kukabidhiwa fedha za mikopo zilizotolewa na Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Juni 10/2026.




Post a Comment