Home
/
HABARI KITAIFA
/
USHIRIKA WA TUGEME, MWANGA WA SAMIA BUTIAMA NA NJAMA ZA KUTAKA KUPORA ARDHI YA FAMILIA YA ONAKA OBARE
USHIRIKA WA TUGEME, MWANGA WA SAMIA BUTIAMA NA NJAMA ZA KUTAKA KUPORA ARDHI YA FAMILIA YA ONAKA OBARE
>> Ushirika wa Tugeme , Mwanga wa Samia wadai kupewa ardhi na STAMICO
Na Mwandishi Wetu, Butiama
FAMILIA ya Onaka Obare wakazi wa Kijiji cha Magunga ,Kata ya Mirwa ,wilayani Butiama mkoa wa Mara, wameingiwa na sintofahamu baada ya wapangaji wao wenye mialo ya uchenjuaji wa madini ya dhahabu kitongoji cha Kitalamanka kutakiwa kuondoka katika ardhi hiyo.
Wapangaji wanadai kwamba watu kutoka ofisi ya madini mkoa wa Mara, wakiwa wameongozana na ushirika wa TUGEME na Kikundi cha Mwanga wa Samia wenye leseni ya uchimbaji wa madini, walifika na kuwataka waondoke katika ardhi hiyo bila kueleza sababu za wao kuondoka.
Victor Joseph ni mpangaji katika ardhi ya familia ya Onaka Obare anaeleza " Sisi ni wapangaji wa John Onaka ambao shughuli zetu ni uchenjuaji wa madini hapa kijijini.

Mialo ya uchenjuaji wa madini ya dhahabu katika Kitingoji cha Kitalamanka,Kijiji cha Magunga wilayani Butiama.
Hivi karibuni walifika watu wa Madini wakiwa wameongozana na baadhi ya viongozi wa ushirika wa TUGEME na Kikundi cha Mwanga wa Samia wakatupatia notisi ya mdomo kwamba kufikia tarehe 19/6/2026 tuwe tumeondoka kwenye ardhi hii.
" Hawakutuambia sababu za kuondoka ila tunasikia kwamba wanaoshinikiza tuondoke ni ushirika wa Tugeme na Mwanga wa Samia wanaomiliki leseni ya uchimbaji katika ardhi ya familia ya John Onaka, wakidai kwamba ardhi ni yao hivyo hatutakiwi kufanya shughuli yoyote ya uchenjuaji wa wadhahabu.
" Sisi ni wanachama wa kikundi cha uchimbaji wa dhahabu cha Irasanilo . Tumewekeza mitaji pale . Eneo lililokuwa limetengwa lilishajaa ndio maana tumepanga kwenye maeneo ya watu wengine" anasema Victor.
Anaongeza kusema " Tuliwahi kupeleka maombi kwa Meneja wa kikundi cha Irasanilo cha uchimbaji wa madini. Alitujibu kuwa eneo limejaa na akatuombea kwa John Onaka wakati huo RMO alikuwa anaitwa Msuya .
" Timu ikaja ikafanya savei kuona kama eneo hilo kuna vyanzo vya maji. Kuna mwalo mmoja ulibainika uko kwenye chanzo cha maji karibu na kisima cha Kijiji ukaondolewa. Sisi wengine tuliendelea na shughuli za mialao na tumekuwa tukifuata taratibu zote na kulipa kodi za serikali " anasema Victor.
Kodi zitokanazo na mialo ardhi ya Onaka
Victor aongeza kwamba wapangaji wanaomiliki mialo katika ardhi ya Onaka ni zaidi ya 30 na kwamba wamewekeza fedha nyingi katika ardhi wanayotakiwa kuondoka jambo ambalo litasababisha familia zao kuteseka lakini pia hata serikali itakosa mapato yatokanayo na mialo ya uchenjuaji wa dhahabu.
" Lundo la mchanga likishafika ukienda kulichenjua kuna tozo za serikali asilimia 9. 3 kati ya tozo hizo kuna mrabaha asilimia 7, Kodi ya TRA asilimia 2, Kodi ya ushuru wa huduma asilimia 0. 25 na asilimia 0.5 ya HIV.
" Mfano , umezalisha kwa miezi 6 Milioni 500 hapo Serikali unailipa Milioni 46.5. Tunaomiliki mialo pale kwenye ile ardhi tupo zaidi ya watu 30. Kokotoa hesabu hapo Serikali itakuwa inaingiza sh. ngapi kwa miezi 6 au mwaka ? .
" Mungu akikubaliki kwa mwaka unasomba lundo mara mbili , unaweza kuzalisha vizuri kwa mwaka serikali ikapata Milioni 90 hiyo ni kwa mtu mmoja . Ukifukuza watu 30 serikali itakuwa imepoteza Bilioni 2. 79 makusanyo kwa mwaka .
Anaongeza , hili eneo la uchimbaji wa madini hapa Buhemba linaongoza kwa ukusanyaji wa mapato. Hata kikundi cha uchimbaji cha madini cha Irasanilo kimekuwa kikipata tuzo kwa ukusanyaji wa kodi ambacho sisi pia ni wanachama wake " anasema Victor.
Mpangaji mwingine anaongeza kusema " Hao TUGEME na Mwanga wa Samia wanalalamika kwamba tunachafua mazingira kwamba mialo haitakiwi, wakati kwenye leseni zao juu ya ardhi kuna mialo ya watu nao wanachenjua lakini wao hawaguswi zaidi ya kusakama wapangaji wa John Onaka.
" Kisima chenyewe kiko mbali na mialo yetu chenyewe kiko juu mialo iko chini . Wanasema tuondoke wakati hawajatutafutia eneo lingine . Ukiangalia kule juu kuna mialo iko kwenye leseni ya Irasanilo juu kidogo kuna mlima ukisema ukaweke kule mlimani mwalo ndo hatari zaidi kuliko hapa tulipo .
" Maana kule mlimani wakati wa mvua maji yanashuka kwa wingi kuja hapa bondeni sasa hapo watakuwa bado hawajamaliza tatizo. Mi naishauri serikali watusaidie vifaa vya kisasa vya uchenjuaji ili watu wasitumie Zebaki kuchenjua dhahabu na sio kutuhamisha maana maeneo rafiki ya uchenjuaji yameisha tutaenda wapi ?" anauliza.
Familia ya Onaka yazungumza
John Onaka Obare mwenye umri wa miaka (68) msimamizi wa ardhi ya familia anasema kwamba ardhi hiyo baba yake ameimiliki tangu mwaka 1978 ,anashangaa kikundi cha TUGEME na Mwanga wa Samia kwa kushirikiana na ofisi ya madini wanawafukuza wapangaji wake wenye mialo katika ardhi ya baba yake.
" Baba alifariki mwaka 1997 aliacha ardhi yenye ukubwa wa ekari nne upande mwingine wa ardhi tumepangisha wachenjuaji wa dhahabu na eneo lingine inaishi familia.
" Nimesikia kwamba wapangaji wangu wanatakiwa kuondoka kwenye ardhi yetu tuliyowapangisha . Wanawatoa kwamba tarehe 19 mwezi huu wawe wameondoka na sababu za kuondoka hazipo. Ardhi yetu tulikuwa tunapakana na JKT wakati huo kabla ya JKT kuwakabidhi ardhi STAMICO , hii sio ardhi ya STAMICO .
" Nilipata taarifa kutoka kwa wapangaji wangu kwamba viongozi wa TUGEME na Mwanga wa Samia wamewafuata wanataka wahame " anasema John.
Anaiomba Serikali imsaidie kujua taratibu za umiliki ardhi " Mimi mwenyewe ni mgonjwa, nimeugua kwa muda mrefu tangu mwaka jana nikiwa nimelazwa hospitali huko Mwanza. Walihisi sitopona nitakufa hivyo wakaona waanzishe njama za kutaka kupora ardhi yetu .
" Serikali inisaidie kujua taratibu za umiliki ardhi maana wanasema wapangaji wahame bila hata kuniita mimi mmiliki wa ardhi wanieleze sababu za msingi za kuwahamisha .
John Onaka anasema " Sijawahi kuitwa na serikali ya Kijiji wala mtu yeyote wala ofisi ya madini zaidi tu ya kusikia wapangaji wangu wanaambiwa wahame. Wanachokifanya sio halali, ofisi ya madini waliangalie hili.
Ameongeza kusema " Zote hizi ni njama za kikundi cha Mwanga wa Samia na TUGEME ambao wanamiliki leseni ya uchimbaji. Lengo lao wanataka wachukue hii ardhi ili wao ndio wawapangishe watu wa mialo kisa tu wanamiliki leseni ya uchimbaji.
" Hao ndo wameanzisha chokochoko mara wakashtaki ofisi ya madini kwamba wapangaji wangu wanafanya shughuli za uchenjuaji karibu na vyanzo vya maji wanadhani wanaweza kumiliki na ardhi ya juu" anasema John .
Paulina Onaka anasema " Mme wangu alikufa akaniacha na watoto 12, tumeanza kuishi hapa mwaka 1979 . Mwezi huu wa sita walikuja watu watano wakasema wanataka wapangaji wangu wahame eti wanaharibu mazingira.
" Naomba serikali iniachie wapangaji wangu ,nani atanitunza na mimi ni mzee? . Hawa wapangaji ndio wananilipa kila mwisho wa mwezi sh. 30,000 . Wananiambia niondoke wakati hata barua hawajawahi kunipa " anasema Paulina.
Catherine Onaka ( 57) anasema " Mimi ni mtoto wa saba kuzaliwa, nashangaa tunatolewa kwenye ardhi ya baba yetu aliyotuachia . Hawa watu wanatumia leseni za uchimbaji kutaka kutunyang'anya ardhi .
" Ushirika wa TUGEME waliandika barua kwenda ofisi ya madini mkoa wa Mara wakilalamika uchenjuaji kwenye ardhi karibu na vyanzo vya maji japo hatupo karibu na chanzo cha maji . Walikuja viongozi wa TUGEME , watu wa Madini na kikundi cha Mwanga wa Samia na kututaka tuhame .
" Hao wamiliki wa leseni wanasema tumevamia eneo lao. Naiomba serikali itusaidie ili tusinyang'anywe maeneo maana ndiyo tunayategemea kujikimu kimaisha tunasomesha watoto. Kumiliki leseni ya uchimbaji haikuhalalishi kumiliki na ardhi ya juu lazima taratibu zifuatwe.
" Eti sisi ndio tunaambiwa tupande mboga mboga lakini ardhi zilizopo jirani yetu wao hawajaguswa hawajaambiwa waondoke ama kuambiwa wapande mbogamboga wanachenjua kama sisi huu ni ubaguzi na hii ni vita ya kimaslahi." anasema Catherine.
Sheria ya Madini
Sheria ya Madini ya mwaka 2010, Sura ya 123 Marejeo ya 2019 kifungu cha 95 kinatoa haki za umiliki wa leseni ya uchimbaji wa madini ya msingi (PML) ambapo mchimbaji ana haki ya kuingia eneo la leseni, kuchimba madini, kufanya shughuli za uchimbaji ndani ya mipaka ya leseni.
Hata hivyo kifungu cha 96 kinaeleza kwamaba Leseni si umiliki wa ardhi
Kifungu hiki kinaweka wazi kwamba
Leseni ya madini haitoi umiliki wa ardhi
inatoa tu haki za madini ndani ya eneo husika.
Hii ina maana kwamaba mtu anaweza kuwa na leseni lakini si mmiliki wa ardhi ya juu (surface land). Kifungu cha 97 kinatoa haki za mmiliki wa ardhi.
Kifungu hiko kinatambua kuwa mmiliki au mtumiaji halali wa ardhi ana haki zake
haki hizo lazima ziheshimiwe hata kama kuna leseni ya madini.
Kifungu cha 98 kinamtaka mwenye leseni kufanya makubaliano na mwenye ardhi au mtumiaji kabla ya kuanza shughuli zinazoathiri ardhi.
Wasema walipewa ardhi na STAMICO
Katibu wa ushirika wa TUGEME, Makene Sabure anasema ushirika wao ulianzishwa mwaka 2008 na kwamba wao ni wamiliki wa leseni ya uchimbaji na ardhi iliyoko juu katika eneo linalodaiwa ni la familia ya Onaka Obare na kwamba ardhi hiyo walipatiwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ambalo nao walipatiwa na Jeshi la kujenga Taifa (JKT) miaka kadhaa iliyopita.
" Mimi nimekuja hapa Buhemba mwaka 2006 chama chetu kimesajiliwa 2008 . Sisi aliyetupatia eneo ni serikali kupitia STAMICO ambao ni wamiliki wa madini na ardhi ya juu. Tulipatiwa pamoja na kikundi cha Irasanilo na Mwanga wa Samia. STAMICO walipewa ardhi na JKT miaka mingi iliyopita .
" Ili upewe ardhi ni lazima mwenye leseni alidhie . Walitupatia ardhi ya juu japo hawajatupatia hatimiliki ya ardhi, tuna leseni ya uchimbaji . Eneo linalolalamikiwa ni la STAMICO. " anasema Katibu.
Agasti , 23, mwaka 2025 ushirika wa TUGEME uliandika barua kwenda ofisi ya madini mkoa wa Mara ukilalamika watu kujenga mialo ya uchenjuaji maeneo yaliyozuiliwa na mkaguzi wa migodi Tanzania aliyetajwa kwa jina moja la Dkt. Mwanga .
Katika barua hiyo ushirika ulilalamika kuwa Dk. Mwanga alipiga marufuku watu kuweka mialo kwenye makazi ya watu na vyanzo vya maji na kwamba maeneo yaliyojengwa mialo yamo ndani ya leseni ya TUGEME ambazo ni PML Na. 2068, 2069 na 2070 huku wakisisitiza kuwa wametoa taarifa hiyo ili isijekuonekana kuwa TUGEME ndio waliruhusu mialao kuwekwa karibu na vyanzo vya maji.
Makene anasema wao ni wamiliki wa leseni hivyo taratibu zinawataka kulinda mazingira katika ardhi ya juu vikiwemo vyanzo vya maji. " Wananchi walilalamika ofisi ya madini kuwa kuna uchafuzi wa vyanzo vya maji kwanini mnaweka mialo hapa .
" Madini wakatutafuta na kutuuliza TUGEME mko wapi nani amewapangisha hawa watu? ,tukasema hapana sisi hatujawapangisha . Madini ikaunda Tume ikaja kuwaondoa watu .
" Wamekuja mwaka huu na wamewapa notisi ya siku 30 wawe wameondoka. Awali aliyekuwa afisa madini Msuya aliwaomba waondoke wakamuomba awaongezee muda " anasema Makene .
Kauli ya Mwanga wa Samia
Mwandishi aliwatafuta viongozi wa kikundi cha wachimbaji wadogo wa dhahabu Mwanga wa Samia ili kufahamu uhalalali wa ardhi inayolalamikiwa.
Katibu wa kikundi hicho Monika Mwita amesema hawezi kuzungumza, kwamba yupo Musoma anauguza mgonjwa huku akisema kwa ufupi kwamba walipewa ardhi na STAMICO.
" Niko Musoma nauguza mgonjwa siwezi kuzungumza. Sisi hatuna mgogoro na John Onaka tulipewa ardhi na STAMICO.
Serikali ya Kijiji
Mwenyekiti wa Kijiji cha Magunga Kata ya Mirwa, Togoro Juma anasema ushirika wa TUGEME na kikundi cha Mwanga wa Samia ni wamiliki wa leseni ya uchimbaji, hawamiliki ardhi ya juu na kwamba mmiliki halalali wa ardhi hiyo ni John Onaka.
" TUGEME na Mwanga wa Samia wana miliki leseni ya uchimbaji na sio umiliki wa ardhi . Mmiliki halali wa ardhi ni John kijana wa marehemu Onaka . Hao ni wageni lakini ndio wanaoleta vurugu kwa ambao wamewakuta .
" Wakati wanapewa hiyo leseni ya uchimbaji walikuta nani akiwa anamiliki ardhi kama sio John ? STAMICO walichukua maeneo ambayo yalikuwa yanamilikiwa na wananchi walikuwa wanaishi kwenye maeneo hayo .Je STAMICO walipochukua maeneo ya watu iliwafidia nini ili waondoke ili ardhi imilikiwe na STAMICO? jibu ni kwamba hawakuwalipa fidia.
" Ninachokifahamu mimi kuna maeneo yalikuwa yanamilikiwa na JKT na wakawapatia STAMICO,na kuna maeneo ambayo baada ya JKT kuondoka wananchi walijitwalia na yapo maeneo mengine ambayo ni ya wananchi hayakuwa ya JKT. " anasema Mwenyekiti.
Anaongeza " Kuna watu wanajeuri ya fedha hawataki hata kushauriwa na viongozi, wanaona wanawazidi fedha utawaambia nini. Hata ukimwendea anataka atumie fedha zake akunyanyase wewe kiongozi" anasema Mwenyekiti.
Aliyekuwa afisa madini mkazi mkoa wa Mara , Amini Msuya alipoulizwa nini anachokifahamu kuhusu shughuli za mialo ya uchenjuaji na iwapo ardhi ni ya STAMICO , amesema hawezi kusema chochote kwakuwa kwa sasa yeye si afisa madini mkoa wa Mara.
Kauli ya afisa madini Mara
Afisa Madini mkazi mkoa wa Mara Daniel Mapunda, anasema changamoto iliyopo kwenye ardhi ambayo wapangaji wametakiwa kuondoka ni changamoto ya mazingira ambapo wamiliki wa mialo ya uchenjuaji wanafanya shughuli hiyo katika maeneo ambayo si rafiki kimazingira .
" Kuna maafisa walikuja huko kwa ajili ya kutoa elimu na kuwataka watu kupisha kutoendelea na shughuli katika hilo eneo kutokana na hali ya mazingira ilivyo " anasema afisa madini.
Anaongeza, Ni maelekezo ya muda mrefu sema sikumbuki ni kiongozi gani aliacha maagizo kwa watu wa madini kusimamia maana mimi nina muda wa miezi sita tangu nihamie mkoa wa Mara.
" Hilo ni eneo ambalo liko kwenye mkondo wa maji na shughuli wanazozifanya zina riski kubwa kwasababu wanatumia kemikali ambazo ni hatari ndio maaana tunataka waondoke .
Akizungumzia kuhusu Ushirika wa TUGEME kuingilia kati kuzuia watu kuweka mialo kwenye ardhi zenye leseni zao za uchimbaji anasema ." Wanaweza kuzungumza kwasababu wana leseni ya uchimbaji. Hata wao wakiamua kuendesha shughuli za uchimbaji katika eneo hilo bado kuna mambo mengi ya kufanya kuhakikisha mazingira yanalindwa " anasema Daniel.
Je Shirika la Taifa la Madini (STAMICO) ni wamiliki halalali wa eneo hilo ambalo ushirika wa TUGEME na Mwanga wa Samia wanasema iliwamilikisha ? , afisa huyo wa madini anasema;
" STAMICO wana historia fulani kwenye hayo maeneo hadi huko wanakochimba Kikundi cha Talani, Irasanilo, Tugeme, Mwanga wa Samia kote huko ni maeneo ambayo kulikuwa na leseni iliyokuwa inasimamiwa na STAMICO, lilikuwa ni eneo tengefu walikuwa na haki zote za madini na haki ya ardhi.
Afisa madini huyo anasema kwamba ardhi ya John haitaguswa hivyo yeye aendelee kufurahia ardhi yake kwa kulima mazao zikiwemo mbogamboga , akifanya hivyo hakuna mtu atakayemgusa kwenye ardhi yake .
" Hata hawa TUGEME na Mwanga wa Samia hawawezi kuchimba kabla ya kupata kibali kwa mwenye ardhi . Sisi tunawataka watu wote wenye mialo kwenye vyanzo vya maji waondoke na si John tu ni agizo kwa watu wote wenye mialo sehemu zisizo rafiki kwa mazingira kwasababu wanatumia Zebaki.
" Zebaki ikishaingia kwenye maji haitoki leo, itakuja kuua vizazi na vizazi . Mwezi wa saba tutazunguka kutoa elimu" anasema Daniel .
Anasema uwepo wa mialo mingi kwao ni furaha kwasababu mialo ndio inazalisha dhahabu na mialo ndio inapeleka dhahabu kwenye masoko ya dhahabu .
" Ukiona tunazuia basi ujue kuna msukumo wa kimazingira ambao unapelekea sisi kufika hatua ya kuzuia . Kanuni za madini za mwaka 2010 zinatupa mamlaka ya kusimamia afya, usalama, na mazingira ya mgodi " anasema Daniel.
Sheria ya mazingira
Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004. Sheria hii imewekwa ili kuhakikisha mazingira yanatunzwa kwa maendeleo endelevu na kudhibiti uchafuzi wa mazingira.
Kifungu cha 4 kimetoa haki ya kuishi Katika Mazingira safi . Pia wananchi wana wajibu wa kulinda mazingira hayo.
Kifungu cha 106 hadi 129 kinasisitiza udhibiti wa uchafuzi wa mazingira uchafuzi wa hewa, uchafuzi wa maji,
uchafuzi wa ardhi, Kelele zisizoruhusiwa.
Sheria inatoa mamlaka kwa serikali kuweka viwango vya ubora wa mazingira.
Wasema ishu sio mazingira ni maslahi
Baadhi ya wamiliki wa mialo wanasema tatizo sio mazingira bali ni wivu wa maslahi ya kiuchumi .
" Mwandishi ishu sio mazingira, pale kuna watu wanaitamani ile ardhi ya John wanamuonea wivu kwasababu anawapangaji wanamlipa pesa . TUGEME na Mwanga wa Samia wanalazimisha kuwa eneo ni la kwao wakijua si kweli bali wanapatamani pale ili wapachukue wapangishe watu wa mialo wawe wanalipwa pesa.
" Mwandishi ili ujue pale ni maslahi ya kiuchumi yanagombewa hao TUGEME na Mwanga wa Samia wana leseni ya uchimbaji kwenye eneo lingine linalopakana na ardhi ya John ambalo nako kwenye ardhi ya juu zinafanyika shughuli za uchenjuaji wa dhahabu lakini wao hawajaguswa wala kuambiwa waondoke ila wamewashtaki tu wapangaji wa John.
" Hao Mwanga wa Samia wana leseni ya uchimbaji katika ardhi ambayo maeneo ni machafu yananuka kutokana na takataka zilizojaa bila kuondolewa na kwenye ardhi ya juu kuna watu wana mialo ya uchenjuaji wa dhahabu .
Uchafu uliokaa muda mrefu bila kuondolewa na hivyo kuwa kero kwa wananchi wanaopakana na jalala hilo.
" Sasa kama ishu ni utunzaji wa mazingira sehemu za migodi mbona zile takataka zipo muda mrefu pale hazijaondolewa na pembeni yake kuna watu wana chenjua dhahabu ? lakini hao Mwanga wa Samia wako kimya hawasemi kitu badala yake wanakomaa na ardhi ya John Onaka, hao ni wadanyanyifu wanataka kupora ardhi ya John kwa kisingizio cha utunzaji wa mazingira " anasema Mmiliki mmoja wa mwalo.
Baadhi ya vikundi vimekuwa vikianzishwa na kusajiliwa kwa majina ya viongozi wakubwa wa kitaifa wakiwemo marais ili kupata umaarufu lakini pindi vinavyopoingia migogoro na jamii heshima ya majina hayo ya viongozi wa kitaifa hushuka na kusababisha uhasama .
Katiba ya Jamhuri
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977, Kifungu cha 24 kinazungumzia Haki ya kumiliki mali
Kifungu cha 24(1) kinasema ,kila mtu ana haki ya kumiliki mali kisheria na kulindwa dhidi ya mtu au mamlaka yoyote kuingilia mali yake bila sababu ya kisheria.
Kifungu cha 24(2) kinasema hakuna mtu atakayenyang’anywa mali yake isipokuwa kwa mujibu wa sheria na kwa masharti ya kulipwa fidia ya haki, na
fidia hiyo kulipwa kwa wakati unaofaa.
Azimio
Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu (UDHR, 1948) Ibara ya 17 linasema kila mtu ana haki ya kumiliki mali peke yake au kwa pamoja. Hakuna mtu atakayenyang’anywa mali yake kiholela.
Ardhi ya mtu haiwezi kuchukuliwa bila sababu ya kisheria na fidia ya haki.
Azimio la Umoja wa Afrika – African Charter on Human and Peoples’ Rights (1981), Ibara ya 14 inalinda Haki ya kumiliki mali . Mali haiwezi kuchukuliwa isipokuwa kwa maslahi ya umma na kwa kufuata sheria. Ibara ya 21 Watu wana haki ya kutumia rasilimali zao za asili.
Mikataba ya kimataifa
Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR, 1966) Ibara ya 17 unasema mtu hatakiwi kuingiliwa katika mali, nyumba au maisha yake binafsi kwa njia isiyo halali.
Ibara ya 2(3) inasisitiza mataifa lazima yahakikishe watu wana njia ya kupata haki pindi haki zao zinapovunjwa.
Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiuchumi, Kijamii na Kiutamaduni (ICESCR, 1966) Ibara ya 11 inasema kila mtu ana haki ya kiwango cha maisha cha kutosha, ikiwemo makazi, chakula, maisha bora.





Post a Comment