HEADER AD

HEADER AD

WAFANYABIASHARA WAIPONGEZA MANISPAA KIBAHA KUTUMIA VIZURI FEDHA ZA MAPATO YA NDANI KUTEKELEZA MIRADI YA MAENDELEO

>> Ni zile zilizotekeleza miradi ya maendeleo

>>  Wafurahia uongozi wa Mkurugenzi wa halmashauri Dkt. Rogers Shemwelekwa 

>> Makusanyo ya mapato ya ndani yaongezeka kutoka Bilioni 5.2 hadi Bilioni 26

 Na Gustaphu Haule, Pwani

WAFANYABIASHARA na wawekezaji waliopo katika Manispaa ya Kibaha wameupongeza uongozi wa Manispaa hiyo chini ya Mkurugenzi Dkt.Rogers Shemwelekwa kwa namna ambavyo wanatumia vizuri fedha za mapato ya ndani kutekeleza miradi ya maendeleo.

Pongezi za wafanyabiashara hao zimetolewa katika mkutano wa wafanyabiashara na viongozi wa Manispaa uliofanyika Julai 15,2026 katika Chuo cha uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo kwa mfipa Kata ya Kibaha.

       Wafanyabiashara wa Manispaa ya Kibaha katika mkutano wa pamoja na viongozi wa Manispaa hiyo uliofanyika katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kibaha kwa Mfipa.

Lengo la mkutano huo ilikuwa ni kufanya tathmini ya ukuaji wa biashara katika Manispaa ya Kibaha kwa mwaka 2025/2026  kupokea changamoto za wafanyabiashara pamoja na kuweka mipango ya utekelezaji wa kibiashara katika msimu wa mwaka mpya wa fedha 2026/2027.

Wamepongeza hatua hiyo mara baada ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa kutoa mada na kuwaeleza kiwango cha makusanyo ya Mapato ya ndani na mchanganuo wa matumizi ya fedha hizo katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo tangu alivyoteuliwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha.

Katika mada yake, Dkt.Shemwelekwa amewaeleza wafanyabiashara hao kuwa zaidi ya asilimia 60 ya makusanyo ya Mapato ya ndani yanakwenda katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na hadi sasa kila Kata imefanikiwa kupata mradi.

     Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa akizungumza na wafanyabiashara katika mkutano uliofanyika Julai 15,2026 katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kibaha kwa Mfipa


Ametaja baadhi ya miradi ambayo imetekelezwa kwa mapato ya ndani kuwa ni pamoja na ujenzi wa Shule za msingi zenye mchepuo wa Kiingereza zilizojengwa katika Kata mbalimbali kwa fedha za  mapato ya ndani, Zahanati na ujenzi wa baadhi ya madarasa ya shule za Sekondari.

Amesema mapato ya ndani yamesaidia kujenga vituo vya Kibiashara katika Kata ya Picha ya Ndege,Kata ya Mkuza na Kata ya Kongowe lakini bado mipango inafanyika kuhakikisha kila Kata kunajengwa vituo vya biashara ( Business Center).

Shemwelekwa amewaeleza wafanyabiashara hao hali ya makusanyo ya Mapato ya ndani kwa kipindi cha miaka minne ambapo hatahivyo aliwashukuru kwa namna ambavyo wamekuwa wakijitoa kuchangia mapato hayo kwani bila wao ni wazi kuwa miradi hiyo isingeweza kutekelezwa.

Amesema mwaka 2021/2022 bajeti ya makusanyo ya Mapato ya ndani ilikuwa Tsh.Bilioni 5.2 lakini makusanyo yalifikia kiasi cha TSh.Bilioni 5.3, na mwaka 2023/2023 bajeti ilikuwa TSh.Bilioni 5 lakini makusanyo yalikuwa Tsh. Bilioni 5.3 wakati 2023/2024 bajeti ilikuwa Tsh. Bilioni 7,lakini makusanyo yalikuwa Tsh.Bilioni 7.5.

Amesema mapato hayo yameendelea kupanda kwani katika kipindi cha mwaka 2024/2025 bajeti ya Halmashauri ilikuwa kiasi cha Sh.bilioni 10.6 lakini makusanyo yalifikia kiasi cha Tsh. Bilioni 21.2 na mwaka 2025/2026 bajeti ilikuwa zaidi ya bilioni 13 lakini makusanyo yakapanda hadi Tsh. Bilioni 26.

Amesema kutokana na kuongeza kwa makusanyo ya Mapato ya ndani anataka kuona Manispaa ya Kibaha inapanuka kuwa kama Kariakoo na hivyo kuwajenga wafanyabiashara kuingia katika soko la ushindani.

Shemwelekwa amewaeleza wafanyabiashara hao kuwa wakati anaingia Kibaha alikuta watu zaidi ya 100,000 na sasa Kibaha ina watu zaidi ya 300,000 na hiyo inaonyesha namna Kibaha inavyokua Kibiashara.

Amesema kutokana na hali hiyo anataka Kibaha hiwe ya kibiashara kwakuwa ni lango la biashara kwahiyo ni muhimu kwa wafanyabiashara kufanya tathmini ya biashara yake inavyoweza kuendelea wakati Serikali ikiendelea kuweka mazingira mazuri ya kibiashara na uwekezaji.

Pamoja na hayo lakini pia mkurugenzi huyo amewafundisha wafanyabiashara hao mbinu mbalimbali za kuendelea biashara zao ikiwa pamoja na kuangalia soko la wateja, kutumia vizuri Mamlaka za  kisheria zinazosimamia biashara.

         Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Dkt . Rogers Shemwelekwa akizungumza katika mkutano wa wafanyabiashara uliofanyika Julai 15/2026 katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kibaha kwa Mfipa.

Pia ,katika mkutano huo aliweka bayana fursa  katika sekta ya viwanda ambazo kila mfanyabiashara na mwekezaji anaweza kuzitumia ambapo amesema katika kipindi cha mwaka 2021/2026 sekta ya viwanda imeongeza.

Amesema mwaka 2021 Kibaha ilikuwa na viwanda 65 hadi viwanda 163 kwa mwaka 2026 ambapo katika viwanda hivyo vikubwa 75, vya kati 58 ,viwanda vikubwa vinavyoendelea kujengwa 21 na viwanda vya kati tisa lakini pia ongezeko la wafanyabiashara ni kubwa kutoka 3,727 mwaka 2023 hadi kufikia wafanyabiashara 14,131 Juni 2026.

Amesema Kibaha bado kuna maeneo mengi ya uwekezaji na tayari Halmashauri imetenga maeneo kwa ajili ya viwanda katika eneo la Zegereni Kata ya Visiga zaidi ya ekari 1,036,Kata ya Mbwawa ekari 2,309,Kata ya Pangani ekari 189.6, na Kata ya Misugusugu ekari 111.3.

Amesema pia , Serikali inaendelea kufikiria namna ya kuwasaidia wafanyabiashara kukuza bidhaa zao na kwamba hatahivyo kwa upande wa watoa huduma wa nyumba za kulala wageni kama vile Lodge na Hoteli Manispaa inajipanga kutoa mafunzo maalum ili kusudi waweze kutoa huduma nzuri kwakuwa wanaopoteza wateja kwakushindwa kutoa huduma nzuri.

Kutokana na mada ya Mkurugenzi huyo baadhi ya wafanyabiashara walifurahi kuona namna ambavyo Manispaa imekuwa na mipango mizuri ya kuwainua wafanyabiashara na hivyo kumpongeza Mkurugenzi pamoja na uongozi mzima wa Manispaa hiyo.

Secilia Mague mfanyabiashara kutoka Sagale Magengeni amesema anampongeza Mkurugenzi wa Manispaa kwa kazi kubwa anayoifanya kwakuwa ameweka wazi namna ambavyo mapato yao yanatumika.

Mague amesema hali hiyo inawavutia wafanyabiashara kuendelea kulipa tozo mbalimbali kwakuwa anajua wanapolipa kuna uhakika wa moja kwa moja kwenda kutekeleza miradi ya maendeleo yenye faida kwa Wananchi wa Manispaa na Taifa kwa ujumla.

Nae Mohamed Lutambi (Lipwai) mfanyabiashara wa simu katika Kata ya Mailimoja amempongeza Mkurugenzi kwa Manispaa pamoja na Meya wa Manispaa ya Kibaha kwa kazi nzuri ya kufufua matumaini ya wafanyabiashara.

      Wafanyabiashara wa Manispaa ya Kibaha katika mkutano na viongozi wa Manispaa hiyo uliofanyika Julai 15/2026.

Lipwai amesema jambo la Manispaa kufanya mkutano na wafanyabiashara na kusikiliza kero na changamoto zao ni jambo muhimu na nzuri ambapo ameshauri mikutano kama hivyo ni vyema ikafanyike angalau mara mbili kwa mwaka ili kusaidia kujenga uelewa kwa wafanyabiashara wa Manispaa.

Kwa upande wake meneja Raslimali Watu kutoka kiwanda cha Keds Eric Rwekaza amefurahishwa na namna ambavyo Manispaa inafanyakazi vizuri kupitia mkurugenzi huyo lakini ameomba changamoto zinazowakabili zifanyiwe kazi.

Rwekaza amesema kuwa changamoto kubwa inayowakabili ni suala la kukatika umeme mara kwa mara jambo ambalo linaathiri uzalishaji kiwandani hapo , ukosefu wa maji na kuwepo kwa barabara mbovu inayopelekea magari ya mizigo kukwama hususani katika kipindi cha mvua.

Amesema anaomba Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha kuhakikisha inafuatilia ili kuweza kutatua changamoto hizo na hivyo waweze kuzalisha katika mazingira mazuri yatakayosaidia kuchangia mapato ya ndani kirahisi zaidi.

Hata hivyo, mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa wa Pwani ( JWT) Abdallah Ndauka amepongeza uongozi wa Manispaa ya Kibaha na Mkurugenzi wake kwa namna ambavyo wanajitoa kuhakikisha wanaweka mazingira mazuri ya wafanyabiashara.

Ndauka ,amesema pamoja na jitihada hizo lakini bado kuna gepu kati ya Halmashauri na wafanyabiashara hasa katika masuala ya kisheria ambapo ameomba pale ambapo wanatunga Sheria basi waone namna ya kuwashirikisha wafanyabiashara ili nao wachangie mawazo yao.


No comments