HEADER AD

HEADER AD

MASAUNI ARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI MIRADI YA KIMKAKATI ILIYOTUMIA FEDHA ZA MAPATO YA NDANI KIBAHA


Na Gustaphu Haule, Pwani

WAZIRI wa Nchi ,Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Hamad Masauni ameridhishwa na utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha kwa kutumia fedha za mapato ya ndani.

Masauni ameridhishwa na miradi hiyo 
mara baada ya kuitembelea, kukagua na kuifungua ukiwemo mradi wa Kituo cha Biashara cha ATN kilichopo Kata ya Picha ya Ndege pamoja na  mradi  wa Shule ya Msingi ya Mchepuo wa Kiingereza Mwambisi iliyopo Kata ya Kongowe .

Masauni ametembelea miradi hiyo Julai 20/2026 ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi  ya siku moja aliyoifanya katika Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha akiwa ameambatana na viongozi mbalimbali wa chama na Serikali.

             Waziri wa Nchi,Ofisi ya makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Hamad Masauni ( Mwenye shati nyeupe Kulia) akiweka jiwe la Msingi katika kituo cha biashara cha ATN kilichopo Kata ya Picha ya Ndege Manispaa ya Kibaha.

Akizungumza na wananchi katika eneo la Kituo cha Kibiashara cha ATN, Masauni amesema Manispaa ya Kibaha imebahatika kupata viongozi wazuri hususani Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa ndio maana miradi mingi inatekelezwa kwa ubora na viwango vinavyotakiwa .

Masauni amesema kuwa mradi wa kituo cha Biashara cha ATN  utachochea ukuaji wa uchumi wa eneo hilo kwa kuongeza ajira kwa vijana, kupanua fursa za biashara na kuimarisha ujasiriamali.

Amewaomba vijana wa Manispaa ya Kibaha kuacha kulalamika na badala yake wajitokeze kutumia fursa zinazotolewa na Serikali hususani kituo cha biashara cha ATN kwakuwa kituo hicho kimejengwa mahususi kwa ajili ya Vijana.

        Wananchi wa Mtaa wa Mwambisi wakiwa katika hafla ya ufunguzi wa Shule ya Msingi yenye mchepuo wa Kiingereza Mwambisi katika Manispaa ya Kibaha .

Masauni amesema kuwa Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imejipanga kuhakikisha inaendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji wa viwanda na hata utoaji wa mikopo ya asilimia 10 lengo ni kuhakikisha vijana wanapata ajira na hata kujikwamua kiuchumi.

"Nawapongeza Manispaa ya Kibaha kwa kutumia Vizuri fedha za mapato ya ndani kutekeleza miradi ya maendeleo lakini lazima tuwapongeze viongozi wa Manispaa akiwemo Mkurugenzi Dkt.Rogers Shemwelekwa na Mbunge kwa kazi nzuri wanayoifanya,"amesema Masauni.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dkt. Rogers Shemwelekwa amesema kuwa mradi wa Kituo cha Kibiashara cha ATN unagharimu zaidi ya Sh.milioni 534 na kwamba hadi sasa zimetumika  Sh. milioni 292.4 .


       Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa kituo cha biashara cha ATN kwa Waziri wa Muungano na Mazingira Hamad Masauni katika ziara iliyofanyika Julai 20/2026.

Mradi wa ATN unajumuisha vyumba 9 vya biashara,eneo la Kuoshea magari ,Karakana ya magari pamoja na ufyatuaji wa matofali ambapo kukamilika kwake kutaiwezesha Manispaa ya Kibaha kupata mapato ya Sh.milioni 270 kwa mwaka fedha ambazo zitaenda kuboresha mapato ya Manispaa na hata kuboresha maisha ya Wananchi wa Kibaha.

Shemwelekwa amesema kuwa  utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 85 na ukimalizika unatarajia kuwanufaisha vijana 150 kupitia ajira na kujiajiri, wafanyabiashara watakaopanga fremu za maduka pamoja na wamiliki wa magari watakaotumia huduma za gereji zitakazojengwa katika kituo hicho.

Amesema kituo hicho kitatumika kama eneo maalum la kuwakwamua vijana kiuchumi kwani watakuwa wanapata mafunzo mbalimbali ya kijasiriamali na kwamba vijana hao watakuwa wanaingia katika hicho kwa awamu.


"Hiki ni kituo cha kuwanoa vijana kibiashara kwani vijana watakuwa wanapita hapa kufundishwa mambo mbalimbali ya kiuchumi na hata ujasiriamali na pale ambapo wanafanikiwa wanaondoka na kuletwa wengine,lengo letu ni kuhakikisha vijana wa Manispaa wanapata mafanikio kupitia kituo hiki," amesema Shemwelekwa.

Kuhusu shule ya Msingi ya Mchepuo wa Kiingereza Mwambisi,Dkt .Shemwelekwa Shule hiyo  imejengwa kwa kutumia Sh.milioni 404.6 za mapato ya ndani ambapo  kupitia fedha hizo, Halmashauri imejenga jengo la utawala, vyumba saba vya madarasa pamoja na matundu 18 ya vyoo, hatua inayolenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuongeza upatikanaji wa elimu bora kwa watoto wa Manispaa ya Kibaha.

      Sehemu ya kituo cha Biashara cha ATN kilichowekwa jiwe la Msingi Julai 20/2026 na Waziri Hamad Masauni.

Dkt.Shemwelekwa, amesema Halmashauri itaendelea kutumia mapato ya ndani kutekeleza miradi yenye tija kwa wananchi ili kuboresha huduma za kijamii na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.

Hata hivyo , Shemwelekwa amesema mafanikio ya utekelezaji wa miradi hiyo ni matokeo ya usimamizi mzuri wa mapato ya ndani na dhamira ya Halmashauri ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora zinazokidhi mahitaji yao.
      Shule ya mchepuo wa Kiingereza Mwambisi iliyopo Kata ya Kongowe Manispaa ya Kibaha.


No comments