MILIONI 9 ZACHANGWA KUSAIDIA WATU WENYE MAHITAJI MAALUM KANISA LA SDA NYAMONGO, SERIKALI TARIME YACHANGIA MILION 3
>>Kelvin Mron atoa baiskeri 10 , Magongo, Mikongojo, Miwani, simu wezeshi
>> Aahidi Baiskeli 50
>> Diwani Kegoye ashauri itengwe asilimia moja fedha za CSR kusaidia wenye ulemavu
>> Atamani shule ya mahitaji maalum ijengwe Tarime DC
Na Mwandishi Wetu , Nyamongo
ZAIDI ya shilingi Milioni 9 na ahadi shilingi laki nane zimetolewa kwa ajili ya kusaidia watu wenye mahitaji maalum(watu wenye ulemavu wa viungo) ambapo pia wamepatiwa misaada mbalimbali zikiwemo baiskeri, Magongo, mikongojo, sabuni , miwani, simu, Biblia pamoja na nguo.
Fedha hizo zimetolewa na wadau mbalimbali katika kanisa la Waadventista Wasabato Nyamongo Kati, wakati wa ibada maalum ya watu wenye mahitaji maalum iliyofanyika Juni, 27, 2026.
Diwani wa kata ya Matongo Godfrey Kegoye aliyemwakilishi mkuu wa wilaya ya Tarime, Edward Gowele , amekabidhi Tsh. Milioni tatu (3,000,000), Diwani wa kata ya Kemambo Rashidi Bogomba amechangia Tsh. 200,000.
Diwani kata ya Matongo Godfrey Kegoye (mwenye skafu ya njano , Kelvin Mroni mwenye tisheti nyeupe wakiwa katika picha ya pamoja na watu wenye ulemavu wa kutoona (waliosimama mbele ) wakiwa wamebeba simu wezeshi.
Wengine ni Kelvin Mroni amechangia Tsh. 500,000, Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyangoto , Zakaria Machage amechangia Tsh. 300,000 ,ambao ni waumini wa kanisa la Roman Katoriki na fedha zingine zimechangwa na waumini wa kanisa la Waadventista Wasabato Nyamongo kati.
Ushauri wa Diwani Kegoye
Akikabidhi Milioni tatu kwa kanisa la Nyamongo kati , Diwani Kegoye amesema kuna haja ya kutenga fedha asilimia moja ya mapato yatokanayo na fedha za uwajibikaji wa makampuni kwa jamii , (CSR) kutoka mgodi wa dhahabu wa Barrick North Mara ili kusaidia watu wenye ulemavu wa viungo katika halmashauri hiyo ili ziweze kuwasaidia katika mahitaji yao mbalimbali.
Diwani wa Kata ya Matongo , Godfrey Kegoye akizungumza wakati alipomwakilisha mkuu wa wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele kwenye changizo kwa watu wenye mahitaji maalum.
Pia amesema kuna haja ya halmashauri ya wilaya ya Tarime kujenga shule ya msingi ya mahitaji maalum kama ilivyo halmashauri ya mji Tarime, yenye shule ya mahitaji maalum ya Magufuli.
" Sisi tuna fungu kutoka mgodini CSR , nimuombe Diwani Bogomba yeye kama Mwenyekiti wa kamati ya maendeleo ya vijiji 11 vinavyozunguka mgodi tutenge fungu la asilimia moja kutoka fedha za CSR ili ziweze kuwasaidia mara kwa mara watu wenye ulemavu.
" Pia kuna haja ya kujenga shule ya mahitaji maalum katika halmashauri ya wilaya ya Tarime, ili kuwezesha watu wenye ulemavu wa viungo kusoma . Hii itahamasisha watu wenye ulemavu kusoma kwakuwa itakuwa na mazingira wezeshi ya mahitaji maalum " amesema Godfrey.
Ameongeza kuwa Mkuu wa wilaya ya Tarime amewaagiza maafisa ustawi wa jamii na maendeleo ya jamii kuwatambua watu wenye ulemavu wa viungo ili waweze kufahamika na kutambuliwa .
Amesema baadhi ya ndugu ama familia zimekuwa zikiwaficha watoto ndani jambo ambalo linawanyima haki zao za msingi ikiwemo haki ya kupata elimu huku jamii ikihimizwa kuwapa haki za msingi watu wenye mahitaji maalum.
Kevin Mroni atekeleza ahadi
Desemba , 27, 2025 Kelvin Mroni aliyekuwa mgeni mwalikwa katika Sabato maalum ya watu wenye mahitaji maalum kanisa la Nyamongo Kati, alitoa msaada wa baiskeli moja na pesa tasilimu Tsh. 1,000,000 huku akiahidi kutoa baiskeli 10 za watu wenye ulemavu wa miguu atakazo kabidhi kanisa hilo Juni, 2026.
Kelvin ametekeleza ahadi yake kwa kutoa Baiskeli 10 kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa viungo zenye thamani ya Tsh. Milioni nne sambamba na Mikongojo 8 , Magongo jozi 12 ,Miwani ya watu wasioona 20 na simu wezeshi 10 zenye thamani ya Tsh. Milioni mbili .
Ameahidi ifikapo Juni, 2027 atatoa baiskeri 50 " Niliahidi hapa madhabahuni baiskeri 10, nimetimiza ahadi leo nakabidhi baiskeri 10. Naahidi tena mwakani mwezi kama huu nitaleta baiskeri 50 " amesema Kelvin.
Amempongeza mratibu wa kitengo cha huduma wezeshi kanisa la Nyamongo Kati ambaye ni mlemavu wa macho Bhoke Orindo , kwa kujitoa kutafuta wafadhili ili kusaidia watu wenye mahitaji maalum .
Kelvin Mroni (kushoto akizungumza, kulia ni Mratibu wa kitengo cha huduma wezeshi kanisa la Nyamongo kati, Bhoke Orindo.
" Bhoke wewe ndio nguzo ,umekuwa ukihangaika huku na kule kutafuta wadau ili kuchanga fedha kuwasaidia watu wenye uhitaji maalum . Niwaombe watu wote huduma hii ya kusaidia watu wenye ulemavu ianzie majumbani tusaidie wahitaji " amesema Kelvin.
Amewashauri watu wenye ulemavu kufanya kazi ili wajiinue kiuchumi " Hawa watu wanao uwezo , utashi , wanaweza kufanya kazi . Mbali na pesa wanahitaji ushauri wa mara kwa mara.
" Wachungaji toeni elimu kwa walemavu ya kuthubutu kufanya kazi . Nawaona hapa kuna vijana wana nguvu waonyeshwe jinsi ya kufanya kazi wawezeshwe.
" Hata kama huwezi kutembea unaweza kufanya biashara ukiwa umekaa unatuma watu wanakuzungushia mzigo wako na wakikuelewa watakufuata kuja kununua bidhaa zao . Tusikae tukijihisi sisi ni wanyonge hatuwezi kufanya kazi, hapana uwezo wa kufanya kazi tunao hata kuwa na viwanda vidogovidogo." amesema Kelvin.
Diwani Kegoye amemshukuru Kelvin Mroni kwa mchango wake wa kusaidia jamii na kusema kuwa ni mtu mwaminifu katika kanisa la Romani Katoriki , ni mtu wa kujitolea huku akimwombea kwa mwenyezi Mungu azidi kumbaliki na akakabidhi Vyeti vya pongezi kwa wadau mbalimbali ambao wamekuwa wakiwasaidia watu wenye ulemavu.
Kiongozi wa vijana kanisa la Nyamongo Kati akipanga Magongo yaliyotolewa na Kelvin Mroni kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa viungo.
Pia biblia 10 vitabu vya nyimbo 10 vimetolewa na Samwel Masabi pamoja na Keraryo Sirasi Maisa . Wadau wengine wametoa sabuni za unga huku Chama cha wanawake (Dorikasi ) kanisa la Nyamongo kati wakitoa jozi 10 za kanga.
Mch. Gadiel asema wanawatambua
Mkurugenzi wa Idara ya huduma wezeshi Jimbo la North Mara , Mchungaji Gadiel Mziray amesema kanisa limekuwa likishirikiana na kitengo cha huduma wezeshi lengo likiwa ni kuwatambua watu wenye uhitaji maalum , kujua changamoto zao na kuzitatua .
Diwani wa Kata ya Matongo Godfrey Kegoye kulia akimkabidhi Mkurugenzi wa Idara ya huduma wezeshi Jimbo la North Mara , Mchungaji Gadiel Mziray cheti cha pongezi kwa ushirikiano wake na watu wenye mahitaji maalum, kulia ni Kelvin Mroni aliyetoa misaada mbalimbali.
" Tulikuwa na mkutano wa watu wenye ulemavu , mkutano uliwezesha kugundua watu waliokuwa wamefichwa ndani . Muhubiri alikuwa kipofu alihubiri na kutembea nyumba kwa nyumba na watu 64 walibatizwa wakiwemo walemavu 3 .
" Sisi kama viongozi wa kanisa tunawatambua watu wenye mahitaji maalum na tunawatia moyo waendelee kusonga mbele tuko pamoja nao .
Amempongeza Bhoke Orindo " Bhoke sio wa kawaida Bhoke ana koneksheni yake inayotoka mbinguni ana fahamiana na watu wakubwa na watu wanatambua huduma yake .
" Tunamuombea kwa Mungu amuongezee koneksheni kubwa asisaidie tu kanisa asaidie na Serikali . Nampongeza na Zabroni , huyu anatembea Jimbo zima anafanya utambuzi wa watoto yatima " amesema Mch. Gadiel.
Mratibu wa huduma ya mahitaji maalum kanisa la Nyamongo kati, Bhoke Orindo ambaye amekuwa akitafuta wafadhili kusaidia watu wenye uhitaji maalum amewashukuru wadau wote wanaoendelea kuwashika mkono wahitaji.
Mgeni rasmi akimkabidhi Mratibu wa huduma Wezeshi Bhoke Orindo kwa mchango wake wa kuwakutanisha pamoja watu wenye uhitaji maalum pamoja na kuwasaidia misaada kupitia wafadhili mbalimbali.
Amewaomba wadau mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara, serikali kuajiri watu wenye ulemavu huku akiwataka kuwaamini wahitaji hao ikiwa ni pamoja na kuchangia biashara zao.
" Sisi kama kitengo cha huduma wezeshi kanisani tumekuwa tukiendelea kuwatambua watu wenye ulemavu ndani ya kanisa na nje ya kanisa.
Tumefanya mahubiri yaliyoendeshwa na watu wenye ulemavu lengo ni kuhakikisha watu wenye ulemavu wanamwabudu Mungu na kushiriki katika kazi za utume lakini pia kuchangamana pamoja kupitia mahubiri ya kanisani .
Bhoke amezitaja changamoto zinazokikabili kitengo cha huduma wezeshi kuwa ni pamoja na ukosefu wa fedha, miundombinu isiyo rafiki kwa watu wenye mahitaji maalum, jamii kutokuwa na uelewa wa kuthamini haki za watu wenye ulemavu.
" Kuna changamoto pia ya Biblia na vitabu kutoandikwa kwa maandishi ya nukta nundu ili kuwezesha wasiosikia kusoma ili kujijengea uelewa . Tunaomba shule za kanisa zitoe punguzo la ada kwa watoto wenye ulemavu. " amesema Bhoke.
Sheria
Sheria Na. 9 ya mwaka 2010).
Kwa mujibu wa Sheria ya Watu Wenye Ulemavu, Na. 9 ya mwaka 2010, Sura ya 183 [Marejeo ya 2023], inataja haki za watu wenye ulemavu kikiwemo kifungu cha 4, 5, 6, 15, 20, 27–31, 32–37, 38–44, na 45–49 ambavyo vinahusu usawa, kutobaguliwa, elimu, afya, ajira, huduma na ulinzi wa haki za msingi.
Kifungu cha 4 cha sheria hiyo kinaweka misingi ya msingi ya kulinda haki za watu wenye ulemavu, ikiwemo kuheshimu utu wa binadamu, kuhakikisha usawa wa fursa, kuondoa ubaguzi, kuwezesha ushiriki kamili na wenye tija katika jamii, pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa huduma na mazingira rafiki kwa watu wenye ulemavu.
Kifungu cha 5 kinaipa Serikali wajibu wa kuchukua hatua zote zinazofaa kuhakikisha haki za watu wenye ulemavu zinatekelezwa kikamilifu kupitia sera, mipango, programu na sheria mbalimbali za maendeleo.
Vilevile, Kifungu cha 6 kinakataza ubaguzi wa aina yoyote dhidi ya mtu mwenye ulemavu na kinahakikisha kuwa watu wenye ulemavu wanapata haki na fursa sawa mbele ya sheria na katika upatikanaji wa huduma zote za kijamii.
Pia, Kifungu cha 7 kinaitaka Serikali na wadau husika kuendesha elimu na uhamasishaji kwa umma ili kuondoa unyanyapaa, dhana potofu na ubaguzi dhidi ya watu wenye ulemavu na kukuza heshima kwa haki na utu wao.
Mikataba ya kimataifa
Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Watu Wenye Ulemavu (CRPD), ni mkataba mkuu wa kimataifa unaolinda haki za watu wenye ulemavu.
Ulipitishwa mwaka 2006 na kuanza kutumika mwaka 2008. Unalenga kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata haki sawa kama wengine katika elimu, afya, ajira, ushiriki wa kisiasa na ufikishaji wa huduma na mazingira.
Itifaki ya Hiari ya Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu huwapa watu binafsi au makundi haki ya kuwasilisha malalamiko umoja wa Mataifa endapo haki zao zimekiukwa. Inasaidia kusimamia utekelezaji wa mkataba mkuu.
Azimio
Azimio la Haki za Watu Wenye Ulemavu la umoja wa Mataifa lililopitishwa mwaka 1975 na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa linalenga kulinda na kutambua haki za watu wenye ulemavu duniani.


























































Post a Comment