LAMECK AIRO NA RAFIKI ZAKE WATOA MILIONI SABA KAMA MOTISHA KWA WALIMU SHULE YA SEKONDARI NYANDUGA -RORYA
>> Ni baada ya matokeo mazuri kidato cha sita
>>112 wapata daraja la kwanza, tisa daraja la pili, hakuna daraja la 3, 4, 0
Na Mwandishi Wetu, Rorya
MBUNGE mstaafu jimbo la Rorya,mkoani Mara, Lameck Airo kwa kushirikiana na marafiki zake wamekabidhi Tsh. Milioni 7.1 kama motisha kwa walimu wa shule ya sekondari Nyanduga iliyopo wilayani Rorya baada ya kufanya vizuri kimkoa matokeo ya kidato cha sita.
Katika matokeo ya mtihani wa Taifa wa kidato cha sita mwaka 2026, wanafunzi 112 kati ya wanafunzi 121 wamepata Daraja la Kwanza na wanafunzi 9 wamepata Daraja la Pili. Hakuna aliyepata daraja la tatu, la nne au sufuri.
Lameck ameupongeza amewapongeza walimu kwa jitihada zao za ufundishaji pamoja na bodi ya shule ambayo imekuwa karibu na uongozi wa shule hiyo katika usimamizi ili kuhakikisha wanafunzi wanajikita katika masomo.
" Shule za wilaya ya Rorya zimefanya vizuri. Nawapongeza walimu, bodi ya shule kwa kusimamia vyema kuhakikisha wanafunzi wanasoma na kufanya vizuri katika mitihani yao bila kuwasahau wazazi na wanafunzi hongereni sana .
" Shule zikifanya vizuri mnakuwa mmeitangaza vizuri wilaya ya Rorya . Mjiandae kuja kupokea wanafunzi wengi maana naamini kwa matokeo haya mazuri yatakuwa chachu kwa wanafunzi wengine kuja kusoma hapa Nyanduga " amesema Lameck.
Amewapongeza marafiki zake ambao wameweza kuchangia fedha ili kuwapa morari ya kazi walimu huku akiiasa jamii na uongozi wa shule hiyo kusaidia wanafunzi masikini ili waweze kusoma bure kwani baadhi wanashindwa kuendelea na masomo kutokana na ukosefu wa fedha ikiwemo michango ya shule.
Mkuu wa shule hiyo, Peter Chota, amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano wa karibu kati ya walimu, wanafunzi na wazazi, pamoja na nidhamu, kujituma katika masomo na kuweka mazingira bora ya kujifunzia.
Diwani wa Kata ya Koryo, Wilaya ya Rorya mkoani Mara, Daniel Omolo amesema kuwa ataendelea kuwekeza zaidi katika kuboresha elimu ya msingi ili kuweka msingi imara wa kitaaluma kwa wanafunzi kabla ya kujiunga na shule za sekondari.
Omolo amesema kuwa maendeleo ya elimu huanza katika ngazi ya msingi, hivyo ni muhimu kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunzia, walimu wanapatiwa ushirikiano, na miundombinu ya shule inaendelea kuboreshwa ili kuongeza kiwango cha ufaulu.
Ameeleza kuwa uwekezaji katika elimu ya msingi utasaidia kuwajengea wanafunzi uwezo mzuri wa kusoma, kuandika na kuelewa masomo mbalimbali, jambo litakalowawezesha kufanya vizuri zaidi wanapoendelea na masomo ya sekondari.
Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Rorya mkoani Mara kimepongeza uongozi, walimu na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Nyanduga kufuatia kufanya vizuri katika matokeo ya mtihani wa Kidato cha Sita mwaka 2026.
Chama hicho kimesema mafanikio yaliyopatikana ni matokeo ya ushirikiano kati ya walimu, wanafunzi, wazazi pamoja na wadau wa elimu, huku kikibainisha kuwa ufaulu huo unaendelea kuiweka shule hiyo katika nafasi nzuri ya kitaaluma ndani ya wilaya na mkoa.
Pia kimewataka walimu na wanafunzi kuendelea kudumisha nidhamu, kujituma katika masomo na kuweka malengo makubwa zaidi ili kuongeza kiwango cha ufaulu katika miaka ijayo.
Chama hicho kimewahimiza wazazi na jamii kuendelea kushirikiana na shule katika kuboresha mazingira ya kujifunzia, kikieleza kuwa elimu bora ni msingi muhimu wa maendeleo ya Taifa na ustawi wa jamii.
Kwa mujibu wa matokeo ya NECTA ya Kidato cha Sita (ACSEE) 2026 na orodha za viwango vya shule, katika mkoa wa Mara, shule ya sekondari Mkono imeshika nafasi ya kwanza kimkoa ambapo shule ya Sekondari Nyanduga imeshika nafasi ya 2 .
Shule iliyoshika nafasi ya tatu ni shule ya sekondari Kasoma, nafasi ya nne shule ya sekondari Bunda na nafasi ya tano shule ya sekondari Chief Ihunyo.

Post a Comment