HEADER AD

HEADER AD

MENEJA WA TRA PWANI AONGOZA MBIO ZA FURAHA

 
Na Gustaphu Haule, Pwani

MENEJA wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Pwani Peter Jackson ameongoza  zoezi la mbio za furaha ( Fun Run) ikiwa ni sehemu ya kuelekea katika maadhimisho ya miaka 30 ya kuanzishwa kwa TRA hapa nchini.

Mbio hizo zimefanyika Juni 27/2026 katika Manispaa ya Kibaha kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo,zikiwemo Klabu za Jogging,wafanyabiashara, baadhi ya viongozi wa Serikali,wakuu wa taasisi za Serikali na binafsi pamoja na Waandishi wa habari.

        Meneja wa TRA Mkoa wa Pwani Peter Jackson akizungumza na wadau mbalimbali waliojitokeza katika makimbio ya furaha (Fun Run) zilizofanyika Juni 27/2026 .

Mbio hizo za kilomita zaidi ya tano zilianza saa 12:30 asubuhi kutoka katika ofisi za TRA Mkoa wa Pwani kupitia Mailimoja, kuelekea barabara ya Magereza,Tanesco na kumalizia katika ofisi hiyo.

Akizungumza na wadau mbalimbali waliokusanyika katika mbio hizo Meneja wa TRA Mkoa wa Pwani Peter Jackson amesema wamefanya makimbio hayo ya furaha ( Fun Run) ikiwa ni sehemu ya kuelekea katika maadhimisho ya miaka ya 30 ya TRA yatakayofanyika Julai 1/2026.

Jackson amesema katika kipindi cha kuelekea katika maadhimisho hayo mbali na kufanya makimbio hayo lakini pia TRA Mkoa wa Pwani imefanya shughuli nyingine mbalimbali za kijamii.

        Wadau mbalimbali wakiwa na meneja wa TRA Mkoa wa Pwani Peter Jackson Juni 27/2026 mara baada ya kumalizika  kwa Jogging iliyoandaliwa na TRA.

Amesema awali walianza kufanya kongamano la wafanyabiashara na walipakodi na kisha kufanya usafi katika kituo cha Mabasi Chalinze, kuwashika mkono Mamalishe wa Chalinze kwa kuwapa vifaa mbalimbali vya kupikia na kuhifadhi chakula,na vifaa vya kuhifadhi taka,kupanda miti,na kuendesha vipindi mbalimbali katika vyombo vya habari.

Jackson amesema kuwa anajivunia miaka 30 ya TRA kwani imefanya kazi kubwa hususani katika kukusanya mapato ambayo kwa kiasi kikubwa yametumika kuwaletea Wananchi maendeleo.

Jackson amewaomba wadau kuendelea kulipakodi kwakuwa fedha zinazokusanywa matunda yake wanayaona kwani ndio zinatumika kuimarisha huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo katika elimu,afya,maji ,barabara na huduma nyingine muhimu.

       Meneja wa TRA Mkoa wa Pwani Peter Jackson ( katikati) akiwaongoza wadau kufanya mazoezi katika viwanja vya ofisi hiyo iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa Kibaha Juni 27/2026.

"Naomba nitumie fursa hii kuwaomba wadau , Wananchi na walipakodi wote wa Mkoa wa Pwani kuendelea kushirikiana na TRA kwa kuhakikisha wanalipa kodi lakini kwa wale wanaonunua bidhaa basi nao wakumbuke kudai risiti,"amesema Jackson.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara mkoa Pwani( JWT) Abdallah Ndauka ameipongeza TRA kwa kuwakusanya pamoja na kufanya jogging hiyo kwakuwa imesaidia kujenga ushirikiano kati ya TRA na walipakodi.

        Hafla ya mbio za furaha (Fun Run) iliyoandaliwa na TRA Mkoa wa Pwani Juni 27/2026.

Ndauka amesema kufanya jogging hiyo kusiwe mwisho kwani waendelee kushirikiana katika shughuli nyingine za mapato ambapo amewaomba wadau kushirikiana na TRA kwa kulipakodi  huku akiziomba taasisi nyingine kuiga mfano huo.

Nae mgeni rasmi katika mbio hizo  Lilian Shirima ambaye alimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson John amewapongeza TRA kwa kufanya Jogging hiyo muhimu sambamba na kuwapongeza walipakodi na wadau hao kwa  kujitokeza.

         Mgeni rasmi katika jogging ya TRA Lilian Shirima akizungumza na wadau mbalimbali waliojitokeza katika hafla hiyo iliyofanyika Juni 27/2026.

Shirima amewasisitiza wadau na Wananchi waliopo katika Mkoa wa Pwani kuhakikisha wanadai risiti pale ambapo wananunua bidhaa ili kuhakikisha TRA inafikia malengo ya makusanyo ya mapato.

Hata hivyo,Lilian amesema kuwa jogging hiyo imefanyika katika kuelekea kwenye maadhimisho ya miaka 30 ya kuanzishwa kwa TRA lakini amewaomba viongozi wa TRA kuendelea na mpango huo kwakuwa ni jambo zuri linalowaunganisha na walipakodi.

No comments